1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

2 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBHN

ANKARA-Erdogan ataka uchaguzi wa haraka

Waziri mkuu wa Uturuki Tayyip Erdowan , ametoa wito kufanyika uchaguzi wa mapema ili kuondoa hali ya mvutano wa kisiasa iliojitokeza hivi karibuni nchini humo.

Waziri Mkuu Erdowan amesema hayo baada ya mahakama ya katiba kutengua uchaguzi wa Rais Ijumaa iliyopita, ambapo chama tawala cha AK, kilitoa mgombea pekee katika uchaguzi huo,Bwana Abdullah Gul.

Erdowan pamoja na chama chake cha AK wanalaumiwa na wafuasi wa vyama vya upinzani na wale wasio wafuasi wa dini ya kiislam, kuwa na ajenda ya siri ya kuligeuza taifa hilo kuwa la kiislam.

Wapinzani wamesema wanakusudia kupeleka shauri katika mahakama ya katiba nchini humo, kuzuia Bwana Gul , kugombea katika uchaguzi huo.

Bunge la Uturuki linakutana hii leo na huenda likaidhinisha kufanyika uchaguzi huo June 24, mwaka huu.

WASHINGTON-Bush apiga turufu

Rais George Bush amezuia muswaada unaolenga kuyaondoa mapema majeshi ya Marekani nchini Iraq.

Rais Bush amesema muda wa kuyaondoa majeshi ya Marekani katika muswaada ulioidhinishwa na bunge la Congress lenye wabunge wengi kutoka chama cha Demokratik, utaweka mazingira magumu kwa makamanda walio katika uwanja wa mapambano nchini Iraq.

Amesema pia mpango huo utapeleka ujumbe tofauti kwa wanajeshi pamoja na magaidi.

Hata hivyo Rais Bush amesema atakutana na viongozi wa bunge la Congress kufikia muafaka baadaye hii leo.

KHARTOUM-UN yashutmu

Umoja wa mataifa umeshutumu kitendo cha hivi karibuni cha kutekwa nyara kwa wafanyakazi sita wa mashirika ya misaada katika eneo lenye mapigano la Darfur.

Mratibu wa shirika la misaada la Umoja wa mataifa, Manuel Aranda Da Silva, ameonya kuendelea kwa vitendo hivyo kutaathiri kazi za shirika lake, kuwahudumia wakimbizi katika eneo hilo.

Wafanyakazi hao sita wa shirika hilo la misaada la Umoja wa mataifa , walishikiliwa na kundi la watu wasiojulikana katika eneo la Um Shalaya, magharibi ya Darfur.

Hata hivyo wafanyakazi hao waliachiwa baadaye katika sehemu ya jangwa na kuokolewa na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.

JERUSALEM-Wito kumtaka Olmert ajiuzulu waongezeka

Shinikizo la kumtaka Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert kujiulu limeingia katika sura mpya baada ya Waziri wake wa mambo ya nje kuungana na umma kumtaka Bwana Olmert kuachia ngazi.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Israel Bi.Tzipi Livni, akihojiwa katika runinga moja nchini humo, amesema ni wajibu wa Waziri Mkuu huyo kuitika wito wa wananchi.

Hapo jana Waziri asiyekuwa na wizara maalum kutoka chama cha Labour, Eitan Cabel, alitangaza kujiuzulu ikiwa ni hatua ya kuipinga serikali ya Bwana Olmert.

Bwana Olmert anatazamiwa kufanya kikao maalum cha baraza la mawaziri hii leo kutathmini mapendekezo ya tume maalum ya uchunguzi wa vita ya Lebanon mwaka jana.

Olmert mwenyewe amekiri kufanya makosa kuamuru majeshi ya Israel kuivamia Lebanon kwa lengo la kuwaokoa askari wawili wa jeshi lake , wanaoshikiliwa na kundi la Hezbollah.

Katika vita hiyo, wanajeshi zaidi ya 100 wa Israel waliuawa ,huku raia takribani 1000 wa Lebanon wakipoteza maisha.

BAGHDAD-Iraq kuchunguza kuuawa kwa Al Masri

Vikosi vya usalama vya Iraq vimesema vinachunguza taarifa ya kuuawa kwa kiongozi wa kundi la Al Qaida nchini humo Abu Ayyub Al Masri.

Al Masri anadaiwa kuuawa hapo jana katika mapigano kati ya kundi la Al Qaida na vikundi vya makabila.

Katika mkutano na waandishi wa habari Msemaji wa serikali Ali Al Dabaga alisema Iraq itafanya uchunguzi wa kina juu ya kifo cha kiongozi huyo wa Al Qaida

.

Kundi la Al Qaida nchini linalaumiwa kudidimiza hali ya usalama nchini Iraq, toka Marekani ilipoivamia kijeshi mnamo mwaka 2003.

HAVANA-Kukosekana kwa Castro kwawatia hofu Wacuba

Kukosekana kwa kiongozi wa Cuba Fidel Castro katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi hapo jana , kumezusha hofu juu ya mustakabali wa kiongozi huyo .

Mamia ya maelfu ya wananchi mjini Havana walimiminika kwa wingi kuadhimisha sherehe za siku ya wafanyakazi wakiwa na matumaini ya kumuona Bwana Castro.

Fidel Castro ambaye alikuwa akiugua kwa muda mrefu , alitazamiwa kuhudhuria katika sherehe hizo za jana , baada ya kupata nafuu.

Castro ambaye ana umri wa miaka 80, hajaonekana hadharani kwa takribani miezi tisa hivi sasa , toka alipoanza kuugua mwaka jana.

TOKYO-Korea Kaskazini yapewa muda zaidi

Marekani imetoa muda zaidi kwa Korea ya Kaskazini kutekeleza mapendekezo ya mwezi February juu ya kuangamiza silaha zake za kinyuklia .

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleeza Rice hata hivyo amesema subira ya ulimwengu haina mwisho juu ya suala hilo.

Bi Rice amesema anatambua juhudi za Pyongyang kutekeleza mapendekezo ya Mwezi February.

Korea ya Kaskazini awali ilikataa kuendelea na mpango huo wa kuangamiza silaha zake za kinyuklia ,hadi itakaporejeshewa fedha zake dola milioni 25 zilizoshikiliwa katika benki ya Macau nchini China.

CAIRO-Iran yasema haitazungumza na Marekani

Irani imefifisha matumaini ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani , katika mkutano wa kutanzua mzozo wa Iraq , unaonza leo katika mji wa kitalii wa Sherm El Sheikh, nchini Misri.

Taarifa hiyo ya Iran imetolewa kufuatia kauli ya hivi karibuni ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi.

Condoleeza Rice, kuwa Marekani bado haijaamua endapo itazungumza na ujumbe wa Iran juu ya tofauti ya nchi hizo mbili.

Iran imesema inashiriki katika mkutano huo kujaribu kurejesha hali ya amani nchini Iraq.

Mkutano huo utayahusisha pia baadhi ya mataifa kadhaa ya mashariki ya kati .

KIEV- Jaji mwingine atimuliwa Ukraine

Rais Viktor Yushenko amemfukuza kazi jaji mwingine wa mahakama ya katiba nchini humo.

Hatua hiyo ya Rais Yushenko imekuja siku mbili baada ya kuachishwa kazi kwa jaji mwingine wa mahakama hiyo.

Uamuzi huo wa Yushenko, huenda ukazidisha shinikizo la kisiasa nchini humo.

Rais Yushenko alitangaza kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mwingine mwezi uliopita, hatua iliyopingwa vikali na wabunge pamoja na Waziri Mkuu Viktor Yanukovich.

Waziri Mkuu Viktor Yanukovich amefungua kesi katika mahakama ya katiba kupinga uamuzi huo wa Rais.

Wakati huo huo serikali ya Ukraine imemuhakikishia Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleeza Rice kuwa Ukraine itaendelea kufuata mkondo wa demokrasia.

BAMAKO-Wapinzani wapinga uchaguzi Mali

Viongozi wa upinzani nchini mali wameupinga uchaguzi wa Rais mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo Rais wa sasa Amadou Toumani Toure, ameibuka na ushindi.

Katika taarifa yao ya pamoja hii leo, viongozi wa vyama vinne vya siasa nchini humo , wamesema uchaguzi wa April 29, haukuwa huru na kweli.

Wafuasi wa Rais huyo wamedai Bwana Toure amepata zaidi ya asilimia 70 ya kura, katika asilimia 60 ya vituo vya kupigia kura.

Toure alichukua madaraka baada ya kuipindua serikali ya kiimla mwaka 1991, na kisha kurejesha utawala wa kiraia na kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2002.

KAMPALA-Brigedia Mayombo afariki

Mmoja wa maafisa wakuu wa jeshi la Uganda , ambaye pia alionekana kama mrithi wa Rais Yoweri Museveni , amefariki dunia.

Afisa huyo Brigedia Noble Mayombo mwenye umri wa miaka 42, amefariki wakati akipatiwa matibabu mjini Nairobi nchini Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa serikali Ofwono Opondo, zinasema kuwa Brigedia Mayombo kutokana na utendaji wake mzuri kama Katibu Mkuu wa wizara ya ulinzi na katika jeshi, alikuwa na uhusiano wa karibu na Rais Yoweri Museveni.

Marehemu Brigedia Mayombo alikuwa akikabiliwa na matatizo ya kupooza.