1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya26 Agosti 2012

Pamoja na masuala mengine wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kifo cha aliekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi na mgomo wa wafanyakazi wa migodini nchini Afrika Kusini

https://p.dw.com/p/15wtW
Aliekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi
Aliekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles ZenawiPicha: picture-alliance/dpa

Juu ya kifo cha aliekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi gazeti la "Suddeutsche Zeitung" linatilia maanani kwamba Zenawi alileta ustawi wa uchumi katika nchi ambayo hadi miaka ya hivi karibuni ilipoteza idadi kubwa ya watu wake kutokana na baa la njaa.

Gazeti la"Suddeutsche"limeandika juu ya Zenawi kwamba kutokana na wasifu wake mtu anaweza kusema kuwa  mwanasiasa huyo alikuwa kiongozi alieng'ara kama nyota. Lakini kila alipotokea hadharani hakuwa hivyo. Inafahamika kwamba hakuwa mtu wa tabasamu.Yumkini tabia hiyo ilitokana na historia yake ya miaka ya nyuma, kwani alikuwa mpiganaji, pamoja na waasi katika vita vya kumng'oa dikteta Mengistu  Mariam.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linasema katika makala yake kuwa Zenawi ameacha mfumo ambao masharika ya misaada yanauita,wa maendeleo ya  kidikteta. Hata hivyo gazeti hilo limetilia maanni ,kwamba uchumi wa Ethiopia umekuwa unastawi vizuri kutokana na uongozi  wake. Zenawi alifariki dunia  jumanne iliyopita akiwa na umri wa miaka 57.

Wafanyakazi wa migodi 44 waliuawa baada ya kushambuliwa na polisi nchini Afrika Kusini. Hizo ni habari  zilizoandikwa na gazeti la "Die Welt". Gazeti hilo linasema mauaji hayo yanakumbusha enzi za utawala wa makaburu .Gazeti hilo linaeleza zaidi kuwa Polisi waliokuwa na bunduki, hawakusita kufyatua risasi na kuwauwa  wafanyakazi wa mgodi wa Marikana wa madini ya platinum Alhamisi ya wiki iliyopita.

Gazeti la "Die Welt" linasema katika makala yake kwamba mauaji hayo  yanakumbusha yaliyotokea katika enzi za utawala wa kibaguzi katika vitongoji vya Soweto, Sharpeville, Soweto na Bisho. Hata hivyo gazeti la "Die Welt" linaeleza kuwa mauaji yaliyotokea katika enzi za makaburu yalifanyika kwa niaba ya serikali ya kibaguzi iliyokuwa inawakandamiza Waafrika. Lakini yalitokea Marikana yalitokana na harakati za tabaka la wafanyakazi dhidi ya kampuni za kimataifa.

Gazeti la "Die  Welt" linaeleza katika makala yake kuwa wafanyakazi wanahisi kuwa wanapunjika, kwani wanalipwa ujira wa Euro mia nne kwa mwezi kwa kazi ngumu na ya hatari kubwa wanayoifanya kwenye migodi.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" limechapisha makala juu ya mzozo ulitokea katika kijiji cha Reketa kwenye wilaya ya Tana River nchini Kenya. Mzozo huo baina ya  makabila ya wapokomo na waorma ulisabaisha vifo vya watu karibu 48 na kati ya hao 31 walikuwa wanawake na watoto 11 Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba mzozo huo ulisababishwa na mapambano ya kugombea maji na sehemu za malisho ya mifugo. Lakini gazeti hilo limetilia maanani katika makala yake kwamba mauaji hayo yametokea wakati Kenya inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu mnamo mwezi wa machi hapo mwakani.

Gazeti la "Süddeutsche linasema mauaji ya wilayani Tana River yanakumbusha machafuko yaliyotokea Kenya baada ya kufanyika uchaguzi wa Rais, mwishoni mwa mwaka wa 2007. Watu wa makabila mbambali zaidi ya 1100 waliuawa kutokana na  kampeni za chuki zilizochochewa na wanasiasa.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia juu ya wasi wasi unaotokana na kujitandaza kwa mtandao wa al-Qaeda barani Afrika.

Gazeti hilo linaeleza kwamba kutokana na shinikizo la majeshi ya Nato nchini Afghanistan,wigo wa operesheni za mtandao huo umekuwa mdogo.Pamoja na hayo wenyeji wao wameshachoshwa. Na kuhusu Pakistan, ni serikali ya nchi hiyo itakayoamua iwapo,watu wa al-Qaeda wataendelea kujibanza katika jimbo la Waziristan. Kwa hivyo,al-Qaeda inahitaji sehemu yenye mazingira yatakayowafaa ambako mipaka na taasisi za dola ni dhaifu.Gazeti la "Frankfurter  Allgemeine" linasema sehemu hiyo ni Afrika.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman