1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Abbas analenga nini?

Maja Dreyer18 Desemba 2006

Mzozo kati ya makundi ya Fatah na Hamas kwenye ardhi ya Wapalestina ndiyo pia mada kuu katika magazeti ya Ujerumani ya hii leo.

https://p.dw.com/p/CHUB

Yale yanaowatia wasiwasi wahariri wa hapa nchini ni uamuzi wa Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kwamba uchaguzi ufanywe upya. Mfano ni maoni yaliyoandikwa katika gazeti la “Frankfurter Allgemeine Zeitung”:

“Kikatiba, Rais Abbas hana haki ya kulivunja bunge. Juu ya hayo, hakuna hakika nani atakayeweza kushinda uchaguzi huu mpya. Kwa nini basi, Abbas anakubali hatari hiyo? Sababu ni kwamba anataka kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe na anatumai kwamba watu wamechoka na makundi mawili yanayogombana tu.”

Na katika gazeti la “Westdeutsche Zeitung” la mjini Düsseldorf tunasoma yafuatayo:
“Kutangaza tu uchaguzi mpya hakutuliza hali kwenye ardhi ya Wapalestina, lakini kumezidisha ukali wa mzozo. Nini basi kutatokea ikiwa kweli Wapalestina watapiga kura upya? Kuna hatari kubwa kwamba kundi la msimamo mkali wa kiislamu la Hamas litakichukua pia kiti cha urais. Halafu Marekani na Umoja wa Ulaya ambazo kwa haraka ziliuunga mkono mpango wa uchaguzi mpya zitafanyaje? Je, zitaongeza vikwazo vya kifedha dhidi ya Wapalestina? Hadi hapa mkakati huu haujafanikiwa.” - ni gazeti la “Westdeutsche Zeitung”.

Gazeti la “General-Anzeiger” linachapishwa hapa mjini Bonn, na maoni yake ndiyo haya:

“Wapigaji kura wa Kipalestina wanajua kwamba msaada wa kifedha utapewa tu ikiwa fedha hizo hazitatumiwa vibaya na Hamas kwa kununua silaha na kulipa pensheni kwa familia za watu waliojitoa muhanga. Lakini huko Mashariki ya Kati watu wanaamua kutokana na hisia zao, hata katika hali duni na umaskini. Kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa chama cha Hamas kikashinda tena kwa sababu hakikubali kununuliwa na nchi za Magharibi.”

Na hatimaye tunaelekea kidogo kwenye michezo, baada ya duru ya kwanza ya ligi ya Ujerumani ikakamilika wikiendi hii iliyopita. Akiyakumbuka mashindano ya kombe la dunia la kandanda yalilofanyika nchini humu mapema mwaka huu, mhariri wa gazeti la “Berliner Morgenpost” anafikiria hali ya soka la Ujerumani. Ameandika:

“Wingi wa furaha ulipungua kabisa na ubora wa klabu hizi 18 zinazokamata nafasi ya juu ni wa wastani tu isipokuwa klabu ya Werder Bremen katika ligi ya Ujerumani na Bayer Munich katika ligi ya klabu bingwa za Ulaya, Champions League. Pia timu ya taifa, iliyoko sasa chini ya kocha Joachim Löw, iliwavunja moyo mashabiki wake katika mechi za kombe la Ulaya. Kusema ukweli, matarajio siyo makubwa. Hisia hizo za kombe la dunia zitarudi tu nyuma baada ya miaka kadhaa, na tena lazima wachezaji chipukizi wapewe nafasi kama Jürgen Klinsmann alivyofanya.”