1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya24 Januari 2014

Wiki hii,magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kuchaguliwa kwa Rais wa mpito katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, mgogoro wa Sudan Kusini na juu ya kujifunua ushungi kwa mwandishi maarufu wa Kenya Binyavanga Wainaina.

https://p.dw.com/p/1Awn5
Rais wa kipindi cha mpito katika Jamhuri ya Afrika ya Kati,Catherine Samba-Panza
Rais wa kipindi cha mpito katika Jamhuri ya Afrika ya Kati,Catherine Samba-PanzaPicha: Reuters

Gazeti la "die tageszeitung limeandika juu ya kuchaguliwa kwa Rais wa kipindi cha mpito katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Gazeti hilo linasema kwa mara ya kwanza katika eneo la Afrika ya Kati,mwanamke amechaguliwa kuiongoza nchi. Mwanamke huyo ni Catherine Samba-Panza.

Hata hivyo gazeti la "die tageszeitung" linasema Samba Panza atakabiliwa na mtihani mgumu atakapojaribu kuutandaza mtandao wa mamlaka yake nje ya mji mkuu, Bangui. Gazeti hilo linasema wakati watu katika mji mkuu wanafurahia kuchaguliwa kwa Rais huyo wa kipindi cha mpito, hali katika sehemu za nje ya mji wa Bangui, inatishia kuenda mrama.

Mrengo wa shoto wapinga Ujerumani kusaidia Jamhuri ya Afrika ya Kati

Gazeti la "Süddeutsche" pia limeandika juu ya Jamhuri ya Afrika Kati lakini kuhusiana na mjadala wa Bunge la Ujeurumani juu ya mgogoro wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Gazeti hilo linaeleza katika makala yake kwamba Chama cha mrengo wa shoto,die Linke,ndicho pekee nchini Ujerumani, kilichoupinga uamuzi wa Bunge juu ya kuwapeleka wanajeshi wa Ujerumani katika Jamhuri ya Kati ili kuyaunga mkono majeshi ya Ufaransa . Hilo siyo jambo la kushangaza, kwani ni sera ya msingi ya chama hicho kupinga vita na ushiriki wa majeshi ya Ujerumani katika maeneo ya migogoro.

Gazeti la "Süddeutsche " limemnkuu mjumbe wa chama hicho aliemo katika kamati ya bunge ya mambo nje Stefan Liebich ,akieleza kwamba, ikiwa mtu anatambua ni kwa kiwango gani Ufaransa imehusika katika kuangushwa kwa serikali kadhaa barani Afrika,basi ataelewa kwa nini chama cha mrengo wa shoto kinapinga majeshi ya Ujerumani kupelekwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Watia saini mkataba wa amani Sudan Kusini

Gazeti la "Berliner Zeitung" limechapisha makala juu ya mgogoro wa Sudan Kusini. Linasema katika makala hiyo: hatimaye pana matumaini katika Sudan Kusini. Pande zinazopigana zimekubaliana kuutia saini mkataba juu ya kuyasimamisha mapigano yaliyoanza mnamo mwezi wa Desemba mwaka uliopita. Watu karibu 10,000 wameuawa kutokana na mapigano hayo. Wengine nusu milioni wamegeuka wakimbizi.

Frankfurt yafungua tawi la masomo Kinshasa
Gazeti la "Die Zeit" limeandika juu ya mradi wenye lengo la kuleta usalama na maendeleo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Mradi huo umenzishwa na shule ya usimamizi wa biashara ya mjini Frankfurt.

Gazeti hilo linaarifu kwamba sasa ni miezi mitatu tokea chuo cha masomo ya biashara cha mjini Frankfurt kianze kutoa masomo ya uzamili kwenye tawi kilicholifungua katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kinshasa. Mkuu wa mradi, Udo Stefan amesema mradi huo wa masomo ni njia mojawapo ya kutoa msaada wa maendeleo barani Afrika.

Gazeti la"Die Zeit" limearifu katika taarifa yake kwamba hadi mwezi wa Oktoba mwaka uliopita, wanafunzi 39 walianza masomo kwenye tawi hilo la Kinshasha la chuo cha biashara cha Frankfurt

Wainaina ajivufunua shungi hadharani

,Mwandishi maarufu wa Kenya Binyavanga Wainaina hatimae ametijoa hadharani na kutamka wazi kwamba yeye ni shoga.Hizo ni habari zilizochapishwa na gazeti la "Süddeutsche Zeitung" Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba hatua hiyo ni ya ujasiri mkubwa kuliko ile ya mwanasoka wa Ujerumani Thomas Hitzlsperger ambae hivi karibuni pia alijitoa hadharani na kutamka kuwa yeye ni shoga.

Gazeti la Süddeustche linasema mwandishi wa Kenya Wainaina amesema hadharani kuwa yeye ni shoga katika jamii yenye sheria na utamaduni unaoguna inapohusu jambo la ushoga.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman