1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA:Ziara ya Kansela Merkel kukita katika maendeleo,haki za binadamu na uchumi

4 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Ic

Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel yuko nchini Ethiopia ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya bara la Afrika.Kiongozi huyo anatarajiwa kuzuru mataifa ya Liberia na Afrika Kusini.Bi Merkel anaandamana na Waziri wa Ushirikiano na Maendeleo Bi Heidemarie-Wieczorek-Zeul,wabunge na viongozi wa kibishara na anatarajiwa kukutana na viongozi wa kisiasa nchini Ethiopia.

Ziara yake ya kwanza ya Bara la Afrika inatazamiwa kukita katika masuala ya haki za binadamu,ugonjwa wa Ukimwi,ushirikiano wa kiuchumi aidha tatizo la kisiasa nchini Zimbabwe.

Bi Merkel anapanga kufanya mazungumzo na Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini hapo kesho na kuelekea Liberia siku ya jumapili.

Kansela wa Ujerumani anatarajiwa kuhutubia Umoja wa Afrika na kufanya mazungumzo na kiongozi wake Alpha Oumar Konare kuhusu hali ya Sudan na jukumu la Afrika katika kikosi kilichoimarishwa cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kinachopangwa kupelekwa Darfur.

Kwa upande mwengine mkutano huo unalenga kufanya maandalizi ya mkutano wa Umoja wa Ulaya na Afrika unaopangwa kufanyika mjini Lisbon nchini Ureno mwishoni mwa mwaka hu.Huu ni mkutano wa kwanza kati ya mabara hayo mawili katika kipindi cha miaka 5.Bi Merkel anatarjiwa aidha kukutana na rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela siku ya jumamosi na kuzuru mji wa Soka kunakojengwa uwanja wa michezo katika matayarisho ya kuandaa kombe la dunia mwaka 2010.