1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI

Abdu Said Mtullya1 Agosti 2011

Magazeti ya Ujerumani yaizingatia hali ya Pembe ya Afrika .

https://p.dw.com/p/127Dj
Umoja wa Mataifa umeanza kupeleka chakula nchini Somalia.Picha: AP

Magazeti karibu yote ya Ujerumani yameripoti juu ya maafa yaliyosababishwa na ukame kwenye eneo la Pembe ya Afrika. Magazeti hayo pia yameandika juu ya migogoro ya Sudan, na vita vya nchini Libya.

Juu ya janga la njaa kwenye Pembe ya Afrika, gazeti la Frankfurter Allgemeine limeripoti juu ya juhudi zilizoanzishwa na Umoja wa Mataifa jumatano iliyopita za kuyaokoa maisha ya mamilioni ya watu, na hasa ya watoto waliomo katika hatari ya kufa njaa nchini Somalia.

Gazeti hilo limearifu kwamba Jumatano,ndege ya kwanza ya Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa, WFP,iliruka kutoka Nairobi kuelekea Mogadishu. Ndege hiyo ilibeba tani 10 za chakula kilichoongezewa lishe maalumu.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limetilia maanani katika taarifa yake kuwa zoezi hilo la Umoja wa Mataifa lilipangwa kuanza siku moja kabla ya hapo, lakini kutokana na matatizo ya ushuru lilicheleweshwa kwa siku moja. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limewakariri maafisa wa shirika la chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, wakiarifu kuwa lengo la shirika hilo ni kupeleka nchini Somalia tani mia moja za chakula kila mwezi.

Gazeti jingine kutoka mji wa Frankfurt, Frankfurter Rundschau,pia limechapisha makala juu ya mafaa ya njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika. Gazeti hilo limefanya mahojiano na kamishna wa serikali ya Ujerumani juu ya masuala ya Afrika, Günther Nooke.

Katika mahojiano hayo, kamishna huyo amezungumzia juu ya mambo yaliyosababisha njaa kwenye Pembe ya Afrika na barani Afrika, kwa jumla. Bwana Nooke amesema katika mahojiano na gazeti hilo, kwamba maafa ya njaa barani Afrika hayasababishwi na ukame peke yake.

Amesema zipo sababu nyingine. Ametoa mfano wa Somalia ambako kwa muda wa miaka mingi pemekuwapo vita vya wenyewe kwa wenyewe. Katika mahojiano hayo mshauri huyo wa serikali ya Ujerumani juu masuala ya Afrika, bwana Nooke, pia amezungumzia juu ya tuhuma kwamba nchi kama Ethiopia inauza ardhi kwa wajasiramali wanaotoka nje, kama vile China. Bwana Nooke ameeleza kuwa sera ya kuzalisha chakula kwa ajili ya kuuza nje itasababisha migogoro ya kijamii barani Afrika.

Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, bwana Ali Ahmed Karti, ameyakanusha madai kwamba malaki ya watu wamekufa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika jimbo la Darfur.

Hizo ni habari zilizochapishwa na gazeti la Die Presse wiki hii. Katika mahojiano na gazeti hilo, Waziri Ali Ahmedi amesema watu waliokufa katika jimbo la Darfur ni kiasi ya alfu 30, na siyo alfu mia tatu.!

Gazeti la Der Tagespiegel wiki hii linameyazingatia matukio ya nchini Libya. Katika makala yake gazeti hilo linauliza jee kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Gaddafi, ndiye atakaenufaika na makubaliano ya kuutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya mazungumzo?

Katika taarifa yake,gazeti hilo limemnukulu Kamanda wa Marekan, Jenerali Michael Mullen, akisema kuwa kijeshi,mambo yamekwama nchini Libya. Gazeti hilo limeeleza kuwa hata baada ya miezi minne tokea ndege za Nato zianze kumshambulia Gaddafi, majeshi yake yameweza kuwazuia wapinzani kuingia katika mji Mkuu,Tripoli.

Der Tagesspiegel pia limefahamisha kuwa ndege za Nato zimeingia katika anga ya Libya mara 16,689 na zimefanya mashambulio 6285. Vita vya nchini Libya tayari vimeshagharimu kiasi cha dola bilioni moja na nusu limefahamisha gazeti hilo. Kwa hiyo sasa pana ishara za kwanza zinazoonyesha kwamba mgogoro wa nchi hiyo unaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na pia lipo wazo kwamba Gaddafi anaweza kuendelea kubakia nchini baada ya kuondoka madarakani.

Gazeti la Der Tagesspiegel limemnukulu kiongozi wa Baraza la Mpito, Mustafa Abdel Jalil, akiliambia gazeti la Wall Street Journal katika mahojiano kwamba Gaddafi anaweza kubakia nchini, lakini kwa masharti ya wapinzani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman