1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

22 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCYp

Rais wa Mamlaka ya Wapelestina Mahamoud Abbas hapo jana amekuwa na mazungumzo na kiongozi wa kikundi cha Hamas aliye uhamishoni Khaled Meshaal, ambapo wamesema kuwa wamepiga hatua kubwa kuelekea muafaka juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja.

Katika mkutano huo uliyofanyika mjini Damascus Syria, hakukuweza kufikiwa mara moja maridhiano ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini viongozi hao wanatarajiwa kuendelea na mazungumzo hayo mnamo wiki mbili zijazo.

Katika taarifa yao viongozi hao wamesema kuwa hawaungi mkono mapigano na uhasama kati ya vyama vya Hamas na Fatah.

Pande hizo mbili zimekuwa katika jitihada za kuunda serikali ya umoja kwa miezi kadhaa sasa, ili kupata misada ya fedha kutoka Marekani na umoja wa ulaya iliyositishwa.

Katika hatua nyingine mkuu wa siasa za nje katika Umoja wa Ulaya, Javier Solana amesema kuwa , ameona kuna mwamko wa kisiasa katika mashariki ya kati kufufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Solana aliyasema hayo jana mjini Jerusalem baada ya mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.

Mapema alikuwa mjini Amman kukutana na Mfalme Abdullah wa Jordan ambaye alimweleza kuwa umoja wa Ulaya una wajibu wa kuunga mkono juhudi za kufufa mazungumzo ya amani katika mashariki ya kati.