1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo6 Julai 2007

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wapinga kuundwa kwa nchi moja ya Afrika. Ghana kuwa mshirika wa jimbo la North Rhine Westphalia hapa Ujerumani. Mashirika ya kuandaa safari za watalii ya Ujerumani yakosolewa kwa kutoa maelezo ya uongo kuhusu bara la Afrika.Na kesi dhidi ya kampuni ya Marekani Pfizer yaanza nchini Nigeria.

https://p.dw.com/p/CHSU

Kuhusu mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliofanyika mjini Accra Ghana, gazeti la Süddeutsche lilisema mkutano huo ni pigo kubwa kwa rais wa Libya Muamar Gaddafi ambaye alitaka kuundwe nchi moja ya bara la Afrika, yaani United States of Africa. Mazungumzo ya viongozi wa serikali zaidi ya 50 za Afrika yaliodumu kwa siku tatu kuanzia Jumapili iliyopita na kumalizika Jumanne usiku, yalipinga kuundwa mara moja kwa serikali hiyo.

Rais Gaddafi akiungwa mkono na rais wa Senegal Abdoulaye Wade, alitaka kwa haraka kuundwe nchi moja ya Afrika itakayokuwa na jeshi lake. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche alimnukulu rais Gaddafi akihoji kwamba ipo haja ya bara la Afrika kuungana wakati huu wa utandawazi duniani. Wanachama wa Umoja wa Afrika walikubaliana kuwa na ushirikiano wa karibu wa kisiasa na kiuchumi.

Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema kulikuwa na hali ya kuchanganyikiwa miongoni mwa viongozi. Rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika, Alpha Oumar Konare, alinukuliwa na gazeti hilo akisema kumalizika kwa mkutano wa Accra kulidhihirisha hali ya kuchanganyikiwa na kupinga wazo la rais wa Libya, Muamar Gaddafi, la kuundwa kwa haraka serikali ya nchi moja ya Afrika.

Gaddafi ambaye alisafiri na msafara wake wa magari kutoka Tripoli Libya hadi Accra Ghana na kuishi kwenye mahema pamoja na ujumbe wake mjini Accra, alitaka kuundwe serikali ya Afrika itakayokuwa na mawaziri 15. Rais wa Ghana John Kufuor na Alpha Oumar Konare walisema mwishoni mwa mkutano huo kwamba wazo hilo ni zuri ila linahitaji muda zaidi.

Ndio maana kukaundwa tume nne zitakazochunguza vipi na lini nchi moja ya Afrika itakapoweza kuundwa. Tume hizo zinatarajiwa kuwasilisha mapendekezo yao kwenye mkutano mwingine wa kilele wa Umoja wa Afrika uliopangwa kufanyika Januari mwaka ujao.

Mada ya pili ilihusu Ghana kuwa mshirika wa jimbo la North Rhine Westafalia hapa Ujerumani. Mhariri wa gazeti la Rheinishe Post akimnukulu mtaalamu wa uchumi Chris Bollenbach, wakati alipokuwa akiuhutubia mkutano wa mwaka wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, alisema Ghana ni miongoni mwa nchi zilizoimarika na kuendelea kiuchumi barani Afrika.

Wahamiaji kutoka Ghana wanaongoza kwa idadi katika jimbo la North Rhie Westfalia na tayari kuna mashirika kati ya 60 na 70 yasiyo ya kiserikali ambayo yanadhamini miradi ya elimu na kilimo nchini Ghana. Hizi ni sababu tosha za kuwepo ushirikiano baina ya Ghana na jimbo hilo. Bollenbach alimueleza waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westfalia, Jürgen Rüttgers, kuwa atasafiri kwenda Ghana mwaka ujao. Tayari jimbo la North Rhine Westfalia lina ushirikiano na jimbo la Mpumalanga nchini Afrika Kusini.

Maelezo yanayotolewa na makampuni yanayoandaa safari za watalii kuhusu bara la Afrika yanapotosha. Hayo yalisemwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine. Mhariri wa gazeti hilo alisema habari zinazotolewa kuhusu Afrika hazizingatii sana ukweli wa mambo katika maisha ya kijamii na maswala ya kiuchumi.

Ripoti ya uchunguzi uliofanywana na shirika la maendeleo la makanisa ya kiinjili, hapa Ujerumani, EED, imebaini kuwa baadhi ya katalogi zinatukuza ukoloni. Maelezo yanayotumiwa katika matangazo ya kibiashara kwenye katalogi hizo yanaiacha nje miji mikubwa na wakaazi wake.

Hatua hiyo inazidi kutoa picha ya Afrika kama bara ambalo limelala na lisilo na maendeleo yoyote. Ipo haja ya kueleza picha halisi kuhusu Afrika ingawa wazo hilo halimo katika masilahi ya wafanyibishara wa safari za watalii. Mhariri alimalizia kwa kusema kutoa picha mbaya kuhusu Afrika kunaongeza uwezekano wa Waafrika kubaguliwa hapa Ujerumani.

Mada ya mwisho inahusu kuanza kwa kesi dhidi ya kampuni ya kimarekani ya Pfizer nchini Nigeria Jumatano iliyopita. Miaka 11 sasa imepita tangu watoto takriban 50 kufariki katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria kutokana na majaribio ya dawa ya Trovan iliyotengezwa na kampuni hiyo ya Pfizer.

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na waakazi wa jimbo la Kano, watoto wengine wasiopungua 50 walipata ulemavu kutokana na dawa hiyo. Nigeria inadai kiasi cha dola bilioni saba kutoka kwa kampuni ya Pfizer kama fidia kwa jamii za waathiriwa.