1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABUJA:Asari Dokubo anyimwa dhamana

8 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBtc

Mahakama kuu nchini Nigeria inakataa kumuachia kwa dhamana kiongozi wa waasi wa Niger Delta Peoples Volunteer Force NDPVF,Mujahid Asari Dokubo.Dokubo anazuiliwa tangu mwezi Novemba mwaka 2005.Kulingana na mahakama hiyo hatua ya kumuachia kwa dhamana ni tisho la usalama wa taifa.

Kesi yake imeahirishwa mara kadhaa kila inapofikishwa mahakamani.Mahakama kuu inaunga mkono uamuzi wa awali uliotolewa mwezi Juni mwaka 2006 wa kubakia rumande kwasababu ya kesi inayomkabili ya uhaini.Kesi yake inasikizwa tena wiki ijayo tarehe 13 mjini Abuja.

Kwa mujibu wa wakili wake Festus Keyamo uamuzi huo wa kumkataza dhamana huenda ukachochea ghasia katika eneo la Niger Delta ambako waasi wengi wanatoa wito wa kuachiwa kwa Dokubo bila masharti.

Mwanasheria huyo analaumu uongozi wa Nigeria kwa kumzuia mteja wake kwenye jela ya chini kwa chini na kutoa wito kwa Rais Umaru Yar’Adua kumuachia huru.

Eneo la Niger Delta lililo na mafuta mengi ndio makao ya viwanda vingi vya mafuta na limezongwa na ghasia na visa vya utekaji katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.Takriban raia 190 wa kigeni wametekwa na kuachiwa baada ya muda wa majuma au siku kadhaa.

Serikali kwa upande wake inalitaja kundi la Dokubo kuwa la wahalifu na kulilaumu kwa kuiba mafuta kutoka mabomba na kuyauza kinyume na sheria.Hata hivyo kundi hilo limesambaratika baada ya Dokubo kukamatwa.