1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

21 Februari 2014

Kesi ya kihistoria ya mauwaji ya halaiki ya Rwanda mjini Frankfurt,Mchango wa Ujerumani katika juhudi za kulinda amani barani Afrika na Libya miaka mitatu baada ya gaddafi magazetini

https://p.dw.com/p/1BDER
Onesphore Rwabukombe akifikishwa mahakamani mjini FrankfurtPicha: imago/epd

Ilikuwa wiki ya matukio muhimu yaliyoripotiwa na wahariri wa magazeti na majarida ya Ujerumani kuhusu Bara la Afrika;kuanzia hukmu ya miaka 14 jela dhidi ya Onesphore Rwabukombe aliyepatikana na hatia ya kuchochea mauwaji ya watutsi zaidi ya 450 waliokimbilia kanisani wakati wa mauwaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994,kiu cha Umoja wa ulaya kutaka kuijua sera mpya ya nje ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani na jinsi wananchi wa Libya wanavyoitathmini miaka mitatu baada ya kutimuliwa na baadae kuuwawa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.Hayo na mengineyo ni miongoni mwa yale yaliyomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.

Tunaanzia Frankfurt ambako kesi ya kihistoria imemalizika na hukmu kutolewa miaka 20 baada ya mauwaji ya halaiki ya Rwanda."Miaka 14 jela kwa kuchochea mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994"ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Süddeutsche Zeitung kuhusu hukmu dhidi ya meya wa mji mdogo nchini Rwanda Onesphore Rwabukombe aliyekuwa akiishi mjini Frankfurt tangu mwaka 2002 baada ya kuomba hifadhi ya ukimbizi.Baada ya kuelezea yaliyotokea katika kanisa la kiziguro April 11 mwaka 1994 na kuzungumzia ushahidi uliotolewa,mhariri wa gazeti hilo la mjini Munich amenukuu mojawapo ya hoja za mahakimu zinazosema hata kama binafsi hajauwa lakini pekee kuwepo kwake mahala mauwaji hayo yalikofanyika kumewapa nguvu waliofanya mauaji hayo.Miaka mitatu imedumu kesi hiyo hadi hukmu kutangazwa-ikiwa kesi ya kwanza kuhusu mauwaji ya halaiki ya Rwanda kufanyika katika ardhi ya Ujerumani-malaki ya Euro yametumika pia kugharimia kesi hiyo.Mhariri wa Süddeutsche Zeitung anakumbusha kesi haijamalizika kwasababu mshatikiwa anapanga kukata rufaa na kudai hana hatia."

Kiu cha Umoja wa Ulaya

"Brussels inasubiri kuijua sera mpya ya nje ya Ujerumani" ndio kibwa cha maneno cha gazeti la "Die Welt" linalokumbusha mataifa mengi na hata Georgia ambayo si mwanachama wa umoja wa ulaya yameshaelezea utayarifu wao wa kuchangia mamia ya wanajeshi kwaajili ya kikosi cha kulinda amani barani Afrika.Umoja wa Ulaya unajiandaa kwa hima kubwa kutuma wanajeshi katika jamhuri ya Afrika kati inayokabwa na vurugu na matumizi ya nguvu.Mkakati jumla wa operesheni hiyo ya kulinda amani umefafanuliwa katika ripoti ya kurasa 400.Duru za Umoja wa ulaya zinalitaja jukumu hilo kuwa "gumu".Kundi la kwanza la wanajeshi hao linatarajiwa kuwasili mjini Bangui,mji mkuu wa jamahuri ya Afrika kati kati ya mapema na katikati ya mwezi ujao wa machi.Hadi wakati huu nchi nane za Umoja wa Ulaya zimeshatangaza zitachangia wanajeshi.Ujerumani haimo katika kundi hilo.Hata hivyo mhariri wa Die Welt anasema Umoja wa Ulaya unataraji matamshi yaliyotolewa na rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck na waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen kwamba Ujerumani inataka kuwajibika zaidi ulimwenguni yatafuatiwa na vitendo.."

Von der Leyen besucht Soldaten in Mali
Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Ursula von der Leyen akiwatembelea wanajeshi wa Ujerumani wanaowapatia mafunzo wanajeshi wa MaliPicha: Reuters

Walibya waonja Ladha ya Uhuru

Na hatimae gazeti la Neues Deutschland linalotahmini miaka mitatu baada ya kutimuliwa madarakani na baadae kuuliwa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi."Tulikuwa majuha lakini hatutokubali kushindwa" ndio kichwa cha maneno cha ripoti hiyo inayotoa picha ya furaha ya kuonja uhuru kwa muda wa miaka mitatu wananchi wa Libya ambayo wakati huo huo imeitumbukiza serikali ya waziri mkuu Ali Zeidan na wananchi kwa jumla katika janga la mitihani ya kila aina.Walibya wamepoteza imani kwa bunge la mpito lililochaguliwa msimu wa kiangazi mwaka 2012,shughuli za kusafirisha mafuta nchi za nje zimepungua kutokana na vizuwizi vilivyotawanywa kila mahala na wamechoshwa na hali ya ukosefu wa usalama.Cha kutia moyo ni kwamba wananchi wameshaonja ladha ya mfumo wa kidemokrasia tangu miaka mitatu iliyopita na wanateremka majiani kudai haki zao."Tulikuwa wapumbavu miaka mitatu iliyopita lakini isiwe sababu ya kukubali kushindwa hivi sasa."

Libyen Feierlichkeiten Revolution Jubiläum
Walibya washerehekea miaka mitatu ya mapinduziPicha: DW/E. Ezzobbair

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Pressem/All/PRESSE-STD

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman