1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kishindo cha Brexit chapiga Afrika

1 Julai 2016

Ripoti ya mwaka ya shirika la UNICEF kuhusu ufukara barani Afrika,madhara ya kura ya Brexit kwa Afrika na jinsi digitali unavyozipatia matumaini mema Afrika miongoni mwa mada magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/1JHKu
Jinsi ukame unavyoathiri maisha nchini MsumbijiPicha: DW/L.de Conção

Tuanzie na ripoti ya mwaka ya shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto UNICEF. Gazeti la Frankfurtzer Allgemeine linasema hata miongoni mwa matajiri kuna wengi walio masikini. Licha ya maendeleo yote yaliyopatikana,gazeti hilo mashuhuri la Ujerumani linainukuu ripoti hiyo ya UNICEF ikisema,bado watoto wengi wanakufa kwa sababu zinazoweza kuepukika. Kwa mujibu wa shirika la UNICEF hadi ifikapo mwaka 2030 watoto na vijana wasiopungua milioni 167 wenye umri wa chini ya miaka 17 watakuwa wakiishi katika hali ya umaskini uliokithiri. Watoto tisa kati ya kumi,watakaoatilika zaidi ,kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka ya UNICEF,watakuwa wale wanaoishi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara. Wakaazi wa eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara wanasumbuliwa zaidi na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwakuwa wengi wao wanategemea shughuli za kilimo. Madhara ya mabadiliko ya tabia nchi mfano wa El Nino yaliyopiga mwaka 2015/2016,yanatajwa kuwa mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu miaka 65 iliyopita na kusababisha hali mbaya kabisa ya hewa;katika baadhi ya nchi El Nino imesababisha ukame na kuteketeza mavuno pamoja na kusababisha njaa. Makadirio ya miaka inayokuja nayo pia si ya kuridhisha linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Ripoti ya UNICEF imezungumzia pia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa. Frankfurter Allgemeine limezungumzia pia malengo ya maendeleo ya Umoja wa mataifa yaliyotajwa katika ripoti ya UNICEF inayohisi hakuna ishara kama malengo hayo yatafikiwa.

Kishindo cha Brexit chaitikisa pia Afrika

Madhara ya kura ya Brexit ya Uingereza kwa bara la Afrika yamechambuliwa na gazeti la "Neues Deutschland" linasema,biashara,vitega uchumi,misaada ya maendeleo,yote hayo wataalam katika nchi za Afrika wanahofia yatahatarika kufuatia kura ya Brexit ya Uingereza. Afrika kusini inajionyesha kuwa karimu linaandika gazeti la Neues Deutschland linalomnukuu waziri wa biashara na viwanda Rob Davies akiiambia Uingereza makampuni yake yanaweza kuja Afrika Kusini na kuendesha shughuli zao ikiwa haitofikia makubaliano pamoja na Umoja wa Ulaya kuingiza bidhaa zake katika nchi za Umoja huo. Kutokana na ushirikiano mpya kati ya Umoja wa ulaya na jumuia ya SADC,Afrika Kusini inaruhusiwa kutuma bidhaa zake katika soko la Umoja wa Ulaya. Neues Deutschland linanukuu gazeti la Daily Maverick la Afrika kusini likidhihaki kwa kusema "ni kichekesho kwamba Afrika Kusini ina uwezo mkubwa zaidi wa kuingia katika masoko ya Umoja wa Ulaya kuliko Uingereza. Brexit imegeuka kuwa ukweli wa mambo na bara la Afrika linabidi lijiambatanishe. Mengi yatategemea jinsi masoko ya hisa yatakavyoweza kurejea katika hali ya utulivu- amesema mkuu wa tawi la Afrika katika benki ya Standard Chartered Bank,Razia Khan. Itakayoathirika zaidi ni Afrika kusini ambayo masoko yake ya hisa yanashirikiana kwa dhati na Uingereza na kila kishindo kinachopiga London kinapiga pia Raas ya Matumaini mema linamaliza kuandika gazeti la Neues Deutschland.

Mfumo wa Digitali wainua Maendeleo Afrika

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu mawasiliano ya Apps kwa lengo la kujitoa katika hali ya umaskini. Der Tagesspiegel linasema mfumo wa digitali unazipatia fursa nchi zinazoinukia kushiriki katika mfumo mpya wa mawasiliano.Thuluthi mbili ya wakaazi wa Afrika wanatumia mfumo mpya wa mawasiliano. Gazeti la Der Tagesspiegel linazungumzia maendeleo yaliyopatikana kupitia mtandao na kuutaja utaratibu wa M-Pesa. Nchini Kenya wenye akonti za benki ni asili mia 30 tu katika wakati ambapo asili mia 70 wanatumia utaratibu wa kutuma pesa kwa njia ya digitali-M-Pesa.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Mohammed Khelef