1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo27 Julai 2007

Umoja wa Ulaya unataka kurejesha uhusiano wa karibu na Libya. Maandamano ya kutaka mfumo wa vyama vingi yafanyika nchini Swaziland. Umoja wa Mataifa waonya juu ya vita kuzuka upya nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Na rais wa Sudan, Omar el Bashir, asema jimbo la Darfur lina usalama na amani.

https://p.dw.com/p/CHSI

Umoja wa Ulaya unataka kurejesha uhusiano wa kawaida na Libya. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema, baada ya kuachiliwa huru wauguzi watano raia wa Bulgaria na daktari mmoja mpalestina, Umoja wa Ulaya sasa umetangaza enzi mpya ya uhusino wake na Libya.

Wataalamu hao wa afya walikuwa wakizuiliwa nchini Libya tangu mwaka wa 1999 wakikabiliwa na hukumu ya kifo kwa kuwaambukiza kwa makusudi watoto zaidi ya 400 virusi vya ukimwi. Ureno, ikishikilia sasa urais wa umoja huo, imeisifu hatua ya Libya kuwaachilia wataalamu hao wa afya na kusema inaongeza uwezekano wa kuimarisha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na Libya katika nyanja mbalimbali muhimu.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine pia alisema rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy kama alivyoshinda uchaguzi nchini Ufaransa ameshinda tena kwa kusaidia kuutanzua mzozo wa wauguzi wa Bulgaria na daktari mplaestina. Ufaransa iliwasaidia sana wataalamu hao na kupitia mke wa rais Sarkozy, Cecilia Sarkozy, aliyekwenda mjini Tripoli Jumatano iliyopita kwa mashauri ya kuachiliwa kwao, uhuru wao ukapatikana. Vyombo vya habari vya Ufaransa vilimtaja mke wa rais Sarkozy kuwa ´Super Cecilia.´

Naye mhariri wa gazeti la Neue Zürcher alisema kujerea kwa wauguzi wa Bulgaria na daktari mmoja mpalestina mjini Sofia kunafungua njia ya kuanza kwa uhusiano wa karibu sana baina ya Umoja wa Ulaya na Libya. Tayari umoja huo unapanga kufanya mazungumzo na Libya ufikie makubaliano baina ya pande hizo mbili.

Mada ya pili inahusu maandamno yaliyofanyika nchini Swaziland ya kutaka mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini humo. Gazeti la Neue Zürcher lilisema maelfu ya raia waliandamana mnamo Jumatano iliyopita mjini Manzini, mji wa pili mkubwa nchini Swaziland. Shughuli zote za kibiashara zilikatizwa na mgomo huo mjini humo huku maduka na maeneo mengi ya biashara yakibakia kufungwa. Maandamano hayo yalifanyika kwa amani na kumalizika Alhamisi.

Mfalme Mswati III bado anaitawala Swaziland akiwa na mamlaka makubwa licha ya katiba mpya kuundwa mnamo mwaka wa 2005. Vyama vya kisiasa sasa ni halali ingawa miaka kadhaa iliyopita ilikuwa marufuku kuwa na chama cha kisiasa nchini Swaziland. Hata hivyo vyama haviwezi kushiriki katika uchaguzi.

Mfamle Mswati hayuko chini ya sheria na ana mamlaka ya kuwateua majaji na mawaziri na kuwatimua jinsi atakavyo. Waandamanaji wa mjini Manzini wanataka wagombea wa urais waruhusiwe kugombea kwenye uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao nchini Swaziland.

Mada ya tatu inahusu onyo la Umoja wa Mataifa juu ya kuzuka tena vita nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Tageszeitung lilisema baraza la usalama la umoja huo lina wasiwasi mkubwa juu ya hali mbaya ya usalama nchini Kongo na limetoa mwito suluhisho la kisiasa na la kidiplomasia lipatikane ili kuumaliza mzozo ulio nchini humo.

Katika kikao chake cha Jumatatu iliyopita, baraza la usalama lilitaka makundi ya waasi ya kigeni yaliyo mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kama vile kundi la waasi wa Rwanda la FDLR, yavunjwe. Baraza la usalama pia limetaka kufanyike mdahalo kati ya makundi ya waasi, serikali ya Rwanda na Kongo. Jeshi jipya la taifa la Kongo linatakiwa liundwe nchini ya usimamizi wa tume ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUC.

Likitukamilishia uchambuzi wetu hii leo gazeti la Tageszeitung liliripoti kuhusu sifa zilizotolewa na rais wa Sudan kuhusu jimbo la Darfur. Gazeti hilo lilisema rais Omar Hassan el Bashir wa Sudan amelieleza jimbo la Darfur kuwa salama na lenye amani na anataka kupunguza tume ya Umoja wa Mataifa katika eneo hilo. Aliyasema hayo Jumapili iliyopita alipokuwa akihutubia baraza lake la mawaziri mjini Khartoum baada ya kufanya ziara ya siku tatu Darfur.

Rais Bashir alisema aliona watu wakiishi maisha ya kawaida na kwamba ripoti juu ya mashambulio, mauaji ya raia na janga la kibinadamu, ni uongo mtupu wa nchi za magharibi. Mhariri wa gazeti la Tageszeitung alimueleza rais Bashir kuwa katika ndoto na anajifanya haoni yanayondelea Darfur. Umoja wa Ulaya bado haujaanza mazungumzo juu ya mpango wa kupeleka majeshi kuwasaidia wakimbizi wa Sudan walio katika kambi za wakimbizi mashariki mwa Chad.