1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA:Ban Ki-Moon kuzungumza na Rais al Bashir wa Sudan

29 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCWt

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliwasili mjini Addis Ababa nchini Ethiopia jana jioni ili kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika AU aidha kufanya mazungumzo na Rais wa Sudan Omar el Bashir.Mazungumzo hayo yanalenga kujadilia suala la kupeleka kikosi cha kulinda amani katika eneo la Darfur kitakachoshirikisha majeshi ya Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa.

Bwana Ki Moon alikuwa akitokea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo alikokutana na Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila baada ya mazungumzo mjini Kisangani katika makazi ya gavana. Kabla kuondoka mjini Kisangani kiongozi huyo aliwahutubia waandishi wa habari na kusisitiza kuwa atamueleza Bwana Bashir umuhimu wa kuanzisha utekelezaji wa makubaliano ya kupeleka kikosi cha kulinda amani katika eneo la Darfur.Bwana Bashir aliidhinisha pendekezo hilo baada ya muda wa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika,AU kumalizika. Majeshi hayo yanazongwa na matatizo ya uhaba wa vifaa.Bwana Ki Moon aidha alimhakikishia Rais Kabila kuwa hakuna mpango wa kuondo au kupunga kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo MONUC kilicho na majeshi alfu 20.Kikosi cha MONUC ndicho kikubwa zaidi cha kulinda amani ulimwenguni.Nchi ya Kongo ilifanya uchaguzi wa kihistoria mwaka jana baada ya kipindi cha miaka 40.

Ban Ki-Moon alifanya mazungumzo na Kamishna wa Umoja wa Afrika AU Alpha Oumar Konare katika mkesha wa kikao cha Umoja huo.Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kuhutubia kikao hicho hii leo baada ya kufanya mazungumzo na naibu Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika Jendayi Fraser .Aidha Bwana Ban Ki-Moon anapanga kufanya majadiliano na baadhi ya viongozi wa bara la Afrika kandoni mwa mkutano huo.Ziara ya siku mbili ya kiongozi huyo ni sehemu ya nne ya ziara yake ya mataifa saba.Hii ni ziara yake ya kwanza katika mataifa ya kigeni tangu kuchukua wadhifa huo kama Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa.