1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

27 wauawa katika mripuko wa bomu Baghdad

26 Desemba 2011

Mshambuliaji wa kujitoa mhanga ameua watu watano kwenye wizara ya mambo ya ndani katika mji mkuu wa Irak Baghdad, wakati mgawanyiko wa kimadhehebu ukizidi kupanuka. Watu makumi kadhaa wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/13ZHW
Mashambulizi mjini Baghdad yameongezeka katika siku za hivi karibuni
Mashambulizi mjini Baghdad yameongezeka katika siku za hivi karibuniPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa maelezo ya maafisa wa wizara ya mambo ya ndani iliyoathiriwa na mripuko huo asubuhi leo, mripuaji alilifuata gari la mafundi wa umeme walipofunguliwa mlango kuingia ndani ya jengo la wizara, na kutumia nafasi hiyo kuliingiza gari lake lililotegeshwa mabomu, na kisha akayaripua. Watu watano walikufa na wengine 27 walijeruhiwa. Mripuko wa leo unafuatia wimbi la miripuko mingine iliyolikumba jiji la Baghdan Alhamisi iliyopita na kuuua watu 60.

Machafuko katika mikoa mingine ya Irak yaliua watu saba, na kufiisha idadi kubwa ya vifo tangu mwezi Agosti.

Irak imenasa katika mzozo wa kimadhehebu; serikali inayodhibitiwa na washia imetoa hati ya kukamatwa kwa makamu rais Tareq al Hashemi ambaye ni msuni, kwa shutuma kwamba anaendesha genge la wauaji. Al Hashemi amekanusha shutuma hizo. Waziri mkuu Nuri al Malik pia ametoa wito wa kutimliwa kazi naibu wake pia wa kisuni Saleh al Mutlak, ambaye amesema waziri mkuu huyo ni mbaya kuliko Saddam Hussein.

Kundi la al Hashemi na al Mutlak la Iraqiya ambalo linaungwa mkono na wasuni limesusia vikao vya baraza la mawaziri na bunge. Tareq al Hashemi ambaye anapewa hifadhi katika nyumba ya wageni wa rais wa Irak Jalal Talabani katika jimbo lenye mamlaka ya ndani la wakurdi, jumapili aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba hana mpango wa kwenda mbele ya mahakama mjini Baghdad, na kuzusha hisia kwamba ananuia kuikimbia nchi.

Makamu Rais wa Irak Tareq el Hashemi ambaye ametolewa hati ya kukamatwa
Makamu Rais wa Irak Tareq el Hashemi ambaye ametolewa hati ya kukamatwaPicha: picture-alliance/dpa

Alisema kukataa kwake kwenda Baghdad ni kwa sababu za kiusalama, akisema kwamba walinzi wake wote wamekamatwa. Al Hashemi alisema vyombo vya sheria vya Irak vinafanya kazi chini ya ushawishi wa serikali na hilo ni tatizo kubwa kwa nchi. Aliongeza kuwa amekimbilia katika eneo la wakurdi kwa sababu huko mahakama haziwezi kutumiwa kisiasa.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema kuwa Tareq al Hashemi hawezi kufukuzwa iwapo atatafuta hifadhi nchini humo, lakini akasema anapaswa kusalia nchini mwake. Al Hashemi mwenyewe alisema hakusudii kutoka ndani ya Irak isipokuwa tu pale atakapohisi kuwa uhai wake uko hatarini.

Waziri Mkuu wa Irak Tareq al Maliki
Waziri Mkuu wa Irak Tareq al MalikiPicha: picture-alliance/dpa

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden amewapigia simu mara nyingi viongozi wa Irak wiki iliyopita, akiwataka kumaliza tofauti zao kwa amani. Jumamosi alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu Nuri al Maliki, na baadaye Jumapili akaongea na kiongozi wa maeneo ya wakurdi Massoud Barzani, na kuahidi msaada wa Marekani katika kuanzisha mazungumzo ya viongozi wa Irak.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri:Yusuf Saumu