1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa magereza ataka Pistorius apewe kifungo cha nyumbani

13 Oktoba 2014

Mawakili wa Oscar Pistorius wanataka mwanariadha huyo wa Afrika Kusini asipewe adhabu ya kifungo Jela, wakisisitiza kuwa anajutia kitendo chake na kuwa ni mtu wa tabia nzuri

https://p.dw.com/p/1DV1M
Oscar Pistorius Ankunft Pretoria Gericht 13.10.
Picha: Reuters/Siphiwe Sibeko

Mwakilishi wa Idara ya Magereza ya Afrika Kusini Joel Maringa amependekeza kuwa Oscar Pistorius aadhibiwe kwa kupewa kifungo cha nyumbani kwa kipindi cha miaka mitatu pamoja na huduma za jamii kwa kupatikana na hatia ya kumuua mchumbake Reeva Steenkamp. Pistorius alipatikana na hatia mwezi uliopita kwa kumpiga risasi na kumuua mchumba wake bila kukusudia mnamo mwaka wa 2013.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 27 mwenye miguu ya bandia, aliondolewa baadhi ya mashtaka makubwa ya mauaji, hukumu ambayo iliishangaza nchi hiyo na kuzusha shutuma dhidi ya mfumo wa sheria nchini Afrika Kusini. Anaweza kupewa adhabu ya hadi miaka 15 jela au hata aepuke kifungo cha jela. Akizungumza katika kikao cha leo, mwakilishi wa magereza Maringa amesema kifungo cha nyumbani kitamwezesha Pistorius kujitathmini na kuirekebisha tabia yake.

Mwendesha mashtaka wa serikali Gerrie Nel alilitaja pendekezo la Maringa kuwa “lisilofaa”. Wakati akimhoji shahidi huyo, Nel alimuuliza Maringa kama alifahamu uzito wa uhalifu ambao Pistorius aliufanya, baada ya kukiri kuwa hakuwa na ufahamu wa kina kuhusu kesi hiyo.

Oscar Pistorius Ankläger Gerrie Nel 7. August
Mwendesha mashtaka wa serikali Gerrie NelPicha: MUJAHID SAFODIEN/AFP/Getty Images

Maringa alikuwa mmoja wa mashahidi watatu walioitwa na mawakili wa Pistorius ambao wanataka mshtakiwa apewe kifungo cha nyumbani. Wakala wake alitoa ushahidi kuhusu kazi yake ya hisani na awali, mtalaamu wake wa ushauri Lore Hartzenberg aliiambia mahakama kuwa Pistorius anajutia kisa hicho cha kumpiga risasi na kumuua Steenkamp.

Upande wa serikali kisha utawaita mashahidi wake kutoa ushahidi wa ni kwa nini mshtakiwa anastahili kupewa adhabu kali, na kuzusha suala la historia ya uzembe katika umiliki wa silaha. Baada ya hukumu kutolewa, pande zote mbili za mashtaka na utetezi zitaweza kukata rufaa, mchakato wa kisheria ambao huenda ukachukua miaka kadhaa.

Uamuzi aliofanya jaji Thokozile Masipa uliwashangaza na kuwakasirisha Waafrika Kusini wengi wakiwemo mawakili ambao waliamini kuwa alitumia vibaya tafsiri ya mauaji, na wakahoji kama mfumo wa mahakama unashindwa kufanya kazi vyema katika nchi hiyo yenye kiwango kikubwa cha uhalifu.

Pistorius kwa sasa yuko nje kwa dhamana ya dola milioni 90,000. Alilazimika kuuza nyumba yake ya kifahari mjini Pretoria ili kufadhili gharama ya kesi hiyo na pia amejiondoa kutoka mashindano ya riadha tangu alipokamatwa. Kikao cha kutoa hukumu kitaendelea hapo kesho.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu