1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

9 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBHM

BAGHDAD-Cheney awasili Iraq

Makamu wa Rais wa Marekani Dick Cheney amewasili mjini Baghdad katika ziara ya ghafla.

Balozi wa Marekani nchini Iraq ,Ryan Crocker amewaambia waandishi wa habari kuwa makamu huyo wa Rais amewasili nchini humo ili kuhimiza maridhiano baina ya vikundi vya kidini vinavyohasimiana, na kulishauri bunge la Iraq , kusitisha mapumziko ya miezi miwili kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.

Pia Balozi Crocker amesema Bwana Cheney anatazamiwa kutia mkazo ushirikiano zaidi katika vita dhidi ya ugaidi, na kwamba jeshi la Marekani pekee halitoweza kukamilisha lengo hilo.

Makamu huyo wa Rais wa Marekani anatazamiwa kukutana na wakuu wa serikali ya Iraq baadaye hii leo.

Wakati huo huo watu 12 wameuawa katika mlipuko wa bomu katika mji wa Arbil nchini humo.

Imeripotiwa watu kadhaa kujeruhiwa katika mlipuko huo kaskazini ya Iraq.

GAZA-Johstone bado ashikiliwa Gaza

Kikundi cha wapiganaji wa kiislam kinachojiita Jeshi la Kiislam ,kimesema kimethibitisha kumshikilia mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji la Uingereza BBC, Alan Johnston ambaye ametoweka wiki nane zilizopita.

Taarifa kupitia njia ya tovuti iliyotolewa leo na kikundi hicho, kikundi hicho kimedai hakitamuachia mwandishi huyo wa BBC; hadi pale wapiganaji wake wanaoshikiliwa kama wafungwa , watakapoachiwa huru.

Sauti za msemaji wa kikundi hicho ilipatikana kupitia mtandao unaotumiwa na kundi la kigaidi la Al Qaida na vikundi vingine vya kiislam.

Katika mtandao huo ilionekana picha ya mwandishi huyo wa BBC pamoja na kitambulisho chake cha kazi.

BERLIN-EU yamtaka Wolfowitz kujiuzulu

Nchi za ulaya zinazidi kutia Shinikizo zaidi kumtaka Rais wa benki ya Dunia Bwana Paul Wolfowitz, kujiuzulu.

Mwakilishi wa benki hiyo nchini Ujerumani Bwana Eckhard Deutscher , amepata muongozo kutoka Berlin, unaomtaka kuungana na mapendekezo ya Bodi ya benki hiyo dhidi ya Wolfowitz.

Nchini Marekani Mwenyekiti wa kamati ya huduma za bunge Bwana Barney Frank ,amesema juhudi za Benki hiyo kufikia malengo ya kupiga vita umasikini chini ya Wolfowitz , hazitafanikiwa.

Bodi hiyo imethibisha Mkuu huyo wa Benki ya Dunia kupatikana na makosa kadhaa, ikiwemo kumpandisha cheo kinyume na utaratibu mpenzi wake anayefanya kazi katika taasisi hiyo nyeti ya fedha duniani.

Ingawa Bwana Wolfowitz ameahidi kuendelea na wadhifa wake , Bodi inatazamiwa kutoa uamuzi wake mapema wiki hii endapo Mkuu huyo wa Benki ya Dunia ataendelea na wadhifa huo.

DILI-Duru ya pili ya uchaguzi leo , Timor ya mashariki

Duru ya pili ya uchaguzi wa Urais inafanyika leo Timor ya mashariki .

Mshindi wa tuzo ya amani , Hosee Ramos Horta anapamabana na mgombea wa chama tawala Franswaar Guatteres katika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Mwezi uliopita katika duru ya mwanzo, hakuna aliyepata wingi mkubwa wa kura´ili kuweza kupata ushindi wa moja kwa moja.

Kiasi cha raia laki tano wana wajibu wa kushiriki katika uchaguzi wa leo.

Hali ya ulinzi imeimaimarishwa kufuatia hofu za kuwepo ghasia kwa wafuasi wa mgombea atakayeshindwa.

Mwaka mmoja uliopita, mapambano yalizuka kati ya makundi hasimu ya jeshi na polisi. Katika mapigano hayo watu 37 walipoteza maisha na wengine wapatao 150,000 waliyahama makazi yao.

Rais anayemaliza muda wake Shanana Gushmao amewataka wapiga kura kukubali matokeo ya uchaguzi wa leo ili kuimarisha amani katika taifa hilo.

WASHINGTON-Clinton na azindua mapambano ya ukimwi

Rais wa zamani wa Marekani , Bill Clinton amezindua makubaliano mapya pamoja na makampuni ya madawa ili kupunguza bei ya dawa za UKIMWI.

Bwana Clinton amesema nia ya makubaliano hayo ni kupunguza asilimia 25 hadi asilimia 50, ili kuwasaidia wagonjwa wa UKIMWI na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI:

Dawa hizo zitatumiwa kwa wagonjwa ambao miili yao kwa sasa haikubaliani tena na mchanganyiko wa dawa za hapo awali.

Bwana Clinton ameongeza matumaini kutokana na utumiaji wa dawa hizo kwa kusema zinasaidia kurefusha maisha ya waathrika endapo muhusika atafuata masharti yaliyowekwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Rais huyo wa zamani wa Marekani, kiasi cha watu milioni saba katika mabara ya Afrika, Asia, na Latin Amerika wanahitaji kupatiwa dawa hizo.

BERLIN-Nchi za Afrika haifaidiki na kufutiwa misaada

Mawaziri wakuu wa nchi za Niger na Togo wamesema msaada wa kuondolewa mzigo wa madeni umeshindwa kutanzua tatizo la Umasikini.

Viongozi hao wametoa mwito kwa mataifa tajiri yaliyoendelea kiviwanda , kuweka vitega uchumi barani Afrika ili nchi masikini zinufaike na utajiri wa malighafi zake.

Waziri Mkuu wa Niger Hama Amadou akizungumza mjini Berlin katika maandalizi ya mkutano wa kilele wa nchi tajiri za G-8, amesema msamaha wa madeni nchini mwake haukusaidia kuondosha umasikini.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Bi. Angela Merkel amesema suala la misaada kwa bara la Afrika litapewa kipaumbele katika mkutano wa G-8 utakaofanyika mwezi June mjini Hailigen-dam.Ujerumani.

Katika mkutano wa nchi hizo mwaka 2005 uliofanyika Scotland ,nchi 18 zilizo masikini kabisa duniani , zilisamehewa madeni ya Euro bilioni 30.

RIYADH-Steinmeier akamilisha ziara nchi za ghuba

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani , Frank Walter Steinmeier amekamilisha ziara yake ya mashariki ya kati, kwa kukutana na baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba(AGCC) mjini Riyadh Saudi Arabia.

Bwana Steinmeier amesema nchi za kiarabu pamoja na zile za umoja wa ulaya zina nafasi nzuri ya kuboresha sekta ya biashara baina yao kupitia biashara huru.

Mazungumzo hayo yayohusisha biashara kati ya nchi za Umoja wa ulaya na nchi za ghuba, yaligubikwa na hofu kuhusu mpango wa amani wa mashariki ya kati.

Waziri wa kigeni wa Saudi Arabia , mwana wa Mfalme, Saud Al Faisal ,amesema majadiliano hayo ya amani yako katika hali nzuri.

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema anaunga mkono juhudi zinazoongozwa na nchi za kiarabu , kutoa uwezekano kuitambua rasmi Israel pindi nchi hiyo itakapoondoka katika maeneo iliyoyavamia mwaka 1967, na pia kukubali haki ya wakimbizi wa kipalestina kurejea makwao.

BRASILIA-Papa awasili Brazil

Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Benedikt wa 16, hii leo anatazamiwa kuanza ziara ya kwanza nchini Brazili , nchi ambayo ina waumini wengi wa madhehebu ya kanisa hilo.

Katika ziara hiyo ya siku tano atafungua mkutano wa maaskofu wa Latin Amerika na Caribean.

Kwa waumini wengi na watafiti wa masuala ya kidini , wanasema kazi kubwa kwa baba mtakatifu ni kurudisha imani miongoni mwa waumini wa madhehebu hayo.

NAIROBI-Kibaki atangaza siku ya maombolezo

Rais Mwai Kibaki wa Kenya ametaitangaza siku ya Jumatau ijayo kuwa siku ya maombolezo ya Kitaifa ,kufuatia ajali ya ndege ya shirika la Kenya , iliyotokea huko nchini Cameroun.

Timu ya waokoaji inajitahidi kusaka na kutambua mabaki ya miili ya wahanga wa ajali ya ndege ya shirika la Kenya , iliyoanguka nchini Cameroun mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ndege hiyo ilianguka katika eneo chepechepe muda mfupi baada ya kuondoka katika uwanja wa ndege wa Doula nchini Cameroun, ikielekea Nairobi Kenya.

Kazi ya kutafuta mabaki ya wahanga hao inazidi kuwa ngumu, baada ya ndege hiyo kutumbukia katika eneo hilo la matope .

Hadi sasa miili ya watu 28 imepatikana miongoni mwa watu 114 wanaosadikiwa kupoteza maisha katika ajali hiyo.

Kisanduku cheusi cha ndege hiyo bado kinafanyiwa uchunguzi na wataalam wa masuala ya anga wa nchi za Kenya na Cameroun.

ABUJA- wanne washikiliwa Niger Delta

Wafanyakazi wanne wa makampuni ya mafuta wanashikiliwa na kikundi cha watu wasiojulikana katika jimbo la uzalishaji wa mafuta la Niger Delta.

Taarifa kutoka katika eneo hilo zinasema miongoni mwa wafanyakazi wanne wanaoshikiliwa mateka , watatu ni raia wa Marekani.

Hatua hiyo imefuatia masaa machache baada ya wafanyakazi 11 kutoka Korea na Ufilpino kuachiwa huru.

Hapo jana kundi la wapiganaji la MEND, lilithibitisha kuhusika na ulipuaji wa mabomba ya mafuta katika eneo hilo.

Vikundi vya wapiganaji katika eneo hilo la Delta vimekuwa vikitaka mgawanyo wa faida , kutokana na uchimbaji wa mafuta katika eneo hilo.

Kwa mwaka huu pekee , takribani wafanyakazi 100 wa kigeni wameshikiliwa na vikundi hivyo.

KABUL-21 wauawa Afghanstan

Majeshi ya muungano na Marekani yamewaua raia 21 katika shambulizi la angani kusini mwa Afghanstan.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa gavana wa jimbo la Helmand, Asadullah Wafa, amesema vifo zaidi vimetokea katika miji ya Sangin, ambapo vikosi vya jeshi la Muungano vinapambana na wanamgambo wa kundi la Taleban.

Kwa mujibu wa Gavana huyo , wengi wa wahanga katika shambulio hilo ni wanawake na watoto.

Lakini jeshi la Muungano limekanusha taarifa hiyo na kusema hakuna raia aliyeuawa, ila limekiri kupoteza mwanajeshi wake mmoja.

Jeshi la muungano limekuwa likilaumiwa kuteketeza raia wasiokuwa na hatia , linapofanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Taleban, nchini Afghanstan.