1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Sudan yakubali kikosi kwa Dafur

13 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBsG

Sudan hapo jana imekubali kikosi mchanganyiko cha wanajeshi wa kulinda amani na polisi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zaidi ya 20,000 kuwekwa katika jimbo lake la vurugu la Dafur baada ya miezi kadhaa ya juhudi nzito za kidiplomasia.

Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika Said Djinnit amesema serikali ya Sudan imekubali kikosi hicho mchanganyiko cha kati ya wanajeshi 17,000 hadi 19,000 pamoja polisi 3,700.Kufuatia mkutano wa siku mbili mjini Addis Ababa Ethiopia Sudan imekubali vikosi hivyo baada ya kupatiwa ufafanuzi na yakinisho kutoka vyombo viwili vya kimataifa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameikaribisha hatua hiyo ya Sudan na kusistiza haja ya kuwepo kwa usitihaji mapigano kabambe katika jimbo la magharibi mwa Sudan.

Ban amesema hatua hiyo inapaswa kuandamana na mchakato wa kisiasa kuekelea ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa Dafur.

Mgororo wa Dafur ulianza mwaka 2003 na umesababisha vifo vya watu 200,000 pamoja na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni mbili kupoteza makaazi yao.