1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya17 Mei 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Mali, juu ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya Afrika na pia yameandika juu ya ghasia zinazotokea nchini Nigeria

https://p.dw.com/p/18a6r
Mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Mali
Mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya MaliPicha: REUTERS

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaarifu juu ya mkutano uliofanyika mjini Brussels mapema wiki hii ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kuijeenga upya Mali.

Gazeti hilo limearifu kwamba wafadhili wameahidi kutoa kwa jumla kiasi cha Euro Bilioni 3, 25 Ujerumani peke yake imeahidi kutoa Euro Milioni mia moja.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine "linafahamisha zaidi kwamba fedha zilizoahidiwa zitatumika kwa ajili ya kuyakabili matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na vita nchini Mali.Gazeti hilo limearifu kwamba njia ya ufanisi ya kuyapunguza matatizo ya Mali ni kuekeza katika kilimo na miundombinu.

Ujerumani yatoa mafunzo ya kijeshi:

Gazeti la "Die Welt" limeandika juu ya mafunzo yanayotolewa na Ujerumani kwa wanajeshi wa Mali.Lakini gazeti hilo linasema kwamba pana tatizo kubwa juu ya mafunzo hayo. Linatufahamisha zaidi kuwa tatizo ni kwamba jeshi la Mali limegawanyika na baadhi ya askari wanawaunga mkono Waislamu wenye itikadi kali.

Gazeti la "Die Welt" pia limefahamisha juu ya tatizo lingine linalolikabii jeshi la Mali. Gazeti hilo limemkariri mwandishi wa habari mmoja wa Mali,Adam Thiam akisema kwamba Mali haina jeshi bali ina askari tu. Mwandishi habari huyo amekaririwa na gazeti la "Die Welt" akieleza kwamba mtu anaweza kusema kuwa nchini Mali wapo askari lakini hakuna jeshi.

Ujerumani inakijua kinachohitajika nchini Mali:

Hata hivyo Luteni Kanali wa jeshi la Mali amesema mchango wa Ujerumani katika kulijenga jeshi la Mali ni muhimu.Amenukuliwa na gazeti la "Die Welt" akisema kuwa Wajerumani wapo nchini Mali muda mrefu sasa na kwamba wanakijua kile ambacho jeshi la Mali linakihitaji"

Mali inaungwa mkono na Niger vile vile, na Rais wa nchi hiyo amesema majeshi ya nchi yake yataendelea kuwapo Mali kwa kadri yatavyoendelea kuhitajika.Rais huyo Mahamadou Issoufou ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" Rais Issoufou ameliambia gazeti hilo kwamba majeshi yake yapo katika mji wa Gao. Lakini pia yapo katika miji ya Meneka na Asongo."Majeshi yetu yataendelea kuwapo nchini Mali hadi hapo tutakapoifikia shabaha yetu."

Rais Issoufou wa Niger ameliambia gazeti la "Frankfurter Allgemeine"kwamba malengo ya jeshi la nchi yake ni kurejeshwa kwa himaya kamili ya Mali na kuandaliwa kwa uchaguzi huru.

Hali ya hatari yatangazwa

Gazeti la"die tageszeitung" limeyatupia macho matukio ya nchi Nigeria.Gazeti hilo limechapisha ripoti juu ya hatua ya Rais Goodluck Jonathan ya kutangaza hali ya hatari katika mjimbo ya kaskazini mwa Nigeria.

Machafuko nchini Nigeria
Machafuko nchini NgeriaPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti hilo limefahamisha kuwa Rais Goodluck Jonathan ametangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno,Yobe na Adamawa kaskazini mwa Nigeria. Gazeti la "die tageszeitung" limetilia maanani kwamba serikali ya Nigeria imewapeleka wanajeshi 2000 katika mji wa Maiduguri uliopo katika jimbo la Borno.Mji huo unatumiwa kama makao makuu ya kundi la Waislamu wenye siasa kali - Boko Haram. Kutokana na machafuko ya hivi karibuni watu zaidi ya 250 waliuawa nchini Nigeria kufuatia mapambano baina ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa kundi la Boko Haram.

Kodi kwa ajili ya maendeleo ya Afrika :

Gazeti la masuala ya kiuchumi "Wirtschftswoche" limeripoti juu ya pendekezo la Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo bwana Dirk Niebel.

Gazeti hilo linaeleza kwamba kodi siyo jambo linaloungwa mkono na chama cha Waziri huyo, FDPnchini Ujerumani. Lakini anataka watu katika nchi za Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara walipe kodi ili wayagharamie mandeleo yao.Waziri Niebel amekaririwa akisema, nchi zinazoendelea zilipata msaada thamani ya Euro zaidi Bilioni 100 mnamo mwaka wa 2011. Lakini watu wakilipa kodi katika nchi hizo watakivuka kiwango hicho. Ni hoja ya Waziri huyo kwamba, kutokana na ustawi mzuri wa uchumi barani Afrika watu wengi zaidi wataweza kulipa kodi na kugharimia maendeleo yao.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deustche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu