1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa zamani wa Netanyahu kutoa ushahidi dhidi yake

John Juma
4 Agosti 2017

Kiongozi wa zamani wa ofisi ya waziri mkuu Ari Harrow amekubaliana na waendesha mashtaka kutoa ushahidi huo kwa niaba ya serikali dhidi ya Netanyahu. Netanyahu anakabiliwa na tuhuma za rushwa.

https://p.dw.com/p/2hia4
Ungarn Budapest -  Benjamin Netanyahu und Viktor Orban bei Pressekonferenz
Picha: Getty Images/AFP/P. Kohalmi

Aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekubali kutoa ushahidi dhidi ya Netanyahu kuhusu madai mawili ya ufisadi yanayomkabili mwanasiasa huyo mwenye misimamo mikali, ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu. Hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Israel.

Ripoti hiyo ambayo imechapishwa kwenye gazeti la kila siku la Haaretz na vyombo vingine vya habari, inasema kuwa Ari Harrow amekubaliana na waendesha mashtaka leo kutoa ushahidi huo kwa niaba ya serikali dhidi ya Netanyahu aliyekuwa mwajiri wake.

Tuhuma za rushwa

Mnamo Alhamisi wiki hii, polisi ya Israel ilifichua kuwa Netanyahu anakabiliwa na tuhuma zinazohusu ufisadi, uvunjifu wa imani na hongo.

Maafisa wa polisi wamekuwa wakimhoji Netanyahu kuhusu madai kuwa alipokea zawadi kutoka kwa wafuasi wake ambao ni matajiri kwa njia isiyofaa ikiwemo kutoka kwa bilionea kutoka Australia, James Packer, na mtengeneza filamu wa Hollywood, Arnon Milchan. Na kwamba alifanya mazungumzo ya kipekee na mchapishaji wa gazeti moja kuu nchini Israel ili kuchapisha taarifa nzuri kumhusu.

Mtengeneza filamu Arnon Milchan
Mtengeneza filamu Arnon MilchanPicha: Getty Images

Netanyahu ameyapuuzilia mbali madai hayo na kukana kufanya makosa yoyote, huku akisema ni njama dhidi yake.

Mjadala ukiwa Netanyahu atajiuzulu

Uchunguzi huo umeibua mjadala wa kisiasa nchini Israel kati ya wanaomuunga mkono Netanyahu na wanaompinga, huku swali likiibuka ikiwa Netanyahu atalazimika kujiuzulu. Daniel Silver ni mkazi wa Jerusalem anayemtetea Netanyahu kwa msingi wa utendakazi wake na kuwa ana imani naye kuhusu usalama wa nchi: "Ninafikiri Netanyahu ni kiongozi bora kwa Israel. Ninafikiri anatuwakilisha vyema nje, ninafikiri haya yote ambayo munayoyasikia kumhusu yeye sivyo alivyo. Hana hatia, hivyo ninamwamini."

Lakini miongoni mwa wakosoaji wa Netanyahu ni mkaazi mmoja wa Jerusalem ambaye hakutaka kujitambulisha jina, akisema anatumai mwanasiasa huyo atapatikana na hatia ili kuwe na mabadiliko katika uongozi: "Tunatumai kuwa watampata na hatia kuhusu kitu kama ufisadi.. ili serikali ya Israel hatimaye ibadilike kwa sababu ni muda mrefu Bibi amekuwa waziri mkuu na ni wakati wa mtu mpya. Tunahitaji amani."

Inaripotiwa kuwa maafisa wa polisi wanayo kanda iliyorikodiwa na Harrow kuhusu mazungumzo kati ya Netanyahu na mchapishaji huyo. Hata hivyo hakuna taarifa rasmi kuhusu ripoti hizo na mahakama imepiga marufuku uchapishaji wa taarifa hiyo ambayo imevujishwa.

Harrow alimfanyia kazi Netanyahu kati ya mwaka 2009 hadi 2010, na pia kati ya mwaka 2014-2015 ambapo alijiuzulu kufuatia madai ya ufisadi.

Mwandishi: John Juma/AP/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef