1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

13 wauwawa katika mapambano Misri

4 Januari 2014

Watu 13 wamepigwa risasi na kufariki wakati waungaji mkono wa kundi la Udugu wa Kiislamu walipopambana na polisi nchini Misri jana(03.01.2014) Ijumaa, wakipinga ukandamizaji dhidi ya kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1Al9R
Ägypten Proteste 3.1.2014
Maandamano yaliyomwaga damu mjini CairoPicha: Virgine Nguyen Hoang/AFP/Getty Images

Kundi hilo linaloelemea katika nadharia za dini ya Kiislamu linapinga kuondolewa kwa rais Mohammed Mursi kutoka madarakani mwezi Julai mwaka jana limekuwa likifanya maandamano ya karibu kila siku, hata baada ya serikali inayoungwa mkono na jeshi kutangaza kuwa kundi la Udugu wa Kiislamu ni kundi la kigaidi wiki iliyopita, na kuongeza adhabu dhidi ya upinzani.

Ukandamizaji waongezeka

Serikali inatumia sheria mpya kuwakamata mamia ya waungaji mkono wa kundi hilo la Udugu wa Kiislamu. Maelfu zaidi, ikiwa ni pamoja na viongozi wa ngazi ya juu wa kundi hilo, wako kizuwizini kwa muda wa miezi kadha, wakikamatwa baada ya jeshi kuchukua madaraka.

Ägypten Proteste 3.1.2014
Maandamano yakiendelea mjini CairoPicha: Reuters

Ukandamizaji huo umepunguza lakini hakusitisha kabisa uwezo wa kundi la Udugu wa Kiislamu kuhamasisha maandamano. Kwa hivi sasa limekuwa likitegemea wanafunzi kuendeleza hali ya mapambano dhidi ya kile inachokiona kuwa ni serikali ya mapinduzi inayoitawala Misri.

Katika wilaya ya mjini Cairo ya Nasr City, polisi wa kutuliza ghasia wakivalia mavazi ya kujikinga na risasi walifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji ambao walikuwa wakirusha fashifashi na mawe. Mapambano kama hayo yalizuka nchi nzima, kama ambavyo imekuwa ni jambo la kawaida kila baada ya swala ya Ijumaa , siku ambayo ni ya mapumziko nchini Misri.

Risasi za moto zatumika

Wizara ya afya imesema kuwa watu watano wameuwawa katika wilaya mbali mbali mjini Cairo. Duru za usalama zimesema wamefariki kutokana na majeraha waliyoyapata baada ya kupigwa risasi.

Ägypten Proteste 3.1.2014
Magari ya deraya mitaani mjini CairoPicha: Reuters

Mmoja kati ya watu hao watano alikuwa mtu ambaye alipigwa risasi na waandamanaji baada ya kuwatolea matusi waandamanaji wa kundi la Udugu wa Kiislamu wakati wakipita nje ya nyumba yake, duru zimesema.

Muandamanaji mmoja na mwanamke wamepigwa risasi na kufariki katika mji wa pwani wa Alexandria , zimesema duru za hospitali na usalama. Haikufahamika wazi iwapo mwanamke huyo alikuwa mmoja kati ya waandamanaji ama ni mtu aliyekuwa kando akishuhudia maandamano hayo.

Watu hao wawili walipigwa risasi na polisi katika mji ulioko katika eneo la mfereji wa Suez wa Ismailia, baada ya maandamano yaliyoanzia katika msikiti baada ya swala ya Ijumaa, zimeeleza duru za hospitali.

Katika jimbo la Fayoum, kusini magharibi mwa Cairo, waandamanaji watatu , ikiwa ni pamoja na mwanafunzi , wamefariki kutokana na majeraha waliyoyapata baada ya kupigwa risasi , afisa wa wizara ya afya wa eneo hilo Medhat Shukri ameliambia shirika la habari la Reuters.

Mwanafunzi mwingine wa chuo kikuu alipigwa risasi na kufariki wakati wa mapambano katika mji wa kusini wa Minya. Wizara ya afya imesema jumla ya watu 58 wamejeruhiwa nchini kote.

Ägypten Studenten Protest Al-Azhar Universität Kairo 27. Dez.
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Al-Azhar wakiandamana mjini CairoPicha: Reuters

Polisi imewakamata watu 122 wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu kwa kuwa na silaha , wizara ya mambo ya ndani imesema katika taarifa. Kundi la Udugu wa Kiislamu limesema kuwa wafuasi wake hawana silaha.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Amina Abubakar