1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa ya wakimbizi

26 Aprili 2015

Wiki hii magazeti ya Ujerumani karibu yote yameandika kwa mapana na marefu juu ya maafa yaliyowakumbuka wakimbizi kwenye bahari ya Mediterania. Pia yameandika juu ya misaada ya maendeleo kwa nchi za Afrika

https://p.dw.com/p/1FF0U
Idadi ya wakimbizi yaongezeka
Idadi ya wakimbizi yaongezeka

Gazeti la "Berliner Zeitung" limeripoti kwamba kila siku wakimbizi kati ya 300 na 700 wanapakiwa katika mashua za wahalifu wanaowasafirisha watu kinyume na sheria ili kuwapeleka Ulaya. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba aghalabu, baadhi ya wakimbizi hawafiki Ulaya. Safari yao huishia baharini.

Gazeti la "Berliner Zeitung" limemkariri Spika wa Bunge la Ulaya Martin Schulz akishauri wazo la kushirikiana na serikali ya Libya ili kuushughulikia mgogoro wa wakimbizi .

Idadi ya watu inaongezeka haraka barani Afrika

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limechapisha makala juu ya mgogoro wa wakimbizi kwa kutilia maani ongezeko la watu barani Afrika.Gazeti hilo linaeleza kwamba Kiwango cha ongezeko la idadi ya watu barani Afrika ni kikubwa na kilichotokea mwishoni mwa wiki iliyopita kinathibitisha mchakato wa watu kulihama bara hilo. Maafa yaliyotokea kwenye bahari ya Mediterania pia yanathibitisha jinsi mifumo ya kijamii katika nchi kadhaa barani Afrika ilivyosambaratika.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine"linasema hakuna sehemu nyingine duniani yenye ongezeko kubwa la idadi ya watu kuliko bara la Afrika.Na kutokana na shinikizo la idadi kubwa ya watu na migogoro mingine katika bara hilo,ni wazi kwamba vijana wanaamua kuzihama nchi zao haraka.

Na ndiyo sababu,gazeti linasema kwamba serikali za Afrika zinapaswa kuifuata njia ya maendeleo, ambayo,siyo tu kwamba italeta ustawi wa uchumi bali pia ile itakayowawezesha vijana wake kuondokana na hali mbaya.

Vijana wengi wanaamua kuzihama nchi zao
Hata hivyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani kwamba ,hata ikiwa nchi za Afrika zitafanikiwa kujenga miundo bora ya kisiasa na kiuchumi bado watakuwapo vijana wa kiafrika watakaoamua kuenda kule kunakopatikana neema kwa haraka, yaani barani Ulaya.

Gazeti la "Neues Deutschland"limechapisha taarifa juu ya wakimbizi kutoka Afrika ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika mji mdogo unaoitwa Strasburg mashariki mwa Ujerumani. Lakini mji huo unazingatiwa kuwa ngome ya chama cha siasa za mrengo mkali wa kulia. Wafuasi wa chama hicho,NPD wanawachukia wahamiaji.

Gazeti hilo linaarifu kwamba miongoni mwa wakimbizi hao ni David Simon kutoka Eritrea. David ameliambia gazeti hilo kwamba baadhi ya wenyeji wa mji wa Strasburg ni wema na wengine ni wabaya.

Wakimbizi wanaishi kwa mashaka barani Ulaya
Gazeti la "Neues Deutschland" limearifu kwamba wakimbizi wa kwanza waliwasili katika mji wa Strasburg mashariki mwa Ujerumani mnamo mwezi wa Novemba mwaka uliopita. Wakimbizi hao walikaribishwa rasmi na wajumbe wa baraza la mji. Lakini gazeti linatufahamisha kwamba mwishoni mwa mwezi huo wa Novemba,nyumba ya wakimbizi hao ilishambuliwa kwa fataki.

Jee mabilioni yanayotolewa yanasaidia?

Katika makala yake nyingine wiki hii gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linauliza iwapo mabilioni ya fedha yanayotolewa ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kweli yanasaidia? Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu kwamba benki ya maendeleo ya Ujerumani KfW inatoa fedha nyingi kwa nchi zinazoendelea ikiwa pamoja na zile za Afrika. Gazeti hilo limeuliza iwapo maalfu ya wakimbizi wanaokimbilia Ulaya wananufaika na fedha hizo hata kidogo?

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema miradi ya maendeleo,34 ilitekelezwa kutokana na kutengewa Euro Milioni 500 za ziada. Lakini gazeti hilo lilifanya mahojiano na mtafiti maarufu wa masuala ya maendeleo William Easterly kutoka Marekani, aliesema kwamba tokea miaka ya 60 nchi zinazoendelea zimepokea dola Bilioni 600 za msaada wa maendeleo lakini hazikuyabadilisha maisha ya watu wengi.

Gazeti hilo limefahamisha kwamba katika miaka iliyofuatia hadi 2013 Afrika ilipokea jumla ya dola Bilioni 300 za msaada lakini pia fedha hizo hazikuleta mabadiliko.


Mtafiti wa maendeleo Easterly amekaririwa na gazeti la "Frankfurter Allgemeine " akisema kwamba bara la Afrika linahitaji mapinduzi kama yale yaliyoletwa baada ya wataalamu kuufafanua kwa usahihi mfumo wa sayari.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu