1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

15 Wakamatwa kabla kuapishwa al-Sissi Jumapili

7 Juni 2014

Polisi ya Misri imewakamata waungaji mkono 15 wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi kabla ya sherehe za kuapishwa kwa rais mteule Abdel Fattah al-Sissi kesho Jumapili(08.06.2014).

https://p.dw.com/p/1CEA1
Fattah al-Sisi
Abdel Fattah al-Sissi rais mteule wa MisriPicha: Reuters

Watu hao waliokamatwa wanahusiaka katika chama kilichopigwa marufuku cha Mursi cha Udugu wa Kiislamu na wanadaiwa kuwa walikuwa wanapanga mashambulizi dhidi ya sherehe za ushindi wa al-Sissi, limeeleza gazeti la serikali al-Ahram jana Ijumaa (06.06.2014). Watu hao wamekamatwa katika mji wa pwani wa Alexandria, ripoti hiyo imeeleza.

Maelfu ya waungaji mkono wa Mursi wamekamatwa tangu Julai mwaka jana wakati jeshi lilipomuondoa madarakani kufuatia maandamano makubwa ya umma dhidi ya uongozi wake wa mwaka mmoja.

Ägypten Abdel Fattah al-Sisi Präsidentenwahl Bekanntgabe der offiziellen Ergebnisse 03.06.2014
Abdel Fattah al-Sissi mkuu wa Zamani wa jeshi la MisriPicha: picture-alliance/dpa

Al-Sissi, ambaye aliongoza kuondolewa kwa Mursi, anatarajiwa kuapishwa kesho Jumapili (08.06) katika mahakama kuu ya katiba mjini Cairo.

Rais wa Iran pia amealikwa

Misri imewaalika viongozi kadhaa , ikiwa ni pamoja na Rais wa Iran Hassan Rowhani, kuhudhuria kuapishwa kwa kiongozi huyo wa zamani wa jeshi.

Viongozi wa Saudi Arabia, Kuwait na Bahrain, ambao ni waungaji mkono wakubwa kifedha wa Misri baada ya kuondolewa kwa Mursi, wanatarajiwa kuhudhuria.

Ägypten Wahlen im Mai
Picha za al-Sissi katika uchaguzi wa mwezi Mei nchini MisriPicha: picture-alliance/dpa

Serikali za mataifa ya magharibi, ambazo zimekuwa mara kwa mara zikielezea wasi wasi wao juu ya kipindi cha mpito cha kisiasa nchini Misri, zinatarajiwa kutuma wawakilishi wao.

Al-Sissi ameshinda kwa asilimia 97 katika kura zilizopigwa katika uchaguzi ulioshirikisha wagombea wawili mwezi uliopita.

Ägypten Proteste Anhänger Muslimbrüder 18.8.2013
Waungaji mkono wa kundi la Udugu wa KiislamuPicha: picture-alliance/dpa

Waungaji wake mkono wanamuona kuwa ana uwezo wa kumaliza mvutano ambao umeikumba Misri katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Ameapa katika mahojiano ya hivi karibuni katika televisheni kuwa kundi la Udugu wa Kiislamu halitakuwa hai katika kipindi chake cha utawala, na kuchochea uvumi wa ukandamizaji mkubwa kuhusu usalama dhidi ya kundi hilo lenye umri wa miaka 86.

Uchumi wa Misri

Wakati huo huo washauri kutoka mataifa ya magharibi wanatayarisha mipango ya kuunda upya uchumi wa Misri, duru zimeeleza , huku rais mteule Abdel Fattah al-Sissi akitoa baraka zake, na ambaye hadi sasa amezungumzia tu juu juu hadharani juu ya kuufufua uchumi wa nchi hiyo.

Ägypten Wahlen 26.05.2014
Jeshi la MisriPicha: Reuters

Msukumo nyuma ya mradi huo wa ushauri ni Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, ambayo pamoja na Saudi Arabia na Kuwait zimeimiminia Misri mabilioni ya dola kama msaada tangu al-Sissi kuliondoa kundi la Udugu wa Kiislamu madarakani mwaka jana, duru zinazofahamu juu ya zoezi hilo na wafanyabiashara wameliambia shirika la habari la Reuters.

Wakati Misri ikijitayarisha kumuapisha kiongozi wake wa nne tangu mwaka 2011, sehemu kubwa ya msaada wa Marekani unaofikia kiasi ya dola bilioni 1.5 utaendelea kuzuiwa huku kukiwa na hofu kuwa taifa hilo linarejea katika ukandamizaji.

Lakini ikijizuwia kumkaribisha al-Sissi kuwa ni hatua ya kuelekea uthabiti, baadhi ya wadadisi wanaitaka Marekani kufikiria upya mpango wake wa miongo kadha wa msaada wa kwa jeshi la Misri kutokana na wasi wasi kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa haki za kiraia.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef