1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yapoteza matumaini ikiadhimisha siku ya uhuru

Admin.WagnerD27 Aprili 2016

Afrika Kusini yasheherekea siku ya uhuru Aprili 27. Ikiwa inaadhimisha uchaguzi wa mwanzo, uliomaliza utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994. Huku chama tawala ANC, kikiwa kinakabiliana na upinzani mkubwa nchini humo

https://p.dw.com/p/1IdL8
Südafrika Kapstadt Jacob Zuma Präsident
Picha: Reuters/M. Hutchings

Mnamo tarehe 27 Aprili mwaka 1994, Afrika Kusini ilifanya uchaguzi wake wa mwanzo uliozishirikisha jamii zote za nchi bila ya kujali ukabila wala rangi. Kila raia alikuwa na haki sawa ya kupiga kura. Nelson Mandela alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo, kwa asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa akiwa ndio mgombea wa tiketi ya chama cha ANC.

Miongo miwili baade, chama cha ANC bado ndicho kinachotawala Afrika Kusini. Na ingawa Rais wa sasa Jacob Zuma bado amesalia kuwa na umaarufu miongoni mwa wafuasi wa chama hicho, lakini amekuwa akikabiliana na upinzani mkubwa katika miezi ya hivi karibuni. Madai makuu yakiwa ni rushwa, pamoja na kutumia fedha za umma kukarabati nyumba yake binafsi ya Nkandla.

Raia wengi wa Afrika Kusini wameshaanza kukata tamaa, na kuwa na wasiwasi mkubwa na kule inapoelekea nchi yao. Huku matatizo mbalimbali yakiwa ndio sehemu ya maisha yao ya kila siku.

"Bado hatuna uhuru wa kiuchumi na tunasema tushapata uhuru wa kisiasa," amesema Bongamisu Shangase mkaazi wa mji wa Durban. "Lakini mambo bado sio sawa, watu bado maskini, bado wanaendelea kuteseka, bado wanaishi katika vibanda, huku rais wa nchi anaishi katika nyumba yenye thamani ya dola milioni 17."

Madai ya rushwa dhidi ya serikali, yanakuja wakati ambapo uchumi wa nchi ukiwa unaanguka. Sarafu ya rand ya Afrika Kusini, imekuwa katika kiwango cha chini cha fedha kwa zaidi ya muongo mzima sasa.

Wengi pia wanadai kuwa huduma za umma, kama vile huduma za afya na elimu zimekuwa zikizorota. Hali hii inawaathiri zaidi watu wenye kipato cha chini, pamoja na wale wasiokuwa na ajira.

Maandamano siku ya uhuru

Protest Jacob Zuma Südafrika Cape Town African National Congress ANC
Raia wa Afrika Kusini wakiandamana dhidi ya chamacha ANC mjini Cape Town, Febuari 2016Picha: picture-alliance/dpa

Halikadhalika kuna wasiwasi juu ya ongezeko la ukosefu wa ajira. Na wengi wanasema utendaji kazi wa rais Zuma, ndio chanzo cha kuwepo kwa uwekezaji mbovu wa kiuchumi nchini humo.

Mark Heywood wa shirika la kitengo cha 27, anasema maandamano yaliyopangwa kufanyika siku hiyo ya uhuru, yataonyesha dhahiri namna gani raia wa Afrika Kusini wamekata tamaa na utendaji kazi wa baadhi ya vingozi wa serikali ya nchi hiyo.

"Watu wana hasira. Wanahisi raisi wao anawaonesha dharau. Wanahasira pia kutokana na hali mbaya ya maisha. Njaa, ukosefu wa ajira na elimu duni ni matatizo yanayozidi kuwa mabaya kila siku," Heywood amesema.

Malema kuchunguzwa

Südafrika Jullius Malema Zuma Anklage Debatte
Julius Malema kiongozi wa chama cha upinzani cha EEFPicha: picture-alliance/dpa/N.Bothma

Wakati huohuo polisi nchini humo wamesema watanfungulia uchunguzi kiongozi wa upinzani Julius Malema, kwa kile walichokiita "kauli ya uchochezi" wakati wa mahojiano ya televisheni amabpo anadaiwa kutishia kuiondoa serikali iliyopo madarakani ya Zuma kwa kutumia njia za nguvu.

Tumebaini kwa wasiwasi mkubwa kauli za uchochezi zinazohusishwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa, " amesema mkuu wa polisi Nathi Nhleko akiwa anazungumza na waandishi habari.

Malema ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF), alizungumza na televisheni ya Al Jazeera na kusema, aghlabu maandamo yanayoandaliwa na chama chake huvunjwa na vikosi vya usalama.

"Tunaelekea kupoteza subira na kitakachofuata ni kuiondoa serikali hii iliyopo madarakani kwa mtutu wa bunduki," amesema Malema

Mwandishi: Ole Tangen Jr.

Tafsiri: Yusra Buwayhid

Mhariri: Yusuf Saumu