1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan: Shambulizi Kabul limewaua watu 40

John Juma
28 Desemba 2017

Watu 40 wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea katika kituo cha kitamaduni cha Kishia mjini Kabul. Kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS limedai kulifanya shambilizi hilo

https://p.dw.com/p/2q2EE
Afghanistan Anschlag in Kabul auf Afghan Voice
Picha: Getty Images/AFP/S. Marai

Watu 40 wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea katika kituo cha kitamaduni cha Kishia mjini Kabul. Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amelitaja shambulizi hilo kuwa shambulizi dhidi ya ubinadamu.

Naibu msemaji wa wizara ya ndani Nasrat Rahimi amesema shambulio hilo lililenga kituo cha kitamaduni cha Tabayan ambacho ni cha Washia, huku akiongeza kuwa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 38 tangu uvamizi wa Kisoviet nchini Afghanistan yalikuwa yakiendelea katika kituo hicho wakati mlipuko ulipotokea.

Rahimi amesema watu 40 wameuawa, 30 wamejeruhiwa lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka. Kulingana na Rahimi, mlipuko mkubwa ulifuatwa na milipuko mingine miwili ya mabomu lakini haikusababisha vifo. Ali Reza ni miongoni mwa walioshuhudia shambulizi hilo:

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan amelilaani shambulizi hilo
Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan amelilaani shambulizi hiloPicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

"Niliona watu wengi waliokufa. Nilikuwa nikimtafuta binamu yangu lakini sikuweza kuupata mwili wake. Sina uhakika amefikwa na masaibu gani. Idadi ya waliofariki imeongezeka"

Rais Ashraf Ghani alilaani shambulizi hilo

Katika taarifa kutoka ikulu, rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amelitaja shambulizi hilo na mengine ambayo yamewahi kutokea siku za nyuma kuwa mashambulizi dhidi ya Uislamu na dhidi ya maadili yote ya kibinadamu.

Kundi linalojiita Dola la Kislamu IS limedai kulifanya shambulizi hilo ambalo limetokea karibu na shirika la habari la Afghan Voice. Ripoti za awali zilidokeza huenda shirika hilo la habari ndilo lililengwa.

Shambulizi la leo limejiri siku chache baada ya mlipuaji wa kujitoa muhanga kuwaua raia sita katika shambulizi lililofanywa karibu na makao ya shirika la ujasusi mjini Kabul. Kundi la IS lilidai kuhusika.

Kabul miongoni mwa maeneo hatari Afghanistan

Kabul imekuwa mojawapo ya maeneo hatari sana katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na machafuko ya kiraia katika miezi ya hivi karibuni, huku kundi la Taliban likiimarisha mashambulizi yao na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS likijaribu kuupanua uwepo wao katika nchi hiyo.

Maafisa wa usalama wakishika doria katika eneo la shambulizi
Maafisa wa usalama wakishika doria katika eneo la shambuliziPicha: picture-alliance/Zuma Press/Xinhua/R. Alizadah

Kundi hilo la Kijihadi, la Mashariki ya Kati limejiimarisha Afghanistan tangu lilipojitokeza katika eneo hilo kwa mara ya kwanza mnamo 2015. Limeendelea kuzidisha mashambulizi mjini Kabul, ikiwemo dhidi ya vituo vya kiusalama na dhidi ya Washia walio wachache nchini humo.

Usalama wa Kabul uliimarishwa tangu Mei 31, wakati mlipuko mkubwa uliofanywa kwa bomu la kutegwa lorini ulitokea katika eneo la kidiplomasia lenye afisi za ubalozi wa nchi mbalimbali. Shambulizi hilo liliwaua watu 150 na takriban watu 400 wengi wakiwa raia, walijeruhiwa.

Vyombo vya habari vyalengwa?

Katika siku za nyuma, vyombo vya habari vya Afghanistan vimewahi kulengwa na wanamgambo, hali inayoashiria hatari inayowakumba waandishi wa habari katika taifa hilo linalozongwa na vita.

Mwezi Novemba, shambulizi katika kituo cha televisheni cha Shamshad mjini Kabul lilisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa. Kundi la IS lilidai kuhusika na shambulizi hilo.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE

Mhariri:Gakuba, Daniel