1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yasaka fursa za kiuchumi kupitia kilimo

Mohammed Khelef
3 Mei 2017

Bara la Afrika linataka kutumia uwezo wake kwenye kilimo kujenga chumi zake na imeitisha kongamano la kimataifa nchini Afrika Kusini kujadili fursa ya kilimo cha  Afrika kwenye Jukwaa la Uchumi Duniani mwezi Juni.

https://p.dw.com/p/2cGii
Burundi Landwirtschaft
Picha: picture alliance/africamediaonline

Afrika ndilo bara lenye kiwango kikubwa kabisa cha ardhi yenye rutuba dunani, lakini halijaweza kukifanya kilimo kuwa na faida, na badala yake mataifa mengi ya bara hilo yamekuwa wategemezi wakubwa wa chakula kutoka nje.

Jambo la kusikitisha ni kuwa wakati yenyewe inaagizia chakula kutoka nje, nayo pia husafirisha takribani asilimia 80 ya chakula chake, huku ikitumia zaidi ya dola bilioli 70 kila mwaka kwenye vyakula vinavyoliwa sana huko, kama vile mahindi, ngano, mchele, maharage na maziwa, kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.

Kuinua mazao ya kilimo cha Afrika ndio maudhui makubwa ya mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi Duniani unaofanyika mjini Durban, Afrika Kusini, mwanzoni mwa mwezi ujao wa Juni.

"Kuna eneo pana sana la uwekezaji katika kilimo na usindikaji wa bidhaa za kilimo, ambao unaweza kuzibadilisha kabisa chumi zinazorota barani Afrika," anasema Profesa Nick Kotze wa Chuo Kikuu cha Stellenbosch cha Afrika Kusini, ambaye pia anaonya kuwa "serikali za Afrika zenyewe ndizo zinazopaswa kuchukuwa juhudi kubwa ya kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya vile vya kigeni."

Nigeria yataka kuwa mzalishaji mkubwa wa mchele

Bildergalerie Millionäre Afrika - Aliko Dangote
Bilionea wa Kinigeria, Aliko Dangote, anataka kuigeuza nchi yake kuwa mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa mchele ndani ya miaka mitano ijayo.Picha: picture-alliance/dpa/B. Von Loebell/World Eco

Nigeria, taifa kubwa kabisa kwa uzalishaji mafuta barani Afrika, linataka sasa kuuchawanya uchumi wake na kuwa msafirishaji mkubwa kabisa wa mchele ndani ya miaka mitano ijayo, kwa msaada wa tajiri mkubwa kabisa barani humo, mjasiriamali wa Kinigeria, Aliko Dangote.

Dangote, ambaye jarida la Forbes linasema utajiri wake sasa unafikia dola bilioni 12.2, aliahidi kuwekeza dola bilioni moja kwenye kilimo na usindikaji wa mpunga, kwa ajili ya kuwalisha Wanigeria na kuongeza mapato ya nje.

"Kwenye suala la mchele, kwa sasa asilimia mia moja tunachukuwa kutoka kwa wakulima wa kawaida. Kawaida walikuwa wakipata tani mbili za mpunga kwa hekta, sasa sisi tumebadilisha iwe tani nane kwa hekta. Tunawapa wakulima mbegu, mbolea na madawa, na wao wanatuuzia mpunga kwa bei ya sokoni. Tunawaambia ikiwa wanaona bei yetu ni ya chini, wako huru kwenda kuuza kwengine na kuturejeshea gharama zetu tu," alisema Dangote kwenye mkutano wa Taasisi ya Mo Ibrahim mjini Marrakech mwishoni mwa mwezi Aprili.

Umoja wa Ulaya ni msafirishaji mkubwa wa chakula kwa Afrika, inakokiuza kwa thamani ya dola bilioni 20 kila mwaka, kwa mujibu wa takwimu za Kamisheni ya Ulaya. Ruzuku huwaruhusu wakulima kwenye Umoja huo kuuza bidhaa zao za kilimo kwa bei ambayo haijumuishi gharama za uzalishaji. 

Lakini sehemu kubwa ya vyakula hivyo - unga wa ngano, maziwa ya unga, nafaka, mafuta ya kupikia, mbogamboga na nyama ya kuku - vinaweza kupatikana kirahisi barani Afrika kwenyewe, isipokuwa mikataba ya kibiashara isiyo na uwiano inawapa wakulima wa Ulaya fursa kubwa zaidi kuliko wenzao wa Afrika, kwa mujibu wa FAO.

Mikataba ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na baadhi ya mataifa ya Afrika, Karibian na Pasifiki maarufu kama EPA, inaupa Umoja huo hadi asilimia 83 ya soko rahisi la Afrika. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Caro Robi