1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Wiki hii katika Magazeti ya Ujerumani

Miraji Othman27 Novemba 2009

Yasemavyo magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

https://p.dw.com/p/Kjjv
Wakimbizi kutokana na mapigano ya Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi KongoPicha: dpa

Hamna mahala duniani ambako Umoja wa Mataifa umezubaa sana kama katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika. Pale wanamgambo wa Kihutu mwaka 1994 walipowachinja mamia kwa maelfu ya Watusi, wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wanalinda amani huko Rwanda waliamriwa wasifanye kitu. Na kwa miaka kadhaa sasa wako wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, lakini wanajeshi hao hawajaweza kuvimaliza vita vya kikatili katika nchi hiyo, na ambavyo wale wauaji wa halaiki wa Rwanda wanatoa mchango mkubwa.

Kwa mujibu wa gazeti la TAGESZEITUNG linalochapishwa katika mji mkuu wa Berlin, sasa mabingwa wa masuala ya vikwazo kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameweka mambo wazi. Ni kwamba licha ya maazimio yote ya vikwazo na hatua za mapambano ya kijeshi katika vita hivyo, wanamgambo wa Kihutu wa kutokea Rwanda wanasaidiwa na nchi zenyewe zilizo wanachama wa Umoja wa Mataifa. Wanamgambo wa Kihutu wa Chama cha FDLR wanasafirisha dhahabu hadi Ubelgiji, kupitia Dubai, na wanajipatia silaha kutoka Ulaya Mashariki. Fedha zinazopatikana hufanyiwa biashara kwa njia isiokuwa ya halali, kwa sehemu nchini Ujerumani, ambako pia kwa njia ya simu maelekezo hutumwa hadi kwenye medani ya vita. Ufaransa inawahifadhi wakuu wa wanamgambo, nazo Spain na Ubelgiji zina mitandao ya misaada ya kifedha ya wanamgambo hao.

Baraza la Usalama linataka kuweka hadharani ukweli huo wa mambo. Lakini unaweza, kutokana na aibu hiyo, ukaibakisha ripoti yake kwenye mashubaka. Hata hivyo, mwishowe umeonekana ukubwa wa tatizo lenyewe. Hamna nchi yeyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa ilio na usemi ambayo ni safi, na hakuna yeyote kati ya nchi hizo ambayo inataka kurusha jiwe la kwanza. Lakini kunyamaa kimya kabisa kutamaanisha kusalimu amri mbele ya vita vinavojiri barani Afrika na kutapakaa kwake. Mtu anaweza kutaraji kwamba kuchapishwa huku mapema kusikopangwa kwa matukeo muhimu ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kutazuwia hali hiyo kutokea.

Gazeti hilo la TAGESZEITUNG linasema kwamba hapa Ujerumani yuko kizuizini kiongozi wa FDLR, Ignace Murwanashyaka, na bila ya ushirikiano wa kimataifa haitowezekana katu kupata uwazi juu ya uhalifu wa kivita na kuuzuwia. Hatua gani ya kurejea nyumam itakuwa ikiwa kikundi cha mabingwa wa kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa kitawekewa mbinyo?

Usawa wa kijinsia unaozungumziwa bado sana kufikiwa. Hivyo ndivyo alivosikitika Karin Nordmeyer, kiongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake hapa Ujerumani. Kampeni ya mfuko wao, iliopewa jina la wanawake wanatoa malengo manane, kumaanisha yale malengo muhimu manane ya milinium yaliowekwa na Umoja wa Mataifa kufikiwa mwaka2015. Gazeti la Bonn la General Anzeiger liliandika kwamba jumatano wiki hii, katika jengo la makumbusho mjini Bonn, zilimalizika sherehe za kutoa zawadi za Mfuko huo wa Maendeleo ya Wanawake katika Ujerumani. Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa: kuimarisha haki za wanawake. Zawadi ya Euro 10,000 zilipewa jumuiya ya Ghana inayoitwa ABANTU kwa ajili ya Maendeleo, kutokana na mradi wake ulio na jina: Ilani ya Wanawake kwa ajili ya Ghana. Jumuiya hiyo ilipendekezwa na Wakfu wa Kijerumani wa Friedrich-Ebert, na ni ya makundi ya akina mama, vyama vya kisiaasa na wabunge. Bibi Hamida Maalim Harrison, alikabidhiwa zawadi hiyo kwa niaba ya jumuiya hiyo. Yeye alifurahi kusema kwamba moja ya malengo yaliowekwa na jumuiya yake yanatekelezwa, kivitendo. Zawadi ya pili ilikwenda kwa ajili ya mradi wa kuwashauri wanawake wa jumuiya ya Peru inayoshirikiana na Shirika la kupamnana na njaa duniani. Jumuiya hiyo inatoa mafunzo katika maeneo ya milima ya Andes na mjini Lima kuwaelimisha wanawake juu ya haki zao yanapokuwa masuala ya matumizi ya nguvu katika familia na ubakaji. Mratibu wa jumuiya hiyo ya Peru, Patricia Zanabriar, alisema Peru imetia saini mikataba mingi juu ya usawa wa jinsia, lakini mikataba hiyo imebakia tu katika karatasi, haiendi na ukweli halisi wa mambo.

Gazeti la Neues Deutschland liliripotio wiki hii juu ya jumuiya ya akina mama huko Senegal, USOFORAL, inayoungwa mkono na Shirika la Dunia juu ya amani. Eneo la Casamance, kusini mwa Senegal, limekuwa halina utulivu. Tangu mwaka 1982 vuguvugu la Nguvu za Kidemokrasia katika Casamance, MFDC, makundi mbali mbali ya waasi na serekali ya Senegal zimekuwa katika mzozo. Kwa sehemu mzozo huo umepelekea mapambano ya kijeshi. Tangu mwaka 2004 mapigano yamesitishwa, lakini kuna hatari kwamba mzozo huo unaweza ukachipuka tena wakati wowote.

Kutokana na matatizo makubwa ya utumiaji nguvu katika shule na jamii, jumuiya hiyo ya USOFORAL ilianza kutoa mafunzo kwa kikundi cha waalimu juu ya kuendesha upatanishi katika mashule. Waalimu hao baadae, bila ya malipo, wanawapa mafunzo waalimu wengine na watoto wa shule juu ya njia za kuleta upatanishi na maelewano. Klabu hizo za upatanishi sasa zimekuwa sehemu muhimu ya majengo ya shule za sekondari. zinakutana kila wakati kuzungumzia matatizo, hatua gani zinazofaa kupendekezwa kuchukuliwa na pia kuwavutia watoto wepya wa shule juu ya fikra ya kuweko mapatano na masikilizano. Mizozo midogo mingine imesuluhishwa kutokana na mradi huo. Katika upatanishi mtu hahukumiwi, lakini suluhisho la kuzuwia kutokea tena mizozo baina ya wanafunzi wenyewe kwa wenyewe na baina ya wanafunzi na waalimu. watu wamefanywa wawe tayari kila mmoja kumsikiliza mwenzake.

Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri: Mohammed Abdulrahman