1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC yapata kipigo nchini Afrika Kusini

5 Agosti 2016

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliokitia kwikwi chama cha ANC nchini Afrika Kusini .Pia yameandika juu ya kuvunjika moyo kwa walinzi wa wanyamapori barani Afrika.

https://p.dw.com/p/1Jc6F
Maandamano dhidi ya Rais Jacob Zuma,Cape Town
Maandamano dhidi ya Rais Jacob Zuma,Cape TownPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Süddeutsche" linatilia maanani kwamba chama tawala ANC kimepoteza udhibiti wa ngome zake, zilizokuwa imara kwa miaka zaidi ya 20.

Juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Afrika Kusini gazeti la "Süddeutsche" linauliza iwapo uamuzi wa wapiga kura kukiadhibu chama hicho ulikuwa hasira za mkizi au chama hicho kimevuna kilichopanda.

Gazeti hilo linaeleza kwaba kwa mara ya kwanza tangu utawala wa kibaguzi ung'olewe nchini Afrika Kusini, chama tawala,ANC kimepoteza sehemu ya mamlaka yamemeguka katika miji muhimu. Wapiga kura katika sehemu za mijini wamevipigia kura nyingi vyama vya upinzani vya Democratic Alliance na EFF .

Gazeti la "Süddeutsche" limemnukulu mwanafunzi mmoja, Nompilo Nkosi akisema kuwa chama cha ANC kinakabiliwa na tatizo la ufisadi.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limesema watu wengi nchini Afrika Kusini wamevunjwa moyo na uongozi wa chama cha ANC kutokana na kashfa za rushwa na hasa ubadhirifu wa Rais Jacob Zuma. Hata hivyo gazeti la "Der Tagesspiegel" linatilia maanani kwamba chama cha ANC bado kinaungwa mkono kwa kiwango kikubwa katika sehemu za mashambani na kwamba chama hicho kina uhakika wa kuendelea kuwepo.

Ukame waikumba kusini mwa Afrika

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatahadharisha juu ya hali mbaya ya ukame katika nchi za kusini mwa Afrika.

Mifugo yateketea kutokana na ukame
Mifugo yateketea kutokana na ukamePicha: picture-alliances/dpa//K. Ludbrock

Gazeti hilo linaeleza kwamba eneo la kusini mwa Afrika limekumbwa na ukame ambao haujawahi kuonekana katika karne iliyopita.Ukame huo umesababishwa na hali ya hewa ya El Nino, na umeleta maafa makubwa. Kwa mujibu wa hesabu za shirika la chakula la Umoja wa Mataifa,WFP, watu Milioni 12,3 watahitaji msaada wa chakula na dola Bilioni 1.2 zitahitajika kwa ajili hiyo.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linafahamisha kwamba hali ya hewa ya El Nino imeteketeza siyo mimea tu bali pia mifugo.Ng'ombe zaidi ya Mia sita alfu wameangamia nchini Afrika Kusini,Botswana,Lesotho,Namibia,Swaziland na Zimbabwe.Gazeti hilo linasema hali inatatiza zaidi kwa sababu kila serikali inautekeleza mkakati wake, badala ya nchi hizo kuratibisha juhudi za pamoja.

Tembo kuendelea kuuliwa

Gazeti la "die tageszeitung" linafahamisha kwamba kila baada ya dakika 15 anakufa tembo mmoja kutokana na ujangili.Gazeti hilo linasema wanyama hao wanauliwa kwa sababu ya meno yao. Ndiyo sababu, kabla ya mkutano wa kimataifa, utakaofanyika mjini Washington kujadili ulinzi wa wanyamapori, nchi za Afrika zimetoa mwito wa kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu.


Lakini gazeti la "die tageszeitung" linasema walinzi wa wanyama pori barani Afrika wamevunjwa moyo baada ya kusikia kwamba Umoja wa Ulaya hautapiga marufuku biashara ya pembe za ndovu. Gazeti la "tageszeitung" limeinukulu Halmashauri ya Umoja huo ikisema mwito wa nchi za Afrika wa kutaka biashara hiyo ipigwe marufuku unaonekana kutokuwa sahihi.

Gazeti hilo linakumbushia tamko la Rais wa baraza la umoja wa nchi 29, la ulinzi wa ndovu,Azizou El Hadj Issa la kuutaka Umoja wa Ulaya uziunge mkono nchi za Afrika kwa kuipiga marufuku biashara haramu ya vipusa.

Hata hivyo gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha kwamba tangu mwaka wa 1989 biashara hiyo imepigwa marufuku. Lakini tangu mwaka 1999 , vipengele vingi vimeingizwa katika mkataba vinavyoruhusu biashara ya vipusa kuendelea.Gazeti hilo linasema maalfu ya ndovu wameuliwa kwa sababu ya vipengele hivyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu