1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABIDJAN : Uchaguzi ufanyike katika kipindi cha mwaka mmoja

15 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD2o

Ivory lazima ifanye uchaguzi wa rais ambao ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwezi wa Oktoba katika kipindi kisochozidi miezi 12 ili iweze kuondokana na mgogoro wake wa kisiasa.

Hayo yametamkwa hapo jana na Gerard Stoudmann Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Uchaguzi nchini Ivory Coast wakati akizungumza na radio ya Umoja wa Mataifa.

Koloni hilo la zamani la Ufaransa limegawika pande mbili tokea waasi walipoteka eneo la kaskazini nusu ya nchi hiyo kufuatia jaribio lililoshindwa la kumn’gowa madarakani Rais Laurent Gbagbo hapo mwezi wa Septemba mwaka 2002 na mpango wa amani uliokuwa ukijikokota tokea wakati huo umeshindwa kuleta utulivu wa kudumu.

Muda wa mpito uliokuwa ukiungwa mkono na Umoja wa Mataifa ulimpa Gbagbo miezi 12 zaidi madarakani wakati uchaguzi uliposhindwa kufanyika hapo mwezi wa Oktoba mwaka jana.

Viongozi wa Afrika wanatazamiwa kukutana katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa hapo Jumanne kujadili jinsi Ivory Coast inavyopaswa kuongozwa baada ya mamlaka ya Gbagbo kumalizika muda wake hapo tarehe 31 Oktoba.

Viongozi hao wanatarajiwa kupendekeza aendelee kubakia madarakani kwa mwaka mmoja zaidi.