1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani,Gbagbo kuachiwa ?

Abdu Said Mtullya18 Juni 2012

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yamechapisha taarifa juu ya uvumi kwamba aliekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo karibu ataachiwa.

https://p.dw.com/p/15Gup
Aliekuwa Rais wa Ivory Coast,Laurent Gbagbo
Aliekuwa Rais Ivory Coast,Laurent GbagboPicha: picture-alliance/dpa

Magazeti hayo pia yameandika juu ya mtuhumiwa wa ugaidi,raia wa Ujerumani aliekamatwa nchini Tanzania.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeandika juu ya uvumi unaomhusu aliekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo ambae sasa amewekwa mahabusi kwenye mahakama ya kimataifa ya mjini ya mjini The Hague,ICC.

Gazeti hilo limelikariri jarida moja la Ufaransa"La Lattre du Continent" likiarifu kuwa Gbagbo anatarajiwa kuachiwa karibuni na kuruhusiwa kuenda Uganda. Jarida hilo la Ufaransa limezinukuu taarifa za kidiplomasia na za mashirika ya ujasusi zikisema kuwa, Gbagbo ataachiwa kwa dhamana.

Katika makala yake gaezeti la "Frankfurter Allgemeine"limetilia maanani kwamba hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu, ICC kumwachia mtu anaetuhumiwa kuwa mhalifu wa kivita.Laurent Gbagbo alikamatwa na kupelekwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC baada ya serikali yake kuangushwa mwezi wa Aprili mwaka jana.

Rais huyo wa zamani aliondolewa madarakani kwa nguvu, baada ya waasi waliokuwa wanamuunga mkono Rais wa sasa Alassane Ouattara kusaidiwa na wanajeshi wa Ufaransa kumwondoa mwanasiasa huyo na kumpeleka kwenye mahakama ya mjini the Hague ambako alitakiwa kujibu tuhuma za kutenda uhalifu wa kivita. Majeshi ya Ufaransa yalipewa ridhaa na Umoja wa Mataifa. Laurent Gbagbo alishindwa katika uchaguzi wa Rais mwaka jana, lakini alikataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi.

Gazeti la"Süddeutsche Zeitung" limechapisha taarifa juu ya raia wa Ujerumani aliekamatwa nchini Tanzania kutokana na kutuhumiwa kuwa gaidi. Gazeti hilo limearifu kuwa mtu anaetuhumiwa kuwa gaidi amekamatwa nchini Tanzania, ambae pia anatafutwa na idara za usalama za Ujerumani.Kwa mujibu wa taarifa,mtu huyo ni Emrah Ergodan,Mjerumani mwenye asili ya kituruki anaetuhumiwa kuhusika na shambulio la bomu kwenye sehemu ya maduka mjini Nairobi lililofanyika tarehe 29 mwezi Mei.

Bara la Afrika linastawi kiuchumi mtindo mmoja .Hizo ni habari zilizochapishwa na gazeti la "NZZ am Sonntag" mnamo wiki hii. Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba Bara la Afrika linastawi siyo kutokana na sekta ya malighafi tu bali pia kutokana na sekta nyingine,kama vile,ujenzi,mawasiliano,kilimo na ya sekta ya mabenki.Gazeti la "NZZ am Sonntag" limeunukuu mtaala unaonyesha kuwa ustawi wa uchumi unafikia hadi asilimia 9 na hali itaendelea kuwa hivyo kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa mtaala huo pato la wastani litaongezeka kwa asilimia 50 mnamo kipindi cha miaka 12 ijayo katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Gazeti la "NZZ am Sonntag" limetilia maanani kwamba hakuna sehemu nyingine yoyote duniani inayostawi kwa kiwango kama hicho. Gazeti hilo limemnukuu mshauri wa mikakati ya biashara na uchumi ,Christian Wessels wa Ujerumani akisema kuwa jambo muhimu sana kwa nchi za Afrika ni kwamba,kwa kiasi kikubwa zimeanza kufanikiwa kuiondoa miundo ya kiuchumi na kibiashara iliyowekwa na wakoloni.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" limechapisha makala juu ya ubunifu wa vijana wa kiafrika na hasa nchini Kenya. Lakini gazeti hilo linasema ,licha ya ubunifu huo waafrika hawafiki mbali kutokana na ukosefu wa mitaji na njia za kulinda ubunifu wao. Gazeti hilo limetoa mfano wa vijana wawili wa Kenya waliovumbua kifaa cha kutia nguvu katika simu,kwa kutumia baiskeli mnamo mwaka wa 2009.

Mwaka mmoja baadae,kampuni ya simu Nokia nayo ilivumbua kifaa kama hicho hicho na kukipeleka sokoni.Gazeti la hilo limesema Wakenya walilalamika kuwa waliibiwa ubunifu wao. Kampuni ya Nokia ilikanusha na mambo yaliishia hapo.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" limemnukuu mwanablogger mmoja wa Kenya akisema kuwa Waafrika wanavumbua, lakini ni wengine wanaonufaika.

Mwandishi:Mtullya Abdu

Mhariri:Yusuf Saumu