1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI.

Abdu Said Mtullya14 Novemba 2011

Magazeti ya Ujerumani yaandika juu ya Julius Malema.

https://p.dw.com/p/13A5I
Aliekuwa Kiongozi wa tawi la vijana la chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, Julius Malema .Picha: AP

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya Julius Malema aliepewa adhabu ya kusimamishwa uanachama wa ANC kwa muda wa miaka mitano.

Katika taarifa yake kutoka Jonannesburg, ripota wa gazeti hilo anasema Simba mdogo-Julius Malema sasa hataunguruma kwa muda wa miaka mitano. Mwandishi huyo Martina Schwikowski amerifu kwamba Kiongozi wa tawi la vijana la chama tawala nchini Afrika Kusini ANC, Julius Malema amepatikana na hatia ya kuiharibu sifa ya chama na ya nchi.

Kamati ya nidhamu ya chama hicho imemtia hatiani Malema, kwa makosa hayo na kumpa adhabu ya kumsimamisha uanachama kwa muda wa miaka mitano. Ripota wa gazeti la die Tageszeitung ametilia maanani katika taarifa yake kwamba wafuasi wa Malema waliamua kutulia kimya baada ya adhabu kutangazwa tofauti na ilivyokuwa mnamo mwezi wa agosti.

Maalfu ya vijana walikusanyika mbele ya makao makuu ya chama cha ANC wakati kamati ya nidhamu ya chama hicho ilipokutana kusikiliza kesi ya Malema anaeitwa JUJU na wafuasi wake. Mnamo mwezi huo wa agosti vijana hao walifanya fujo kuashiria msimamo wa kumuunga mkono kiongozi wao. Lakini ripota wa gazeti la die Tageszeitung amearifu kutoka Johannesburg kwamba safari hii wafuasi wa Malema wameamua kuwa watulivu!

Gazeti la die Tageszeitung wiki hii pia limeyatupia macho matukio ya kisiasa nchini Liberia ambako raundi ya pili ya uchaguzi wa Rais imefanyika. Katika makala yake gazeti hilo limetilia maanani kwamba kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, CDC bwana Winston Tubmann ameususia uchaguzi huo wa raundi ya pili. Pamoja na hayo amesema hatayatambua matokeo ya uchaguzi huo. Gazeti la die Tageszeitung pia limearifu kuwa idadi ya wapiga kura ilikuwaya chini safari hii.

Rais aliemo madarakani EllenJohnson Sirleaf ameshinda katika raundi hiyo ya pili na ataendelea kuiongoza Liberia.

Gazeti la der Tagespiegel wiki hii limendika juu ya kile inachokiita"Mkasa wa Afrika" .Gazeti hilo linaeleza kwa ufupi. Mama mmoja aliuawa mnamo mwaka wa 2003 nchini Burundi. Wauaji walifika nyumbani kwake asubuhi ya saa 12. Watoto wake wawili walikimbia baada ya kuona mama yao na dada yao wameuliwa .

Kwa muda wa miaka mingi watoto hao walifanya juhudi za kumtafuta baba yao wa kisomali. Hatimaye walimwona baba yao. Lakini walishtuka kutambua kwamba alikuwa kiongozi wa kikundi kimoja cha al -Shabaab. Baada ya mauaji kutokea ndugu hao walikimbilia njia mbalimbali. Walipoteana kwa muda wa miaka mitano kabla ya kukutana tena .

Kwa sababu hapakuwa na mtu alieyaamini waliyokuwa wanayasema, waliamua kumtafuta baba yao waliemwona kwa mara ya mwisho miaka miwili, kabla ya mkasa wa kuuawa kwa mama yao. Ndugu hao walikutana tena Kenya.

Juhudi za kumtafuta baba yao zilifanikiwa, ila tu walitambua kwamba baba yao wa kisomali ni kiongozi wa al-Shaabab- yaani wanaitikadi kali wa kiislamu . Ndugu hao wawili Abdul na Ali sasa wamo tena hatarini.

Gazeti la der Freitag wiki hii limechapisha makala juu ya dhamira ya wamarekani ya kuenda Sudan ya Kusini kama watoaji misaada ya maendeleo. Lakini gazeti hilo linaarifu kwamba ni mafuta ya petroli yanayowapeleka wamarekani hao Sudan ya Kusini.

Katika makala yake gazeti la der Freitag linasema tokea Sudan ya Kusini itangaze uhuru wake,Marekani imeonyesha dhamira kubwa ya kusaidia katika kuendeleza miundombinu itakayosaidia katika shughuli za uzalishaji wa mafuta katika Sudan ya Kusini.

Gazeti la der Freitag limemkariri Mjumbe maalamu wa Marekani katika Sudan Princeton Lyman ,akisema kuwa mipango inafanyika ili kuyaruhusu makampuni ya mafuta ya Marekani kufanya biashara katika Sudan ya Kusini licha ya vikwazo vilivyopo.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika juu ya Afrika kutokea, New York. "Rekodi na donge nono kwa G. Mutai" linasema katika makala yake.

Gazeti hilo limeripoti juu ya mbio za marathoni zilizofanyika New York ambako mkimbiaji huyo kutoka Kenya Geofrey Mutai alishinda kwa kuwaacha wakimbiaji wengine nyuma sana. Gazeti hilo linasema haijawahi kutokea katika miaka karibu 20 iliyopita katika mbio hizo za New York. Mutai alikimbia kwa muda wa saa 2.dakika tano,na sekunde 6. Na kwa ufanisi huo alilipwa zaidi ya dola nusu milioni.

Mwandishi Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/-Othman Miraji/