1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

28 wauawa shambulizi la Misri

Lilian Mtono
26 Mei 2017

Washambuliaji waliokuwa na silaha na kujifunika nyuso zao wamelishambulia basi lililokuwa limewabeba waumini wa Kikristu wa madhehebu ya Koptiki waliokwenda kuzuru makao ya watawa yaliyopo Kusini mwa Misri Ijumaa hii

https://p.dw.com/p/2deLu
Ägypten Polizist vor der koptischen Kirche in Tanta
Picha: Reuters/M. Abd El Ghany

Wengi wa wahanga wa shambulizi hilo ni watoto. 

Kulingana na taarifa zilizotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Misri, washambuliaji hao waliokuwa kwenye gari aina ya Pick up walilishambulia basi hilo lililokuwa limebeba wageni waliokuwa wakielekea kwenye makao ya watawa ya Mtakatifu Samuel katika mkoa wa Minya, umbali wa kilomita 200 kutoka mji wa Cairo, kabla ya kukimbia.

Rais Abdel Fattah al-Sisi aliitisha kikao cha maafisa wa usalama, na baraza la mawaziri limesema washambuliaji hao hawatafanikiwa kuligawa taifa. 

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulizi hilo ambalo limekuja katika mkesha wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Limekuwa ni tukio la karibuni zaidi la kuwashambulia waumini wa madhehebu ya Koptiki baada ya mashambulizi yalilofanywa na kundi la jihadi linalojiita Dola la kiislamu, IS kwenye makanisa matatu mnamo mwezi Disemba na Aprili na kuua Wakristu wengi.

Viongozi wa Kiislamu wamelaani mauaji hayo. Imam mkuu wa kituo cha al-Azhar Ahmed al-Tayeb amesema shambulizi hilo lilikuwa na nia ya kuidhoofisha nchi. Mufti mkuu wa Misri Shawki Allam amewaita washambuliaji hao kuwa ni wasaliti.

Picha za basi zilizorushwa na kituo cha televisheni cha serikali zimeonyesha gari hilo likiwa limeshambuliwa vibaya na risasi za bunduki za rashasha na madirisha yakiwa yamevunjwa kwa risasi. Kituo hicho kimewanukuu maafisa wa wizara ya afya waliosema idadi kubwa ya wahanga ni watoto. 

Ägypten Hunderte Kopten von der ägyptischen Sinai-Halbinsel in die Stadt Ismailia am Suezkanal geflohen
Mashambulizi dhidi ya wakristu wa madehebu ya Koptiki nchini Misri yamezidiPicha: Getty Imgaes/AFP/Stringer

Jumuiya za Kimataifa zalaani shambulizi hilo.

Shambulizi hili linakuja baada ya kundi la jihadi kutishia kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya Wakristu wa Koptik, ambao ni asilimia 10 tu ya idadi ya Wamisri Milioni 90. Washambuliaji wa kujitoa muhanga wakiwa na kundi la Jihadi walishambulia kanisa Disemba 11 mwaka jana, karibu na kiti cha papa wa madhehebu hayo ya Koptik na kuua watu 29.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake amesema, Israel inalaani vikali mashambulizi mabaya ya kigaidi nchini Misri, na kutuma salamu za pole kwa niaba ya wananchi wake kwa rais Fattah al-Sissi na watu wa Misri. Amesema, ugaidi utaangushwa haraka kama mataifa yataungana pamoja dhidi yake" 

Ujerumani imelaani vikali tukio hilo. Msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni Martin Schaefer amesema taarifa hiyo imepokelewa kwa simanzi kubwa kwa kubainisha kuwa Ujerumani kwa sasa inahifadhi idadi kubwa ya kusanyiko la waumini wa madhehebu ya Protestanti na Wakoptiki wakiwa miongoni mwao. Imeahidi kushirikiana na Misri katika kuhakikisha kwamba mashambulizi kama haya hayatokei tena katika siku za mbele. 

Aprili 11, washambuliaji waliokuwa na mabomu walishambulia makanisa mawili katika eneo la Kaskazini mwa Cairo katika Jumapili ya matawi na kusababisha vifo vya watu 45, katika shambulizi ambalo limesalia kwenye vichwa vya waumini wa dhehebu hili kama ni la kutisha zaidi.

Shambulizi la leo hii linafanywa baada ya ziara ya kihistoria ya kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis nchini Misri iliyolenga kuonyesha mshikamano na waumini wa Kikristu nchini humo.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/ape/afpe
Mhariri: Josephat Charo