1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya25 Januari 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya mgogoro wa Mali,juu ya mradi wa Waziri Dirk Niebel wa kuhimiza uelewano baina ya Ujerumani na Afrika na juu ya mitumba kutoka Ujerumani

https://p.dw.com/p/17RXq
Waziri wa Ujeurmani wa ushirikiano wa maendeleo Dirk Niebel
Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo Dirk NiebelPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Bild Zeitung" linalouliza jee, bara la Afrika sasa linatekwa na Waislamu wenye itikadi kali? Gazeti hilo limechapisha makala juu ya ugaidi nchini Mali,Algeria na Nigeria.Katika makala hiyo gazeti hilo limeyaorodhesha matukio yanayowahusisha waislamu wenye itikadi kali.

Gazeti hilo linasema jeshi nchini Algeria limepambana na magaidi katika juhudi za kuwakomboa watu zaidi ya 40 waliotekwa nyara na magaidi wenye uhusiano na al-Qaeda .Nchini Mali wanajeshi wa Ufaransa wanapambana na waasi wa Mali wenye itikadi kali.

Juu ya hatari ya magaidi barani Afrika gazeti la "Bild am Sonntag" limeandika maoni. Linasema. Ujerumani imejizatiti katika harakati za kupambana na magaidi ambao ni waislamu wenye itikadi barani Afrika. Gazeti hilo linasema ni wazi kwamba Waafrika wenyewe wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika harakati hizo.Lakini jeshi la Mali bado ni dhaifu. Sasa kinachohitajika ni kuujenga uwezo wa majeshi ya Afrika kwa kuyaunga mkono kwa fedha.

Gazeti la"Der Tagesspiegel"pia limeandika juu ya Mali,lakini kwa kuingalia timu ya kandanda ya Mali inayoshiriki katika mashindano ya kugombea ubingwa wa mataifa ya Afrika nchini Afrika kusini.

Malian soldiers speak to journalists in Niono January 19, 2013. African leaders meeting in Ivory Coast on Saturday are expected to sign off on a regional mission that is due to take over from French forces fighting al Qaeda-linked militants in Mali, but is still short on financing and planning. REUTERS/Joe Penney (MALI - Tags: CIVIL UNREST POLITICS MILITARY CONFLICT)
Wanajeshi wa MaliPicha: Reuters

Katika taarifa yake mwandishi wa gazeti hilo anaeleza kuwa tabasamu haizionekani wazi katika nyuso za wachezaji wa timu ya kandanda ya Mali.Gazeti la "Der Tagesspiegel" limemkariri mchezaji mmoja Sigamary Diarra akisema kuwa miili yao ipo kiwanjani Afrika Kusini,lakini nyoyo zao wakati wote zipo nyumbani kwa ndugu na jamaa.

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel ameingia katika lawama kutokana na mradi wake wenye lengo la kuhimiza uelewano baina ya Ujerumani na nchi za Afrika. Hizo ni habari zilizoandikwa na jarida la "Der Spiegel".

Jarida hilo linaeleza kuwa mpango wa Waziri Niebel wa kuendeleza uelewano baina ya Ujerumani na nchi za Afrika unagharimu Euro Milioni nane.Lakini kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa katika hatua mbalimbali,mafanikio ya mpango huo bado hayajaonekana wazi.

Jarida la "Der Spiegel" limearifu kwamba lawama zinazoelekezwa kwa Waziri Niebel zinatokana na kushiriki kwa "Wakfu wa Ushirikiano na Afrika" katika mradi huo.Jarida la"Der Spiegel" linasema katika taarifa yake kwamba Wakfu huo umeshindwa kuonyesha usimamizi mzuri wa fedha.

Gazeti la"Kölner Stadt-Anzeiger"wiki hii limechapisha makala juu ya mitumba inayokusanywa nchini Ujerumani.Linauliza jee nguo hizo kiasi, cha tani laki saba na nusu zinaenda wapi? Gazeti hilo linaeleza: Biashara ya mitumba imestawi na kuwa soko kubwa sana. Wataalamu wanakadiria kwamba mitumba kiasi cha tani laki saba na nusu zinakusanywa nchini Ujerumani kila mwaka.Gazeti la "Kölner Stadt Anzeiger"linaeleza kuwa nguo hizo zinakusanywa kwa ajili ya masikini nchini Ujerumani.Lakini haziwafikii wakati wote.

Gazeti la"Kölner Stadt-Anzeiger " limearifu kuwa nguo hizo zinapelekwa nje ya Ujerumani katika nchi kama Tanzania na Kenya. Gazeti hilo limewakariri wataalamu wakisema,kuwa asilimia 50 ya watu nchini Tanzania wanatumia mitumba.Na jee mitumba hiyo inaviua viwanda vya nguo nchini Tanzania.

Mtaalamu, Friedel Hütz Adams amekaririwa na gazeti la"Kölner Stadt-Anzeiger" akisema: ukweli ni kwamba biashara ya nguo kuu kuu, imechangia kwa kiwango kikubwa katika kuviua viwanda vya nguo katika nchi nyingi za Afrika."

Kati ya mwaka1981 na 2000 biashara ya mitumba imesababisha uzalishaji wa viwanda vya nguo kuanguka kwa asilimia 40 na kuteketea kwa nafasi za ajira kwa asilimia 50 katika nchi za Afrika.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri: M.Abdul-Rahman