1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika mkutano wa kilele wa G8

Dittrich / Oummilkheir25 Aprili 2007

Jinsi mataifa tajiri kwa viwanda yanavyofikiria kulisaidia bara la Afrika

https://p.dw.com/p/CB4T
Kansela Merkel akizungumza na Tony Blair na Kofi Annan mjini Berlin
Kansela Merkel akizungumza na Tony Blair na Kofi Annan mjini BerlinPicha: AP

Kansela Angela Merkel aliwakaribisha wageni wawili jana:waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan anaeongoza hivi sasa kamisheni iliyoundwa hivi karibuni ya “Maendeleo barani Afrika.”Na hiyo hasa ndio mada iliyojadiliwa na wanasiasa hao watatu-yaani jinsi nchi za viwanda vinavyobidi na zinavyostahiki kulisaidia bara la Afrika.

Waziri mkuu wa Uengereza alikua wa mwanzo kubuni fikra hiyo:Miaka miwili iliyopita Tony Blair alipowakaribisha viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda, suala la kupigwa vita umaskini barani Afrika lilikua juu kabisa katika orodha ya masuala yaliyojadiliwa katika mkutano wa kilele wa Gleneagles - Scottland.

Wiki chache kutoka sasa itakua zamu ya kansela Angela Merkel kuwakaribisha viongozi wa mataifa saba tajiri kwa viwanda pamoja na Urusi-G-8 huko Heiligendamm.Na katika ajenda ya mazungumzo yatakayoongozwa na kansela Angela Merkel pia,bara la Afrika linakamata nafasi ya juu kabisa.

Ndio maana ameridhika na kushukuria,amesema waziri mkuu Tony Blair,aliemsifu kansela Angela Merkel,mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya mataifa tajiri kwa viwanda G-8.Suala hapa sio la maadili,ni suala la masilahi ya Ulaya amesema waziri mkuu huyo wa Uengereza na kusisitiza:

“Kila nnapoangalia kinachotokea Afrika na hasa katika maeneo ya mizozo mfano Somalia au Sudan,ndipo nnapozidi kuamini,tunapaswa naa tunastahiki kuwajibika kwa muda mrefu barani Afrika.La sivyo, madhara yake tutayaona mpaka huku Ulaya, ikiwa ni pamoja na balaa la umasikini,mikururo ya wakimbizi na kuenea visa vya kigaidi .”

Kansela Angela Merkel anakubaliana moja kwa moja na mgeni wake,na kusema mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kwa viwanda G-8 mwezi Junee ujao unabidi uzipe msukumo wa aina mpya juhudi za kulisaidia bara la Afrika.

Katika mkutano wa kilele wa Gleneagles,miaka miwili iliyopita,viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda walipitisha mpango wa kivitendo kwa Afrika-mpango unaozungumzia miongoni mwa mengineyo juu ya kuongezwa mara dufu misaada ya maendeleo hadi dala miliadi 50 hadi ifikapo mwaka 2010.Zaidi ya hayo viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda wamekubaliana kuziondolea mzigo wa madeni –kitita cha dala miliadi 40,nchi masikini kabisa za dunia.

Lengo la misaada kwa Afrika limeshawekwa,anasema kansela Angela Merkel:

„Hivi sasa,kinachohitajika ni kuutumia wakati ulioko ili kutia njiani hatua zinazohitajika kuweza kulikamilisha lengo hilo.Inamaanisha,tunabidi tuwe tumeshayakamilisha baadhi ya mambo hadi ifikapo mwaka 2010 na baadae katika mwaka 2015.Kwa hivyo tunabidi tufanye kila la kufanya ili mambo yasizorote,tusije baadae,katika mwaka 2008 au mwaka 2009 tukajikuta tukisema ,kwa bahati mbaya hakuna wakati.“

Mgeni wa pili aliyekaribishwa na kansela Angela Merkel jana mjini Berlin ni katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan.Amefurahishwa sana na matamshi ya kansela seuze tena masaa machache tuu kabla ya hapo alichaguliwa kua mwenyekiti wa kamisheni mpya ya maendeleo barani Afrika.Kofi Annan ameutolea mwito Umoja wa Ulaya akisema.

„Nnapata moyo ninapotupia jicho mradi wa kusisimua wa Umoja wa ulaya.Hii leo kuzuka vita barani Ulaya si jambo linalowezekana hata kidogo,japo kama ni katika bara hili hili ambako vita viwili vikuu vya dunia vilikoanzia. Nnataraji, itafika siku ambapo wanangu au wajukuu zangu wataweza kusema „vita si jambo linalowezekana kutokea hata kidogo barani Afrika.“

Kamisheni ya maendeleo ya Afrika,inaoyoongozwa na Kofi Annan imepania kuhimiza mdahalo kati ya viongozi wa serikali za Afrika na jumuia ya kimataifa