1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini kujitoa katika mahakama ya ICC

Mjahida13 Oktoba 2015

Chama tawala Afrika Kusini ANC kinaitaka nchi hiyo kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu ICC. Chama hicho kimesema mahakama hiyo imepoteza muelekeo na haiwezi tena kutimiza wajibu wake.

https://p.dw.com/p/1GnBm
Majaji wa Mahakama ya uhalifu ya ICC mjini The Hague
Majaji wa Mahakama ya uhalifu ya ICC mjini The HaguePicha: AP

Umuzi huo umetolewa baada ya mkwaruzano na mahamaka hiyo ilioko mjini The Hague kufuatia Afrika Kusini, kushindwa kumkamata rais wa Sudan Omar al Bashir alipowasili nchini humo mwezi Juni mwaka huu alipohudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika.

Bashir anasakwa na mahakama ya ICC kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita unaohusishwa na mgogoro wa Darfur nchini Sudan.

"Baraza la kitaifa la Afrika Kusini limeamua kuwa Afrika Kusini inapaswa kujitoa katika Mahakama ya ICC lakini hilo litafanyika tu baada ya sisi kufuata hatua kadhaa," alisema Obed Bapela, anayeongoza tume ya mahusiano ya Kimataifa ndani ya chama tawala.

Hata hivyo chama hicho African National Congress ANC kinasema bado inaamini kanuni zilizoundwa na ICC kwa mfano kuzuwiya mauaji ya halaiki na kukomesha ukiukwaji wa haki za binaadamu na kwamba kanuni hizo ndizo zilizoifanya Afrika kusini kujiingiza katika mkataba wa Roma unaounda mahakama hiyo ya Kimataifa, Lakini Bapela amesema mahakama hiyo kwa sasa imekosa muelekeo.

Rais wa Sudan Omar el Bashir
Rais wa Sudan Omar el BashirPicha: Reuters/S. Sibeko

Afrika Kusini ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza za Afrika kutia saini mkataba na ICC mwaka wa 2002. Aidha chama tawala cha ANC kimesema kuna mataifa mengine ambayo sio mwanachama wa mahakama hiyo lakini wanaonekanakuwa na mamlaka ya kupeleka mambo katika mahakama hiyo. Marekani ni moja ya nchi ambayo haikutia saini mkataba w aroma unaounda mahakama ya ICC.

Bapela ameongeza kuwa sababu ya hatua iliyochukuliwa na Afrika Kusini ni lazima iwasilishwe kwa mataifa mengine barani Afrika.

Mahakama ya ICC yasema Ombi la Umoja wa Afrika litasaidia

Wakati hayo yakijiri mahakama hiyo ya ICC imeupa Umoja wa Afrika wiki moja kuwasilisha maombi yalio na utata kuridhia ushahidi uliokuwa umekataliwa. Ibara hiyo ya 68 ilitumika kuridhia ushahidi uliobadilishwa katika kesi dhidi ya makamu wa rais wa Kenya William Ruto.

Makamu wa rais wa Kenya William Ruto
Makamu wa rais wa Kenya William RutoPicha: Michael Kooren/AFP/Getty Images

Lakini katika uamuzi kama huo jaji wa mahakama ya rufaa ya ICC Piotr Hofmanski ilikataa ombi la Kenya Uganda na Namibia, zilizoiandikia mahakama hiyo juu ya namna inavyoitumia ibara hiyo ya 68, kitu ambacho kimesababisha hisia tofauti miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. ICC imeupa Umoja huo wa Afrika wiki moja kuwasilisha ombi juu ya takwa lake kuhusiana na suala hilo.

Kwa upande wake Jaji Hofmanski ameridhika kwamba ombi la Umoja wa Afrika kuwasilisha maombi kama rafiki wa mahakama hiyo katika kesi dhidi ya William Ruto na muandishi habari Joshua Arap Sanga itasaidia.

Jaji huyo amesema maombi hayo yatasaidia mahakaa ya rufaa kuona iwapo majaji wanaoendesha kesi hiyo wanaitumia ibara hiyo kama inavyotakiwa na mahakama ya ICC.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Daily Nation

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman