1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kusini,Somalia na bei ya Maadini ya Afrika magazetini

9 Machi 2012

Maandamano makubwa ya umma yaliyoitishwa na COSATU nchini Afrika kusini,hali nchini Somalia na biashara ya maadini ya thamani ni miongoni mwa mada za Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii .

https://p.dw.com/p/14IIN
Maandamano ya Afrika kusiniPicha: Reuters

Tuanzie lakini Afrika kusini ambako gazeti la Die Tageszeitung linachambua kuhusu mgomo mkubwa wa aina yake kuwahi kufanyika nchini Afrika kusini tangu miaka kadhaa iliyopita."Fulana nyekundu na bendera za rangi ya manjano dhidi ya Zuma" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo la mjini Berlin inayozungumzia jinsi shirikisho kubwa la vyama vya wafanyakazi vya Afrika kusini-Cosatu na makundi ya mrengo wa shoto walivyofanikiwa kuwaleta pamoja umati wa watu kuandamana dhidi ya mwenyekiti wa chama tawala cha ANC,Jacob Zuma.Hata kiongozi aliyefukuzwa wa kundi la vijana la ANC,Julius Malema alishiriki katika maandamano hayo ,linaandika gazeti la die Tageszeitung linaloeleza jinsi eneo la kati la mji wa Johannesburg lilivyogeuka "bahari ya umati wa watu waliovalia mashati mekundu,maelefu wakiongozana wakipepea bendera za rangi ya manjano na mabango yaliyokosoa malipo kwa wenye magari wote wanaotumia barabara kuu mpya.Wakati huo huo wanaandamana dhidi ya mikataba ya muda mfupi na ambayo kwa maoni yao,wanahisi si ya haki."Ni mtindo wa utumwa mambo leo" .Gazeti hilo limewanukuu waandamanaji hao waliokuwa wakicheza ngoma za kienyeji majiani wakisema.Njia zilifungwa na polisi wakitumia mabomba ya maji kuwatawanya waandamanaji-Maduka yamefungwa kwa hofu yasije yakaporwa.Hata hivyo gazeti linaendelea kuandika maandamano hayo yanayotajikana kuwa makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Afrika,yalipita kwa amani.

Katika wakati ambapo shirikisho la vyama vya wafaanyakazi wa Afrika kusini COSATU linajisifu na kusema zaidi ya waandamanaji laki mmoja waliteremka majiani,waajiri wanayakosoa maandamano hayo na kusema mikataba ya muda mfupi ni muhimu kwa sababu bila ,ya mikataba kama hiyo,idadi ya wasiokuwa na kazi nchini Afrika kusini ingepindukia kiwango cha sasa cha asili mia 24.Linamaliza kuandika gazeti la Die Tageszeitung.

Somalia Soldat von AU in Mogadischu
Mwanajeshi wa Uganda wa kikosi cha Umoja wa Afrika akipiga doria mjini MogadishuPicha: AP

Somalia pia imemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani katika kipindi cha wiki hii inayomalizika.Lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine lililomulika hali katika nchi hiyo ambayo gazeti linasema ni kitambulisho cha nchi iliyofeli na zahama za wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam.Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaendelea kuandika kwamba Mogadischu ni tathmini ya matumizi ya nguvu ya koo zinazohasimiana na makundi ya wanamgambo.Gazeti linazungumzia ndege ya shirika la ndege la Uturuki iliyotuwa mjini Mogadischu.Ni ndege ya kwanza ya kimataifa kutuwa katika uwanja huo tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita.Shirika la ndege la Uturuki,linaendelea kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine limedhamiria kuuhudumia mji huo.Kama dhamiri hizo zitaleta tija ni suala la kusubiri na kuona.Hata hivyo Frankfurter Allgemeine linasema hali imeanza kurejea kuwa salama,wanamgambo wa itikadi kali wamerejea nyuma na vikosi vya Umoja wa Afrika vimepanua uwanja wa shughuli zao.Ni jambo la maana linalostahiki sifa na kuendelea kuungwa mkono kwa hali na mali,linahisi gazeti la Frankfurter Allgemeine linalomalizia kwa kuelezea jinsi Uturuki inavyojijenga barani Afrika.

Goldmünzen in Schatztruhe
Mapeni ya dhahabuPicha: mdi/Fotolia

Lilikuwa gazeti hilo hilo la Frankfurter Allgemeine lililoandika pia kuhusu biashara ya maadini ya thamani katika masoko ya dunia."Shaghla Baghla katika soko la maadini ya thamani ulimwenguni" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalozungumzia jinsi bei ya maadini ya platin au dhahabu nyeupe ilivyo rahisi kulinganisha na ile ya dhahabu ya rangi ya manjano katika wakati ambapo maadini ya platin ni adimu.Hata kumalizika ugonvi uliosababisha damu kumwagika katika migodi mikubwa kabisa ya maadini ya platin ulimwenguni hakujasaidia kubadilisha hali ya mambo linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.Hapo gazeti linazungumzia mvutano uliozuka mwezi uliopita katika mgodi wa Impala Platinum nchini Afrika kusini.Wachimba migodi 5000 walipogoma bei ya Platin ilipanda kwa asili mia 20 kwa muda,lakini mgomo ulipomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita bei hiyo ikaporomoka kwa asili mia 10 na kubakia dala 1631 kwa kila wakia moja.Wakati huo huo dhahabu inagharimu dola 1685 kwa wakia moja.

.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Presedatenbank

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman