1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

13 Juni 2008

Wapiga kura katika Jamhuri ya Ireland wanaelekea wameukataa mkataba wa Ulaya uliopitishwa katika mkutano wa viongozi mjini Lisbon.

https://p.dw.com/p/EJMY

Mkondo wa uamuzi wa wapiga kura kuukataa mkataba huo, ulianza kujitokeza baada ya kupatikana matokeo kutoka karibu robo tatu ya majimbo 43, yakiipa ushindi kambi ya wanaoupinga mkataba huo .

Inaelekea mkataba huo umepingwa zaidi katika maeneo ya mashambani na ya watu wa tabaka la wafanyakazi.

Waziri wa sheria Dermot Ahern alikiri kwamba inaelekea kambi ya hapana imepata ushindi katika kura hiyo ya maoni. lakini alielezea wasi wasi wake kwamba Jamhuri ya Ireland inaelekea kwenye dharuba ikiwa itaikataa katiba hiyo yenye lengo la kuweka utaratibu wa maamuzi katika umoja wa ulaya wa wanachama 27 .

Mfanyabiashara tajiri Declan Ganley , kiongozi wa kundi linalojulikana kama LIBERTAS lililoongoa kampeni ya kuupinga mkataba huo alisema ni siku ya"kujivunia mno kwa umma wa Ireland." Itakumbukwa kwamba mkataba wa ulaya wa hapo awali ulipingwa pia katika kura ya maoni nchini Uholanzi na Ufaransa miaka mitatu iliopita kabla ya kufanyiwa marekebisho na kuzaliwa mkataba mpya wa Lisbon.

Wapiga bila shaka waligawanyika. Mmoja wao aliyeiunga mkono katiba hiyo alisema,"Nilipiga kura ya ndiyo. Niliuangalia waraka na niliona mabadiliko katika mkataba wa Lisbon yana maana."

Ama mwengine aliyeupinga alikua na sababu kuwa,"Nilipiga kura ya hapana kwa sababu sikuuelewa awaraka wenyewe-Ni hivyo, kama huufahamu unapaswa kupiga kura ya hapana."

Jamhuri ya Ireland ni mwanachama pekee wa umoja wa ulaya kuitisha kura ya maoni juu ya mkataba huo. Hadi sasa nchi 18 zimeshauidhinisha mkataba huo katika mabunge yao ya taifa, mkataba ambao ulipangwa kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka ujao 2009 baada ya kuidhinishwa na nchi zote 27 wanachama.

Hivi sasa kutokana na matokeo ya kura hiyo ya maoni katika Jamhuri ya Ireland, ina maana mkataba huo hauwezi kuanza kazi.

Bunge la uhispania linatarajiwa kuuidhinisha mkataba huo kabla ya mwisho wa mwezi huu. Pamoja na hayo Waziri mkuu wa Poland Donald Tusk amesema kupingwa mkataba huo na wapiga kura wa Ireland hakutouhujumu mkataba huo. Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zinatarajiwa kutangaza kwamba zitaendelea na hatua za kuuidhinisha sawa na Jamhuri ya Cheki na Sweden

Viongozi wa umoja wa ulaya watakutana mjini Brussels wiki ijayo na wanatarajiwa kuitaka Ireland ifafanuwe jinsi inavyopanga kuendelea mbele.