1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan-Isaf

Hamidou, Oumilkher23 Septemba 2008

Baraza la usalama la umoja wa mataifa larefusha kwa mwaka mmoja shughuli za vikosi vya kimataifa vya Isaf nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/FNLv
Mwanajeshi wa Ujerumani akisaidiana na wanajeshi wa Afghanistan huko Taloqan,karibu na KunduzPicha: AP


Baraza la usalama la umoja wa mataifa limerefusha muda wa shughuli za vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya magharibi NATO nchini Afghanistan.Hata hivyo taasisi hiyo muhimu ya kimataifa imeelezea wasi wasi wake kutokana na kuzidi makali matumizi ya nguvu ya wataliban yanayogharimu maisha ya raia wa kawaida.



Baraza la usalama la umoja wa mataifa limepitisha kwa sauti moja azimio nambari 1833 kuhusu kurefushwa hadi October 12 mwaka 2009 shughuli za vikosi vya kimataifa vionavyoongozwa na jumuia ya NATO -ISAF nchini Afghanistan.


Katika azimio hilo, baraza la usalama la Umoja wa mataifa linasema tunanukuu; "japo kama yanaeleweka matatizo makubwa yanayotokana na opereshini za kujibu vitisho vya "wataliban,Al Qaida na makundi mengine ya wafuasi wa itikadi kali" hata hivyo baraza la Usalama limeingiwa na wasi wasi mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wahanga miongoni mwa raia."


Libya imeunga mkono pia azimio hilo,hata hivyo balozi wake,Ibrahim Dabbashi ameelezea wasi wasi wa nchi yake kuelekea janga hilo.


""Mapambano dhidi ya ugaidi hayahalalishi hata kidogo vifo vya raia wengi kama hao."Amesema balozi huyo wa Libya katika Umoja wa mataifa na kuongeza tunanukuu:

"Matumizi ya nguvu pekee hayatasaidia kuleta amani na usalama nchini Afghanistan,kama mdahalo hautaendelezwa kusaka suluhu ya taifa" mwisho wa kumnukuu balozi wa Libya katika umoja wa mataifa.



Jumla ya raia 1445 wameuwawa kufuatia matumizi ya nguvu nchini Afghanistan tangu mapema mwaka huu-.Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa hilo ni ongezeko la asili mia 39,ikilinganishwa na idadi ya wahanga katika kipindi cha miezi minane ya mwanzo ya mwaka jana.Wengi wao wanauwawa kufuatia mashambulio ya wataliban,lakini pia makosa yanatokea katika opereshini za vikosi vya kimataifa na kuzusha ghadhabu miongoni mwa jamii na malalamiko ya viongozi wa serikali ya mjini Kaboul.


Wanajeshi 70 elfu wa kigeni,33 elfu kati yao ni wa kimarekani wanatumikia vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na NATO- Isaf nchini Afghanistan na vile vinavyoongozwa na Marekani kwa jina "opereshini ya uhuru usiobadilika."


Baraza la usalama la umoja wa mataifa limezitolea mwito nchi zinazochangia wanajeshi nchini Afghanistan zizidishe idadi ya wananchi wao na vifaa vyao ili kufanikisha shughuli zao.


Nchini Afghanistan kwenyewe gavana wa mkoa wa kusini wa Registan pamoja pia na mkuu wa polisi wa eneo hilo wameuwawa bomu liliporipuliwa karibu na gari yao huko Kandahar.Wataliban wamedai kuhusika na shambulio hilo.


Wataliban wamedai pia dhamana ya shambulio la leo asubuhi dhidi ya vikosi vya Ujerumani katika mji wa Kunduz,kaskazini magharibi ya nchi hiyo.Mbali na gaidi aliyejiripua pamoja na gari yake,hakuna hasara ya maisha wala ya mali iliyoripotiwa.


Kanali Roner Boska wa kituo cha kijeshi cha Ujerumani huko Kunduz amesema magari mawili ya NATO yameharibika kidogo tuu.


Ujerumani imetuma wanajeshi 3220 kutumikia vikosi vya Isaf,na wote wanakutikana katika sehemu ya kaskazini ya Afghanistan.