1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

200,000 wamekimbia mapigano Libya

5 Machi 2011

Vikosi vinavyomuunga mkono kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi viliendelea na mapigano hapo jana.

https://p.dw.com/p/10TqV
Wahamiaji wanakimbilia Tunisia na MisriPicha: DW

Waasi wamesema wameudhibiti mji ulio na kampuni ya kusafisha mafuta, Ras Lanuf, katika mapigano makali ya uasi huo yaliosababisha vifo vya watu wengi, tuhuma ambazo afisa mmoja wa serikali amezikanusha. Mapiganao hayo yalionekana kuthibitisha mgawanyiko nchini humo kati ya eneo la magharibi karibu na mji mkuu Tripoli, linalodhibitiwa na vikosi vya Gaddafi, na mashariki kunakodhibitiwa na waasi hao.

Unruhen in Libyen Dossierbild 1
Picha: AP

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa

Wakati huohuo, Kanali Gaddafi amemchagua aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Libya kuwa mjumbe wake nchini Marekani, na kuchukuwa nafasi ya aliyekuwepo ambaye alijitenga na utawala wake. Umoja wa mataifa unasema serikali ya Gaddafi inaomba mwanadiplomasia mkuu wa Libya, Ali Abdussalam Treki aidhinishwe kuwa mwakilishi mpya wa Libya wa Umoja wa mataifa. Msemaji mmoja wa katibu mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-moon, hapo jana alisema kuwa ofisi ya mkuu huyo ilipokea barua ya pili ya kutaka balozi Mohamed Shalgham na naibu wake Ibrahim Dabbashi waondolewe mamlaka ya kidiplomasia. Wote walijitenga wazi na Gaddafi kufuatia hatua ya kiongozi huyo dhidi ya waandamanaji waliomtaka aondoke madarakani.

DOSSIER komplettes Bild Libyen März 2011
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: picture alliance/dpa

Wakati huo huo mashirika ya kutoa misaada yanasema idadi ya watu wanaoikimbia Libya kutafuta hifadhi nchini Tunisia na Misri, imezidi laki mbili tangu kuanza machafuko mnamo tarehe 15 mwezi Uliopita. Hali inasemekana kuimarika kiasi, lakini serikali za nje zinahofia kuwa huenda idadi hiyo ikapindukia iwapo mapigano yatazidi Libya. Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa msaada wa kibinaadamu Kristalina Georgieva anasema vifaa vya usaidizi vinapungua na kwamba hali ni mbaya. Alisema pia wataalamu wa Umoja wa mataifa hawajafanikiwa kufika katika mji mkuu Tripoli. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Philip J Crowley, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ndege mbili za usafiri za jeshi la Marekani, zilituwa nchini Tunisia hapo jana, zikiwa zimebeba maji, mablanketi na vifaa vingine vya usaidizi, kwa watu hao walioyakimbia mapinduzi.

Tangu siku ya Alhamisi, Umoja wa Ulaya umekuwa ukiratibu mpango mkubwa wa usaidizi kwa wakimbizi katika mpaka wa Tunisia na Libya. Ndege ya kimataifa inawasafirisha maelfu ya wakimbizi kutoka eneo la Djerba nchini Tunisia. Mataifa ya Umoja wa Ulaya, zikiwemo Ujerumani, Uhispania, Italia na Ufaransa, zinatuma ndege na meli za ziada.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Afpe/
Mhariri:Grace Patricia Kabogo.