1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya24 Novemba 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kesi inayowakabili Rais Kenyatta wa Kenya na makamu wake Ruto na pia yameandika juu ya kijana maarufu wa Afrika Kusini Julius Malema

https://p.dw.com/p/1ANMt
Kijana maarufu wa Afrika kusini Julius Malema
Kijana maaruf wa Afrika Kusini Julius MalemaPicha: Reuters

Lakini tunaanza na makala iliyochapishwa na gazeti la "die tageszeitung" juu ya shinikizo linalofanywa na nchi za Afrika kutaka sheria za Mahakama Kuu ya Kimataifa ;ICC zibadilishwe. Kwa usemi mwingine nchi hizo zinataka kubadilishwa kwa msingi wa sheria zinazofuatwa na Mahakama hiyo inayopambana na uhalifu,I

Gazeti hilo linatilia maanani katika makala yake kwamba kwenye mkutano wa mwaka wa nchi wanachama wa Mahakama Kuu ya Kimataifa ya mjini The Hague,ICC Kenya ikiungwa mkono na nchi nyingine za Afrika imewasilisha ombi la kujadiliwa kwa uwezekano wa kukiondoa katika sheria za mahakama hiyo, kipengele kinachowezesha kushtakiwa kwa marais waliomo madarakani.

Gazeti la "die tageszeitung" linasema utata unaotokana na msimamo wa nchi za kiafrika kutaka marais waliomo madarakani wapewe kinga dhidi ya kufikishwa mahakamani, umesababisha mvutano baina ya nchi hizo na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague.

Julius Malema

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limeandika juu ya mkasa wa kijana maarufu wa Afrika Kusini Julius Malema. Malema anakabiliwa na tuhuma za rushwa. Na jumatatu iliyopita alifikishwa mbele ya mahakama ya Polokwane.

Gazeti la "die tageszeitung" linatuhafamisha zaidi kwamba Julius Malema sasa anaweza kushiriki katika uchaguzi. Mahakama ya mjini Polokwane katika jimbo la Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini imeahirisha kesi inayomkabili ya tuhuma za wizi. Malema anatuhumiwa na mwendesha mashtaka wa serikali kufanya njama za kupata tenda ya ujenzi wa barabara thamani ya Rand Milioni 52 na kwamba yeye amejinufaisha kwa kiwango kikubwa na tenda hiyo. Kesi hiyo itasikilizwa tena mnamo mwezi wa septemba mwaka ujao.

Gazeti la "die tageszeitung" linafahamishha zaidi katika makala yake kwamba, kutokana na kuahirishwa kwa kesi, Malema ataweza kugombea Urais mwezi Aprili mwaka ujao kwa tiketi ya chama chake kipya kinachoitwa "Economic Freedom Fighters."

Biashara peke yake siyo suluhisho la mabadiliko ya tabia nchi

Gazeti la" Neues Deutschland" wiki hii limefanya mahojiano na mwanaharakati wa ulinzi wa mazingira Ruth Nyambura kutoka mtandao wa uhai anuai.Katika mahojiano hayo mwanaharakati huyo amesema kuwa mfumo wa soko hautalitatua tatizo la mabadiliko ya tabia nchi .Bibi Ruth Nyambura ameliambia gazeti la "Neues Deutschland" kwamba kilimo kinapaswa kuwa cha asili na kwamba wakulima hawahitaji kemikali,yaani madawa,kwa ajili ya kuzalisha mazao zaidi.

Mwanaharakati huyo ameeleza kuwa madawa,njama za kubadili asili ya mbegu na matumizi ya nishati za kale ni mambo yanayochangia katika kusababisha mabadiliko ya tabia nchi. Amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha uhaba wa raslimali, jambo linalochochea migogoro baina ya jamii mbalimbali katika nchi nyingi za Afrika.

Ujerumani yasaidia polisi watesaji Kenya

Ujerumani imegeuka kuwa rafiki wa polisi watesaji wa nchini Kenya. Habari hizo zimeandikwa nagazeti la "Süddeutsche Zeitung" Gazeti hilo linafahamisha katika taarifa yake kwamba idara Kuu ya Ujerumani ya kupambana na uhalifu,BKA inatoa mafunzo kwa kikosi maalumu cha Kenya.Gazeti hilo linauliza jee vipi kuhusu haki za binadamu?

Gazezi la Neues Deutschland linafahamisha zaidi kwamba Kikosi hicho maalumu,ATPU ni cha kupambana na ugaidi, .Kikosi hicho kinafanya uhalifu mtindo mmoja bila ya kuadhibiwa. Gazeti hilo linaeleza kuwa, ripoti ya Umoja wa Mataifa imethibitisha uhalifu wa kikosi hicho.

Hivi karibuni kikosi hicho kilimteka nyara mtu mmoja mwenye itikadi kali ya kiislamu, kwa jina Mohammed Abdul-Malik na kumkabidhi kwa maafisa wa Marekani.Lakini kabla ya hapo mtu huyo alishikiliwa kwa muda wa wiki mbili akiteswa.Gazeti la "Neues Deutschland"linasema katika taarifa yake kwamba kikosi hicho cha Kenya kimepata mafunzo kwa muda wa miaka mitatu kutoka kwa idara kuu ya Ujerumani ya kupambana na uhalifu BKA.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman