1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya ujerumani

Oummilkheir20 Oktoba 2006

Yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

https://p.dw.com/p/CHUe

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia,hali katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,wiki chini ya moja kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais , kinyang’anyiro cha kuania madaraka nchini Côte d’Ivoire na njaa nchini Burundi na Eritrea ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii kuhusu bara la Afrika..

Tuanzie na mzozo wa Somalia.”Vita vya jihad” ndio kichwa cha maneno cha jarida la Der Spiegel,linasema vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vimeenea mpaka katika nchi jirani.Jarida la Der Spiegel linazungumzia uamuzi wa serikali ya mjini Nairobi wa kutuma mamia ya wanajeshi kujaribu kuulinda mpaka wenye urefu wa kilomita 700 ili kuzuwia wakimbizi wasizidi kumiminika.Lakini hali ya kusikitisha imezuka sasa katika katika eneo hilo la nusu jangwa linalozigawa nchi hizo mbili.”

Baraza la mahakama ya kislam linaituhumu Ethiopia kuingilia kati katika mapigano ya kuania mji wa kusini wa Burhakaba. Jarida la Der Spiegel linahisi waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi anapalilia mambo aliposema:”Tukihisi wafuasi wa itikadi kali wanatishia usalama wetu,bila ya shaka tunahaki ya kujihami kwa kila hali.”Matamshi hayo ndiyo yaliyomfanya Sheikh Shariff Ahmad,mmojawapo wa viongozi wa baraza la mahakama ya kislam kutangaza vita vya jihadi dhidi ya Ethiopia.Jarida la Der Spiegel linamaliza kwa kutahadharisha “mapigano yakitapakaa,basi yatawaathiri pia jamii ya wachache ya wasomali wa Ogaden,kusini mashariki ya Ethiopia.”

Gazeti la NEUES DEUTSCHLAND linazungumzia hali namna ilivyo katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na mtihani wanaokabiliana nao wanajeshi wa kusimamia amani kutoka nchi za umoja wa ulaya.”Umoja wa Ulaya unabidi usimame kidete“ ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linaloelezea jinsi ofisi ya ubalozi wa Umoja wa ulaya ilivohujumiwa mjini Kinshasa na wanajeshi wanaomlinda rais Kabila wakati balozi mwenyewe akilazimika kwenda kujificha katika makao makuu ya mpinzani wake Jean Pierre Bemba hadi wanajeshi wa Umoja wa ulaya walipokua kumuokoa.

Imekuja bainika lakini kua mambo ni akhasi zaidi,linaandika Neues Deutschland linalonukuu ripoti ya shirika la kimataifa la kuepusha mivutano-International Crisis Group-ICG linalosema machafuko ya Agosti iliyopita mjini Kinshasa yamechochewa pia na polisi wa Kongo waliopatiwa mafunzo na Umoja wa ulaya na kupatiwa vifaa kwa msaada wa fuko la maendeleo la Umoja wa ulaya.

Baada ya kuelezea kwanini wanajeshi wa umoja wa ulaya wamepelekwa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,gazeti la Neues Deutschland linazungumzia kitisho cha kuzuka tena machafuko duru ya pili ya uchaguzi wa rais itakapoitishwa.Gazeti linakosoa pendekezo la shirika la kimataifa la kuzuwia mivutano ICG :Neues Deutschland linasema jambo kama hilo halitakawia kuzusha hisia mbaya ,pale wananchi watakapokumbuka enzi za kale za ukoloni.”LInamalizia gazeti la Neues Deutschland.

Gazeti la TAGESZEITUNG limechapisha mahojiano pamoja na mshauri mkuu wa rais She Okitundu aliyeshambuliwa hivi karibuni mjini London.Tageszeitung linalinganisha kisa hicho na mashambulio ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya.

Gazeti hilo hilo la Tageszeitung limeandika pia kuhusu kinyang’anyiro cha kuania madaraka nchini Côte d’Ivoire,baada ya Umoja wa Afrika kurefusha kwa mwaka mmoja wadhifa wa rais Laurent Gbagbo lakini wakati huo huo waziri mkuu Charles Konan Banny amepewa madaraka makubwa zaidi .

Lakini kama uamuzi huu wa sasa utatekelezwa linajiuliza gazeti la Tageszeitung linalokumbusha uamuzi kama huo ulipitishwa mwaka jana na baraza la usalama la umoja wa mataifa lakini haukuheshimiwa.

Die Tageszeitung linaashiria mvutano :linasema upande wa upinzani na waasi wanaoshikilia sehemu ya kaskazini ya Côte d’Ivoire hawataki kumuona Gbagbo akisalia hata siku moja zaidi,seuze mwaka mmoja na wameshaonya kuitisha mgomo mkubwa oktober 31 ijayo,siku ya uchaguzi ulioakhirishwa na baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika hadi siku kama hiyo mwakani.