1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali mwandamizi auwawa Burundi

2 Agosti 2015

Jenerali wa ngazi ya juu nchini Burundi na mshirika wa karibu wa masuala ya usalama wa Rais Piere Nkurunziza ameuwawa baada ya gari lake kushambuliwa mjini Bujumbura Jumapili (02.08.2015).

https://p.dw.com/p/1G8hL
Wanajeshi wa Burundi.
Wanajeshi wa Burundi.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Jenerali wa ngazi ya juu nchini Burundi na mshirika wa karibu wa masuala ya usalama wa Rais Piere Nkurunziza ameuwawa baada ya gari lake kushambuliwa mjini Bujumbura Jumapili (02.08.2015).

Jenerali Adolph Nshimirimana aliuwawa wakati gari lake liliposhambuliwa kwa risasi na watu waliokuwemo kwenye gari jengine katika kitongoji cha Kamenge mjini Bujumbura Jumapili asubuhi.

Akithibitisha kuuwawa kwa generali huyo ambaye ndie aliekuwa akishughulikia usalama wa taifa hilo la Afrika ya kati lililokumbwa na mzozo na hata kuhesabiwa kama ni kiongozi anayeshika nafasi ya pili katika uongozi wa nchi, Wily Naymwite msemaji wa rais ameandika katika mtandao wake wa twitter kwamba amempoteza kaka na mshirika katika mapambano.

Kwa mujibu wa Nyamitwe walimfyetulia risasi Generali Nshimirama na walinzi wake pamoja na kulirushia guruneti gari lake ambapo baadae alikufa kutokana na majeraha.

Uchaguzi tata

Kuuwawa kwa generali huyo kumekuja wiki moja na kitu hivi baada ya Rais Nkurunziza kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi uliozusha utata na kupatiwa mamlaka ya muhula wa tatu kuongoza nchi mfululizo licha ya maandamano ya upinzani kupinga uchaguzi huo ambao pia umeshutumiwa na jumuiya ya kimataifa.

Burundi wakati wa uchaguzi.
Burundi wakati wa uchaguzi.Picha: DW/S. Schlindwein

Ugombea wa Nkurunziza umelaaniwa kuwa unakiuka katiba na umechochea machafuko yaliyodumu kwa miezi kadhaa na kusababisha takriban watu 100 kupoteza maisha yao kutokana na hatua kali zilizochukuliwa na serikali kuvunja maandamano hayo na jaribio la mapinduzi lililoshindwa kati kati ya mwezi wa Mei.

Duru kutoka ofisi ya rais imesema hali nchini Burundi ni mbaya sana na kuonya juu ya uwezekano wa kuzuka kwa wimbi la mashambulizi ya visasi.Duru hiyo ambayo imekataa kutajwa jina imekaririwa ikisema "tunajaribu kudhibiti hali hiyo lakini sio rahisi na kwamba vijana wao wanataka kulipiza kisasi."

Wasi wasi watanda

Duru za polisi zinasema watu saba wamekamatwa na duru kuroka shirika la ujasusi la taifa nchini Burundi SNR imesema vikosi vya usalama vina wasi wasi.Duru hizo zimesema mtu hawezi kujuwa Generali Adolphe alikuwa ana maana gani kwao.

Mwanajeshi wa serikali nchini Burundi.
Mwanajeshi wa serikali nchini Burundi.Picha: S. Kambou/AFP/Getty Images

Jenerali mwengine mwandamizi anayemuunga mkono Kurunziza ambaye ameomba kutotajwa jina amesema wametangaza vita na watakiona watakachokipata.

Hakuna mtu aliyedai kuhusika na mauaji hayo juu ya kwamba wale waliokula njama za kufanya mapinduzi wamekuwa wakijikusanya kuungana kaskazini mwa nchi hiyo na pia wamekuwa wakihusishwa na mfululizo wa mashambulizi ya maguruneti mjini Bujumbura.

Mwezi uliopita serikali ya Burundi imesema jeshi lake limezima uasi kaskazini mwa nchi hiyo na kuuwa waasi 31 na kuwatia mbaroni wengine 171.Kuna hofu kwamba kuzuka upya kwa mzozo nchini Burundi kunaweza kufufuwa umwaji damu chini ya misingi ya kikabila kati ya Watutsi na Wahutu na kusababisha janga jengine la kibinaadamu katika eneo la maziwa makuu barani Afrika lenye vurugu.

Vita vya mwisho vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi viliomalizika mwaka 2006 vimepelekea kuuwawa kwa takriban watu 300,000.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/AP

Mhariri : Isaac Gamba