1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watumishi wa Umoja wa Mataifa kuhamishwa.

Abdu Said Mtullya5 Novemba 2009

Umoja wa Mataifa unawaondoa baadhi ya watumishi wake nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/KOzX
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wakati wa ziara yake nchini Afghanistan.Picha: AP

Umoja wa Mataifa umeamua kuwaondoa watumishi wake kutoka Afghanistan kufuatia mashambulio ya hivi karibuni katika mji wa Kabul.

Msemaji wa Umoja huo ameeleza leo kuwa watumishi wapatao 600 ambao siyo muhimu watahusika na zoezi hilo.

Hatua hiyo inafuatia shambulio lililofanywa na taliban wiki jana ambapo watumishi watano wa Umoja wa Mataifa pamoja na raia watatu wa Afghanistan waliuawa katika makao ya Umoja Mataifa mjini Kabul.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Dan McNorton ameeleza leo kwamba watumishi watakaobakia ni wale tu wenye majukumu muhimu.

Karibu watumishi 600 wataondolewa nchini Afghanistan na idadi ndogo watahamishiwa katika sehemu zingine za nchi.

Zoezi la kuwahamisha watu hao litaanza kutekelezwa mara moja.

Hatahivyo msemaji wa Umoja wa Mataifa amefafanua kwamba uamuzi huo utakuwa unarelejewa mara kwa mara wakati hatua za usalama zikiimarishwa.

Katika tamko lake, Umoja wa Mataifa umesema, shirika hilo litaendelea kujizatiti katika kuwasaidia watu wa Afghanistan kama ambavyo limekuwa linafanya kwa muda wa zaidi ya nusu karne.

Umoja wa Mataifa ulitoa mchango mkubwa katika kuandaa uchaguzi mkuu nchini Afghanistan. Aidha mashirika yake kama UNICEF yanatekeleza miradi ya afya,elimu na mingine ya maendeleo nchini. Umoja huo umesema huduma hizo zitaendelea kutolewa.

Umoja wa Mataifa una watumishi wapatao 5600, nchini Afghanistan- idadi kubwa wakiwa raia wa nchi hiyo. Ni asilimia 12 tu watakaohusika na zeozi la kuhamishwa au kuondolewa.

Mwakilishimkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Kai Eide anatarajiwa baadae leo kuzungumza na waandishi habari ili kufafanua utekelezaji wa uamuzi wa kuwahamisha watumishi Umoja huo.

Uamuzi wa Umoja wa Mataifa ni pigo kwa mkakati wa rais Barack Obama wa kupambana na taliban wakati ambapo rais huyo wa Marekani bado anatafakari pendekezo la jenerali wake mkuu nchini Afghanistan juu ya kuwapeleka wanajeshi 40,000 zaidi nchini humo.

Katika tukio jingine nchini Afghanistan, Australia imemwambia mshirika wake Marekani, kwamba haitaongeza majeshi nchini humo.Waziri wa ulinzi wa nchi hiyo John Faulkner amewaambia maafisa waandamizi wa Marekani kwamba Australia haitaongeza askari zaidi ya 1550 waliokuwapo nchini Afghanistan kwa sasa.

Mwandishi Mtullya Abdu/ RTRE/AFP/ZA

Mhariri/Abdul-Rahman