1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katíka magazeti ya Ujerumani

Miraji Othman13 Novemba 2009

Nini yanasema magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika?

https://p.dw.com/p/KWaD
Boti yay ulinzi wa baharini huko Italy ikiwa imebeba wakimbizi kutokea Libya ambao wanataka kuingia UlayaPicha: AP

Wakati ule ule ambapo wiki hii kulifanyika sherehe katika mji mkuu wa Ujerumani kuadhimisha miaka 20 tangu kuporomoka Ukuta wa Berlin, serekali ya Libya ilielezea mafanikio ilioyapata katika kuweka vizuzi vya uhuru wa kusafiri wa Waafrika kuelekea bara la Ulaya. Ilitajwa kwamba idadi ya wahamiaji wa Kiafrika ambao walijaribu kuelekea Ulaya kwa kuivuka Bahari ya Mediterrenean kutokea Libya kwa njia ya maboti imepungua kwa asilimia 90 tangu mwezi Februari. Gazeti linalochapishwa kila siku mjini Berlin, TAGESZEITUNG, lilimnukulu waziri wa mambo ya ndani wa Libya, Salah Rajab al-Masmari, akiliambia shirika la habari rasmi la Libya kama hivi:

"Tumeweza kutekeleza majukumu yetu kuelekea upande wa Italy, kwa vile uhamiaji haramu umepungua kwa asilimia 90, na tumeyavunja magengi ya watu wanaosafirisha binadamu kwa njia zisizokuwa za kisheria pamoja na kuwakamata watu hao."

Waziri huyo aliyaelezea hayo alipokutana mjini Tripoli na waziri mwenzake wa kutokea Italy, Robrto Maroni. Mwaka 2008 Italy iliwafikiana na Libya kuendesha doria za pamoja katika Bahari ya Mediterrenean kupambana na watu wanaosafirishwa kwa boti kwa njia haramu. Kutokana na habari za kutoka IItaly ni kwamba kufuatana gazeti hilo la TAGESZEITUNG, kati ya miezi ya Mei na Agosti mwaka huu, karibu wakimbizi 750 wamerejeshwa Libya kabla ya hata kukanyaga ardhi ya Ulaya.

Kujisifu huku kwa Libya kunakuja katika wakati yanafanyika mashauriano ya kuweko mkataba wa ushirikiano baina ya Libya na Umoja wa Ulaya, mashauriano ambayo yataendelezwa mwezi huu.

Kwa upande mwengine, gazeti hilo la TAGESZEITUNG limesema idadi ya Waafrika wanaofukzwa Libya kurejeshwa katika nchi zao, chini ya Jangwa la Sahara, imeongezeka. Tarehe 30 Septemba Wamali 153 walirejea nyumbani baada ya kuwekwa kizuizini Libya wa miezi miwili, na wakaripoti juu ya hali isiokuwa ya kiutu waliokabiliana nayo walipokuwa vizuizini. Pia karibu Wa-Nigeria 1,000 waliofukuzwa kutoka Libya mwezi Oktoba, na wiki iliopita waliiomba serekali yao iwapatie msaada wa kuanza maisha mepya. Pia Wa-Nigeria wengine 700 bado wako katika magereza ya Libya.

Gazeti la kila siku la SUDDEUTSCHE ZEITUNG liliripoti juu ya hali ilivyo huko Zimbabwe likianzia na ule mkasa wa Roy Bennett ambaye tangu mwezi Februari mwaka huu alitarajiwa kuwa makamo wa waziri wa kilimo wa nchi hiyo. Lakini hapo jumatatu alifikishwa tena mahakamani mjini Harare. Kambi ya Rais Robert Mugabe inamtuhumu Bennett, mkulima wa kizungu, mwenye umri wa miaka 52, kwa kuwa na silaha kinyume na sheria na kupanga kutaka kufanya mapinduzi. Yeye anakanusha tuhuma hiyo, lakini pindi atapatikana na hatia, basi huenda akakabiliwa na hukumu ya kifo. Kama ushahidi kulionyeshwa bunduki na risasi. Mkuu wa mashtaka, Johannes Tomana, kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, alisema mashtaka hayo ni ya hatari na alitaka Bennett akatazwe kusema kwamba ushahidi unaombana ulitolewa kutokana na mbinyo. Chama cha Bwana Bennett cha MDC kinaiona kesi hiyo kuwa ni ujanja wa Rais Mugabe. Kutokana na hali hiyo, chama hicho cha waziri mkuu Morgan Tsvangirai kilijitoa kutoka serekali ya umoja wa taifa, ambayo ilitakiwa ijaribu kuzuwia Zimbabwe isizidi kuporomoka, kiuchumi, na pia itayarishe uchaguzi wa haki. Katika uchaguzi wa hapo kabla, Robert Mugabe alipata ushindi dhidi ya mpinzani wake, Tsvangirai, kwa njia ya mizengwe.

Lakini, mwishoni mwa wiki, Morgan Tsvangirai alisema hatasusia tena kushiriki katika serekali, lakini alitaka tafauti baina ya chama chake cha MDC na chama cha Mugabe cha ZANU-PF zitanzuliwe mnamo mwezi mmoja. Hajasema, lakini, vipi mambo yatakavoendelea pindi hakutakuweko na muwafaka. Chama cha MDC kilitaka aachishwe kazi mkuu wa benki kuu ya Zimbabwe na pia mkuu wa kuendesha mashtaka. Wao wanasemakana kwamba ni watu walio watiifu kwa Mugabe na, kwa sehemu, wanahusika katika hali ngumu ilioko katika nchi hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, mashirika ya kupigania haki za binadamu duniani, Amnesty International na Human Rights Watch, yameonya kwamba Zimbabwe itakumbwa na mawimbi ya ghasia. Licha ya mazungumzo baina ya Tsvangirai na Mugabe, wapinzani wa serekali, maafisa wa jumuiya za kupigania haki za binadamu na waandishi wa habari wenye kuhakiki mambo wanakamatwa ovyo.

Bila ya kuweko Rais Omar al-Bashir wa Sudan, ulifunguliwa jumatatu hii mjini Istabul, Uturuki, mkutano wa kilele wa Umoja wa Nchi za Kiislamu, OIC. Rais wa Uturuki, Abdullah Gül, alitangaza kwamba nchi yake inataka kuimarisha na kupanua uhusiano wake na nchi za jumuiya hiyo ya OIC, na jambo hilo halipingani na juhudi za Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hadi jumapili iliopita, ilitangazwa huko Ankara kwamba Rais Hassan al-Bashir wa Sudan, mtu ambaye anakabiliana na mashtaka mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu, mjini The Hague, atahudhuria mkutano huo wa Istanbul. Wakati huo huo kulifanyika juhudi nyuma ya mapazia ya mkutano huo wa kilele kutaka al-Bashir asihudhurie mkutano huo. Ilitaja kwa njia isiokuwa rasmi huko Ankara kwamba upande wa Sudan ulifahamu shida ambayo itazuka kutokana na al-Bashir kushiriki katika mkutano huo. Ilijulikana kwamba serekali ya Sudan ilipelekewa risala ya upole kwamba kuwasili al-Bashir katika mkutano huo kungeweza kusababisha matatizo. Kwa hivyo, Rais huyo wa Sudan aliivunja safari yake hadi Uturuki, lakini alitaja sababu kuwa ni shughuli alizokuwa nazo kutokana na mashauriano yanayofanyika kuhusu matayarisho ya kufanyawa kura ya maoni hapo mwaka 2011 ambayo huenda ikaamuwa Kusini mwa Sudan iwe nchi huru. Kwa mujibuwa gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG, likinukulu vyombo vya habari vya Uturuki, ni kwamba Hassan al-Bashir alimpigia simu rais Abdullah Gül na kumuarifu kwamba alikuwa hana wakati wa kutembelea Istanbul.

Licha ya malalamiko kutoka Umoja wa Ulaya na jumuiya nyingine za kimataifa, Uturuki ilitetea mpango wa ziara hiyo ya al-Bashir. Kutoka wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki ilitajwa kwamb rais huyo wa Sudan anakwenda tu Uturuki kama mgeni wa Jumuiya ya nchi za Kiislamu duniani, na sio kutokana na mwaliko wa serekali ya Uturuki. Kukamatwa al-Bashir, kama vile inavoomba waranti iliotolewa na mahakama ya kimataifa hapo Machi mwaka huu OIC, ni jambo ambalo halijazuka kwa vile Uturuki haimo kati ya zile nchi 110 ambazo zimeuidhinisha ule mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo. Pia Rais Gül alisisitiza kwamba mkutano huo wa kilele ni wa jumuiya kimataifa ambayo wanachama wake wote wanabidi watendewe usawa. Wazi kabisa aliweka waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, ambaye aliutetea msimamo wa Uturuki. Alisema Muislamu, kimsingi, hawezi kufanya mauaji ya kiholela. Katika mahojiano ya redio, Erdogan alisema haamini kwamba huko Darfur watu wanalazimishwa kuchanganyishwa na jamii ya watu wengine au kunafanya mauaji ya kiholela.

Na kwa ripoti hiyo ya gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG ndio namaliza makala haya ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

Mwandishi :Miraji Othman

Mhariri : Mohammed Abdulrahman