1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatari ya njaa nchini Ethiopia

6 Mei 2016

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yanauliza kwa nini eneo la Sahel ni muhimu kwa Ulaya? Na pia yameandika juu ya kuchomwa moto kwa vipusa nchini Kenya

https://p.dw.com/p/1IjK5
Picha: Reuters/T. Mukoya

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeandika juu ya ziara ya mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank -Walter Steinmeier na wa Ufaransa Jean -Marc Ayrault katika nchi za Sahel. Gazeti hilo linauliza kwa nini eneo hilo la kaskazini/ magharibi mwa Afrika ni muhimu kwa Ulaya.?

Linaeleza kwamba mawaziri hao walifanya ziara kwa pamoja nchini Mali na Niger ili kuonyesha kwamba nchi zao zitaendelea kutoa mchango katika juhudi za kuudumisha utulivu katika sehemu hiyo isiyokuwa na usalama wa uhakika.

Mashambulio ya magaidi yasababisha vifo nchini Mali

Gazeti hilo limekumbusha juu ya mashambulio yaliyofanywa na magaidi nchini Mali na kuwaua watu 22. Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaeleza kwamba Ujerumani na Ufaransa zinaizingatia, Mali kuwa muhimu katika harakati za kudumisha utulivu katika eneo la Sahel, na Niger inazingatiwa kuwa muhimu katika juhudi za kuutatua mgogoro wa wakimbizi.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeinukuu taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ikisema kuwa Niger imegeuka kituo kipya cha wakimbizi wanaopanga kuelekea barani Ulaya.

Askari alinda usalama baada mashambulio ya kigaidi nchini Mali
Askari alinda usalama baada mashambulio ya kigaidi nchini MaliPicha: Getty Images/AFP/S. Rieussec

Vipusa vyachomwa moto
Serikali ya Kenya ilichoma moto tani 105 za pembe za ndovu na tani 1.5 za pembe za faru. Jee hatua hiyo itasaidia katika juhudi za kupambana na majangili?

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaeleza kwamba hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya ina lengo la kuipiga vita biashara haramu ya vipusa na pia kuihamasisha dunia juu ya umuhimu wa kuwalinda wanyama pori.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Rais Uhuru Kenyatta akisema kwake itakuwa furaha kubwa ikiwa tani zaidi ya mia moja za pembe za ndovu zitapigwa moto ili kuwakomesha majangili na watu wanaoshirikiana nao.

Rais Kenyatta amekaririwa akisema kwama ikiwa hatua hazitachukuliwa kuwalinda wanyama pori,watoto wa leo, watakuwa Waafrika wa kwanza, katika kipindi cha miaka 10,000 iliyopita, watakaokua bila ya kuwaona ndovu na faru barani Afrika!

Hata hivyo gazeti linasema wachambuzi wana mashaka iwapo hatua ya kuvichoma moto vipusa itaathiri soko. Lakini mtaalamu na mlinzi wa wanyama pori, Richard Leakey amenukuliwa akisema kuwa watu katika nchi za Asia,kwenye soko kubwa kabisa la vipusa, wanafikiri pembe wanazonunua zinatoka kwa wanyama pori waliokufa kwa njia za kawaida.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Richard Leakey akieleza kuwa macho ya watu katika nchi za Asia yatafunguka baada ya serikali ya Kenya kuzichoma moto pembe za faru na tembo thamani ya dola Milioni mia moja.

Hatari ya njaa nchini Ethiopia

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii pia limechapisha makala juu ya hali mbaya ya ukame nchini Ethiopia. Na kwa ajili hiyo limefanya mahojiano na Mwenyekiti wa shirika la misaada la Ujerumani "Welthungerhilfe" Till Wahnbaeck.

Bwana Till Wahnbaeck ameliambia gazeti hilo kwamba watu nchini Ethiopia hawana tena akiba ya chakula kutokana na ukame. Mwenyekiti huyo amesema Ethiopia imekumbwa na ukame mbaya zaidi kuliko ule wa miaka ya 1980 uliosababisha vifo vya watu karibu Milioni moja.

Bwana Wahnbaeck ameliarifu gazeti la "Frankfurter Allgemeine" kwamba watu zaidi ya Milioni 10 wamo katika hatari ya kukumbwa na njaa nchini Ethiopia na mamia tayari wameshakufa kutokana na utapiamlo.

Mwenyekiti wa shirika la misaada la Ujerumani ametahadharisha katika mahojiano na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" kuwa hali mbaya inayowakabili mamilioni ya watu nchini Ethiopia inasahauliwa na jumuiya ya kimataifa hasa kutokana na mgogoro wa wakimbizi katika nchi za Ulaya.

Bwana Wahnbaeck amesema dunia imesahau kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hakuna tone la mvua hata moja lililodondoka nchini Ethiopia, na hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabia nchi iliyosababishwa na nchi za viwanda.Mwenyekiti huyo wa shirika la misaada la Ujerumani ametahadharisha kwamba Ethiopia peke yake haitaweza kukabiliana na mgogoro huo mkubwa.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu