1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yasalia nyuma maendeleo ya binaadamu

Admin.WagnerD13 Agosti 2014

Mizozo na mikasa ya asili imetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia kuzorota kwa maendeleo ya binadamu duniani huku mataifa ya kusini mwa jangwa la sahara yakiathirika zaidi.

https://p.dw.com/p/1Cu3Q
Wahlen in Lesotho Afrika
Picha: DW/Poppendieck

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya ustawi wa maendeleo ya mwaka 2014 iliyozinduliwa Jumatano mjini Nairobi na Shirika la Ustawi wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP. Mataifa ya Kanda ya Afrika ya Mashariki na Kati ni miongoni mwa nchi zilizoorodheshwa kuwa na viwango vya chini vya ustawi wa maendeleo.

Ripoti hiyo ambayo kauli mbiu yake ni "Kuimarisha ustawi wa binadamu: Kupunguza athari na kudumisha ukuaji," imeorodhesha nchi 187 huku mataifa ya Afrika Mashariki na Kati yakiwa miongoni mwa mataifa 40 yaliyo na kiwango cha chini cha ustawi wa maendeleo. Kenya imeshika nafasi ya 147, Rwanda nafasi ya 151,Tanzania 157, Uganda 164, nayo Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa nafasi ya 186.

"Mizozo, ghasia, vita na ukame ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuzorota kwa maendeleo," alisema Roba Sharamo, mkuu wa kitengo cha Kudumisha amani na kuzuia mizozo katika shirika la UNDP, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Zaidi ya watu nusu bilioni duniani wako katika hatari ya kuathiriwa na mizozo huku milioni 200 wakiishi katika viwango vya umasikini kupindukia. Juhudi ambazo zinahitajika kufanywa ni kuhakikisha watu wanaojinasua kutoka kwa umasikini hawarudi tena katika hali hiyo.

Ramani inayoonyesha maendeleo ya binaadamu, ambapo nyekundu inawakilisha mataifa yaliyo na maendeleo kiduchu.
Ramani inayoonyesha maendeleo ya binaadamu, ambapo nyekundu inawakilisha mataifa yaliyo na maendeleo kiduchu.

“Hatupaswi tu kushukisha viwango vya umasikini bali tunapasa kuhakikisha wale wote wanaoondoka kutoka kwa umasiki wanasaidiwa wasirudi tena katika umasikini,” alisema Stephen Wainaina, katibu wa mipango ya kiuchumi katika wizara ya Fedha nchini Kenya.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwepo kwa mifumo bora ya maongozi hasa kisiasa kuhakikisha sera zinazobuniwa zinazingatia ukuaji wa maendeleo kwa watu wote. Nados Bekele Thomas, mwakilishi wa shirika la Ustawi wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Kenya anasema siasa zinazozingatia raia ni muhimu kwani mikakati yote inayofanywa na wanasiasa inatekelezwa kutilia maananni raia.

"Na ikiwa siasa hazijali maslahi ya wote nasi inaiweka nchi katika hatari ya kuanguka kutokana na mikukumo ya nje.”

Huku utandawazi ukitarajiwa kuleta maendeleo kigezo hicho kimeonekana kupeta athari za kudororra kwa uchumi na kusababiusha uhaba wa chakula. Ustawi wa maendeleo ya binadamu sio tu ukuaji wa uchumi bali urahisi wa kupatikana kwa huduma za kijamii kama vile huduma za afya, elimu na usalama.

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Josephat Charo