1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Africa itatue matatizo yake yenyewe

6 Desemba 2015

Mataifa 50 ya Afrika pamoja na China yamekamilisha mkutano wake muhimu wa kilele jana Jumamosi(05.12.2015)yakiahidi kuweka msukumo wa suluhisho la matatizo ya ndani la amani na usalama katika bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/1HI5u
Südafrika China Präsident Xi Jinping in Johannesburg
Rais wa China Xi Jinping na mkewe wakihudhuria chakula katika mkutano mjini JohannesburgPicha: picture-alliance/Zumapress/Huang Jingwen

Viongozi hao walikutana kwa kile rais wa Afrika kusini Jacob Zuma alichosema kuwa ni mazungumzo ya "kihistoria", yenye lengo la kuimarisha mahusiano baina ya bara hilo na mshirika wake mkubwa wa kibiashara China.

"Tunabaki kuwa na nia ya kutafuta kutatua mizozo kupitia mazungumzo na mashauriano, na China inaiunga mkono Afrika katika juhudi zake za kutatua matatizo kupitia suluhisho la Waafrika," wamesema viongozi hao katika azimio.

Südafrika China Präsident Xi Jinping in Johannesburg
Rais wa China Xi Jinpingakihutubia mkutano kati ya China na AfrikaPicha: picture-alliance/dpa/E. Jiyane

Wamekubaliana kutekeleza mpango wa China wa amani na usalama kwa bara la Afrika na "wauanga mkono ujenzi wa mfumo wa pamoja wa usalama katika bara la Afrika."

Viongozi 48 waliohudhuria mkutano huo wa pili wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)ambao umefanyika kwa mara ya kwanza katika bara la Afrika.

China kusaidia ujenzi wa miundo mbinu

China imetoa fungu la dola bilioni 60 litakalolenga maeneo 10, ikiwa ni pamoja na viwanda, miundo mbinu, huduma za fedha , kupunguza umasikini na amani na usalama.

Südafrika Jacob Zuma Flugzeug
Rais Jacob Zuma na mkewePicha: picture-alliance/dpa/R. Sitdikov

Sehemu ya mpango huo , dola milioni 60 itakwenda katika kusaidia ujenzi wa jeshi jipya la Umoja wa Afrika lenye wanajeshi 25,000 litakalokuwa tayari kuingia katika maeneo ya mizozo katika bara la Afrika.

Mwezi Januari China iliweka kikosi cha kulinda amani nchini Sudan kusini.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan kusini Barnaba Benjamin ameueleza ujumbe wa China wa kulinda amani nchini mwake chini ya mwanvuli wa Umoja wa Mataifa kuwa ni "mabadiliko ya msingi katika sera za mambo ya kigeni za China".

Addis Abeba Äthiopien Bahn Straßenbahn Haltestelle
Moja ya miradi iliyojengwa na China nchini Ethiopia ya usafiri wa mjiniPicha: picture-alliance/dpaMarthe van der Wolf

Rais wa China Xi Jinping amekiambia kikao cha mwisho cha mkutano huo kwamba "china na Afrika ni nguvu muhimu katika kuimarisha amani na utulivu duniani na kuhimiza maendeleo ya dunia na ufanisi."

Jukumu la China lapanuka

"Tuna jukumu na uwezo wa kuchukua hatua kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa."

African Union Hauptquartier in Addis Abeba
Jengo la makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa lililojengwa na ChinaPicha: AFP/Getty Images/J. Vaughan

Mohammed al-Bairi , waziri wa mambo ya kigeni wa Libya nchi inayokumbwa na machafuko ameikaribisha nafasi inayopanuka ya China barani Afrika kutoka kuwa tu ya kiuchumi na miundo mbinu na kufikia masuala ya amani na usalama.

"Ni hatua ya kusonga mbele kwetu katika bara la Afrika," amesema.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika kusini Maite Nkoana-Mashabane amesema uamuzi wa mkutano huo "umeinua ushirika huo katika kiwango cha juu cha mkakati" na "utabadili mtazamo wa bara letu kwa kiasi kikubwa."

China Afrika Engagement
Mfanyakazi kutoka China akisimamia ujenzi wa barabaraPicha: AP

Viongozi katika mkutano huo wamepuuzia maelezo kwamba China inapora mali asili za Afrika na inakuwa mkoloni mamboleo katika bara hilo.

"Ni upuuzi," kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe amekiambia kituo cha televisheni cha China CCTV. "China haijawahi kuwa mkoloni katika bara la Afrika ama nchi yoyote. Ni wao, (mataifa ya magharibi) ambayo yamelipora bara la Afrika na bado wanafanya hivyo hadi sasa."

"China inatoa ushirika wa nipe nikupe katika bara la Afrika, na tutafaidika na hilo."

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Isaac Gamba