1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi mashakani

21 Desemba 2015

Wiki hii, magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya matukio ya nchini Burundi, kutikisika kwa nguzo za utawala wa Jacob Zuma na pia yameandika juu ya uhaba wa madaktari barani Afrika.

https://p.dw.com/p/1HQvy
Ghasia zatanda Burundi
Ghasia zatanda BurundiPicha: picture-alliance/AP Photo

Gazeti la "die tageszeitung" linadai kwamba wanajeshi wa Burundi wanafanya ukatili katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura.Na limewanukulu wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanaotahadharisha juu ya kutokea mgogoro mwingine baina ya Wahutu na Watutsi nchini Burundi.

Gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha katika makala yake kwamba tangu kushindikana kwa jaribio la kuiangusha serikali nchini Burundi mnamo mwezi wa Mei,watu wengi wameshauawa na vitendo vya ukatili dhidi ya wapinzani wa serikali vimeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Gazeti la "die tageszeitung" limezikariri taarifa rasmi za serikali zikiwaita watu wanaouawa kuwa ni maadui. Gazeti hilo limetoa mfano wa watu waliouawa hivi karibuni,ambao kwa mujibu wa taarifa ya serikali , walijaribu kuivamia kambi ya wanajeshi. Gazeti la "die tageszeitung" limeikariri taarifa rasmi ya serikali ikisema kuwa watu hao walitaka kupora silaha kwenye kambi hiyo.

Gazeti hilo linasema vyombo habari vinatoa taarifa zinazotafautiana na zile za serikali. Mtandao wa" SOS Medias" Burundi umeripoti juu ya mkasa wa mkaazi mmoja wa kitongoji cha Nyakabiga.Mtu huyo aliuambia mtandao wa SOS Medias Burundi" kuwa askari waliwavamia usiku. Amesema askari hao waliwaambia watu wafungue milango yao na walipokataa wanajeshi walirusha magurunedi ndani ya nyumba zao .

Jaocb Zuma ayumba

Gazeti la "Die Welt" wiki hii linayazingatia matukio ya nchini Afrika Kusini. Na linasema katika kichwa cha habari ,"nguzo za utawala wa Rais Jacob Zuma zinayumba. Linaeleza kwamba mnamo muda mfupi wa siku nne tu, watu nchini Afrika Kusini walishuhudia uteuzi wa mawaziri wa fedha watatu.

Rais Jacob Zuma matatani
Rais Jacob Zuma matataniPicha: picture-alliance/landov

Hali hiyo ilisababisha malalamiko siyo tu kutoka kwa wapinzani wa jadi, yaani vyama vya kisiasa , kama Democratic Alliance, bali pia kutokea ndani ya chama cha Zuma, ANC.


Gazeti la "Die Welt" linaeleza kuwa kukuru kakara zilianza baada ya Rais Jacob Zuma kumwachisha kazi waziri wa fedha mahiri Nhlanhla Nene bila ya kutoa sababu yoyote. Lakini gazeti la "Die Welt" limebainisha kwamba waziri huyo alikataa kutoa ridhaa ya ujenzi wa vinu vya nyukilia vinane kwa bei ya dola Bilioni 100 chini ya mkataba wa kizani na Urusi.

Gazeti la "Die Welt" linasema utawala wa Zuma uliyumba kutokana na malalamiko yaliyotokea ndani ya chama chake cha ANC, kutoka kwa chama ndugu cha kikomunisti na pia kutoka kwa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Cosatu.

Uhaba wa madaktari waathiri huduma za afya barani Afrika

Gazeti la "Neues Deutschland" linazungumzia juu ya uhaba mkubwa wa madaktari katika nchi za Afrika.Gazeti hilo linaarifu kwamba katika nchi 47 za kusini mwa jangwa la Sahara, vipo vyuo 170 tu vya kuwafundishia madaktari.

Gazeti la "Neues Deutschland" linafahamisha kuwa huduma za afya katika nchi nyingi za Afrika zimo katika hali mbaya. Hadi utakapofika mwaka wa 2035, patakuwa na pengo la wahudumu wa afya, Milioni 4 ,3 .Mafunzo ni duni na pia hakuna fedha .

Gazeti la "Neues Deutschland" linaeleza kuwa hali hiyo mbaya katika sekta ya afya siyo jambo jipya. Limeinukulu ripoti ya shirika la afya duniani WHO, inayothibitisha kwamba, tayari mnamo mwaka wa 2013, palikuwapo na uhaba wa wahudumu wa afya Milioni 1,8 katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Gazeti hilo linasema hali hiyo inatokana na ukosefu wa fedha na miundo mbinu inayohitajika.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu