1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
1 Juni 2018

Pamoja na masuala mengine magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya juhudi za kuutatua mgogoro wa nchini Libya na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/2yoM3
Feierlichkeiten zum 1. Todestag von Mandela 05.12.2014 Pretoria
Picha: Reuters/S. Sibeko

die tageszeitung

Makala ya gazeti la die tageszeitung yanaelezea juu ya mkutano uliofanyika mjini Paris mapema wiki hii kwa lengo la kutafuta  suluhisho la mgogoro wa nchini Libya.  Mkutano huo wa kimataifa wa mjini Paris uliwaleta pamoja viongozi wa Libya wanaopingana, kamanda wa jeshi la sehemu ya mashariki mwa nchi hiyo Khalifa Hafter, spika wa Bunge Agila Saleh, waziri mkuu Fayez Mustafa al-Sarraj wa serikali inayotambuliwa kimataifa pamoja na mwenyekiti wa baraza la rais. Viongozi hao waliujadili mpango wa katiba mpya na uchaguzi mpya  uliopangwa kufanyika mnamo mwezi wa Desemba. Gazeti hilo la die tageszeitung linasema kutokana na magogoro wa kisiasa, mfumo wa uchumi nchini Libya umo hatarini kusambaratika .Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba mgogoro huo unatoa mwanya kwa wahalifu wanaosafirisha watu kinyume cha sheria na pia unatoa mwanya wa kuimarika kwa makundi ya kigaidi.

Der Tagespeigel

Nalo gazeti la Der Tagespeigel wiki hii linaturudisha kwenye wasifu wa Nelson Mandela wakati akielekea kutimiza miaka 100 tangu kuzaliwa pindi angekuwa hai. Katika kuadhimisha mwaka ambapo Mandela angelitimiza umri wa miaka mia moja endapo  angelikuwa hai, Gazeti hilo limechapisha muhtasari wa nyasifu mbili juu ya Mandela.

Marehemu rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela (12.2013 DW Liveübertragung Trauerfeier Nelson Mandela Portrait)
Marehemu rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela

Waandishi wa nyasifu hizo wanauliza maswali kadhaa kwa mfano vipi iliwezekana kwa Mandela kutumikia kifungo jela kwa muda wa miaka 27 na vipi aliendelea kuwa na nguvu baada ya kutoka jela wakati alikuwa ameshavuka umri wa miaka 70? Na vipi aliweza kuhimili misukosuko ya jela bila ya kusambaratika kiakili na kimwili ? Katika nyasifu zao juu ya Madiba waandishi ambao wote ni Wajerumani wameshangazwa na moyo wa Mandela wa kuwa tayari kufikia maridhiano badala ya kulipiza kisasi. Hata wakati wa matatizo  makubwa katika maisha yake Madiba alikuwa na uhakika wa kufanikiwa katika harakati zake. Mandela aliyetoka kifungoni mnamo mwaka 1990 alionyesha uadilifu, ubinadamu, moyo wa upendo na ucheshi wa moyoni.

Die Zeit

Mjadala wa muda mrefu juu ya turathi za sanaa zilizotekwa wakati wa ukoloni umerejea tena. Hiyo ni makala iliyochapishwa na gazeti la Die Zeit Lakini gazeti hilo linasema  utaratibu wa kuzirudisha turathi hizo ni mgumu kuliko watu walivyotarajia hapo awali na linaeleza zaidi kwamba Endapo malalamiko ya miaka mingi ya wanaharakati yangelisikilizwa, kazi za sanaa zilizoporwa na wakoloni zingelikuwa njiani kurudishwa kwa wamiliki wa haki. Na mtu angeliweza kusema kwamba hatimaye bara la Ulaya limetambua kuwa nyumba zao za makumbusho zinaonyesha vitu venye dosari ya damu. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameashiria kuwa tayari kuzirudisha kazi hizo za Sanaa kwenye makoloni yake ya zamani.

Hata hivyo Die Zeit  linasema mambo hayaendi kiurahisi kama watu walivyofikiria. gazeti hilo linaeleza kuwa yapo maswali kadhaa yanayopaswa kujibiwa kwa mfano,ni lini urithi huo wa kisanaa uliporwa, na nani aliupora urithi huo, ni askari wa kikoloni au wamishenari waliozichukua turathi hizo baada ya kupatana na wamiliki? Ni vigumu kuwa na uhakika juu ya kila kazi ya sanaa iliyoletwa barani Ulaya kutoka kwenye makoloni. Mfano ni turathi maarufu za shaba kutoka Mali wakati ilipokuwa nchi ya kifalme. Inadaiwa kuwa turathi hizo ziliuzwa kibiashara kwa wazungu.Gazeti la Die Zeit linasema nia njema peke yake haitasaidia katika kuwezesha kurudishwa kwa turathi hizo. Mambo ya kisheria ambayo ni magumu yanapaswa kuzingatiwa.

Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila
Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

die tageszeitung

Makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung juu ya utatanishi unaohusu daftari la wapiga kura katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba wapinzani wanalalamika kuwa udanganyifu umefanyika na linaeleza kuwa uchaguzi wa rais unapaswa kufanyika mnamo mwezi wa Desemba katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini tayari hata wachambuzi wa kimataifa wameyathibitisha wanayoyasema wapinzani kwamba daftari la wapiga kura lina dosari. Kwa mujibu wa wapinzani hao daftari hilo lina majina hewa ya wapiga kura wapatao milioni 10. Die tageszeitung limewanukulu wapinzani wakisema kuwa wanataka majina hayo hewa yaondolewe na tume ya uchaguzi ibadilishwe. 

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman