1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo24 Agosti 2007

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, kuitembelea Libya mwezi Oktoba mwaka huu. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa larefusha tume ya kulinda amani nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/CHS2

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema waziri Rice ataitembelea Libya mwezi Oktoba mwaka huu. Kwa Condoleezza Rice na hata rais wa Marekani, George W Bush, upatanisho na Libya ni swala muhimu sana. Tangu Jumanne iliyopita, kiongozi wa idara inayohusika na maswala ya Mashariki ya Kati katika wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, David Welch, alikuwa mjini Tripoli Libya.

Lengo kubwa la ziara yake lilikuwa kufanya mazungumzo ya siku mbili na waziri wa mashauri ya kigeni wa Libya, Shalgam, pamoja na viongozi wengine wa serikali ili kuandaa ziara ya Condoleeza Rice nchini humo. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani nchini Libya tangu ziara aliyoifanya John Foster Dulles, mnamo mwaka wa 1953, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani wakati Dwight Eisenhower alipokuwa rais.

David Welch si kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kukaribishwa mjini Tripoli tangu mwishoni mwa mwaka 2003 wakati Marekani iliporudisha uhusiano wake na Libya. Mshauri wa rais Bush katika maswala ya usalama wa kitaifa na vita dhidi ya ugaidi, Frances Fragos Townsend, na naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Negroponte, wamewahi kuitembelea Libya.

Maendeleo yaliyopatikana katika wiki za hivi karibuni yanaongeza matumaini ya uhusiano kati ya Libya na Marekani kuendelea kuimarika. Uamuzi wa Libya kuwaachia huru wauguzi watano raia wa Bulgaria na daktari mmoja wa kipalestina waliokabiliwa na kifungo cha maisha gerezani kwa kuwaambukiza watoto zaidi ya 400 virusi vya ukimwi kwa makusudi katika hospitali ya Bengazi, ilikuwa hatua muhimu.

Gazeti la Süddeutsche lilikuwa na taarifa kuhusu hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kurefusha muda wa tume ya Umoja wa Afrika ya kulinda amani nchini Somalia kwa miezi sita. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amependekeza uwezekano wa kupeleka kikosi cha umoja huo kulinda amani nchini Somalia.

Uamuzi huo umeungwa mkono na wengi ikizingatiwa hali ya kibinadamu nchini Somalia ambayo imekuwa ikiendelea kuwa mbaya tangu majeshi ya serikali ya mpito ya nchi hiyo yakisadiwa na majeshi ya Ethiopia yalipofaulu kuwafukuza wanamgambo wa kiislamu mjini Mogadishu mwezi Disemba mwaka jana.

Gazeti la Süddeutsche pia liliripoti mauaji ya kiongozi wa mbari ya Abgal, Maalim Harun Yusuf, mjini Mogadishu. Mauaji hayo ni pigo kubwa kwa mazungumzo ya kitaifa yanayolenga kuzipatanisha mbari zinazohasimiana nchini Somalia. Kiongozi huyo wa umri wa miaka 63 alijua angekabiliwa na hatari kwa kuiwakilisha mbari yake kwenye mazungumzo ya amani yanayozijumulisha mbari nyengine na serikali ya mpito ya Somlia ya waziri mkuu Ali Mohamed Gedi.

Mada ya tatu inahusu raundi ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Sierra Leone kufanyika tarehe 6 mwezi ujao. Gazeti la Neue Zürcher lilisema matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi nchini Sierra Leone yalidhihirisha kiongozi wa upinzani Ernest Koroma akiongoza kwa asilimia 44.2 ya kura. Makamu wa rais wa chama tawala cha Sierra Leone People´s Party, SLPP, alifuatia katika nafasi ya pili akiwa na asilimia 38.3.

Mhariri wa gazeti hilo anasema matokeo hayo ni ishara kwamba raia wa Siera Leone wanataka mabadiliko ya kisiasa nchini mwao. Wapigaji kura wengi wanakilaumu chama tawala cha SLPP kwa kushindwa kuiendeleza nchi na kupunguza umaskini uliokithiri miongoni mwa raia.

Jimbo la Northrhine Westfallia litasaini mkataba wa ushirikiano na Ghana mwezi Novemba mwaka huu hapa mjini Bonn. Gazeti la General Anzeiger lilisema hayo kwa mujibu wa waziri anayehusika na kuwajumuisha wageni katika jimbo la Northrhine Westfalia, Armin Laschet. Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uchumi na wahamiaji kutoka Ghana watakuwa kama daraja kati ya Ujerumani na nchi yao.