1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFROPRESS

Kitojo, Sekione25 Julai 2008

Mandela atimiza miaka 90, Bashir kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, na Mugabe kuzungumza na hasimu wake ndio mada kuu zilizoandikwa katika magazeti ya ujerumani.

https://p.dw.com/p/EjYy
Nelson mandela Madiba, akiwa na familia yake katika hafla ya sherehe yake ya kuzaliwa , wakati akitimiza miaka 90 tangu kuzaliwa. Happy Birthday Madiba.Picha: picture alliance/dpa


Karibuni wapenzi wasikilizaji katika makala ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani hii leo. Hii ni makala inayohusu yale yaliyojiri katika bara la Afrika na kuandikwa katika magazeti ya Ujerumani.


Tunaanza na gazeti la Die Welt ambalo limezungumzia kuhusu sherehe za kutimiza miaka 90 ya kuzaliwa kwa Nelson Mandela Madiba. Gazeti hilo linaandika katika kichwa chake cha habari kuwa jabali la uadilifu Nelson Mandela latimiza miaka 90 tangu kuzaliwa.

Happy Birthday Madiba , linaadika gazeti la Die Welt, likieleza kuwa mamilioni ya watu wamempongeza Mandela kwa kusherehekea miaka 90 ya kuzaliwa siku ya Jumamosi iliyopita tarehe 18 Julai. Katika maeneo ya viwanda na maofisi, shule na maeneo ya wapitao kwa miguu mijini kila mahali kumekuwa na ishara ya mapenzi na pongezi kwa shujaa huyo aliyeleta amani nchini Afrika kusini.


Nafasi ndogo kwa Zimbabwe : Linaandika gazeti la Berliner Zeitung.

Ni mafanikio madogo kwa upande wa upinzani nchini Zimbabwe. Rais Robert Mugabe analazimika sasa kuzungumza na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kuhusiana na hali ya baadaye ya kugawana madaraka nchini humo.


Gazeti la Zürcher Zeitung kuhusu suala hilo linaandika Mugabe azungumza na hasimu wake. Mbele ya rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki , rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wameahidi mjini Harare kufanya mazungumzo yatakayohusu hali ya baadaye ya nchi hiyo. Katika makubaliano hayo viongozi hao wawili wameweka msimamo wa kuendesha mazungumzo hayo yenye nia ya kutatua mzozo wa kisiasa ambao umetokana na uchaguzi uliofanyika nchini humo ambao haukupata uhalali katika jumuiya ya kimataifa , mwishoni mwa mwezi wa Juni.



Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung, likiandika kuhusu habari hizo limeandika katika kichwa cha habari ; makubaliano kuhusu mazungumzo. Kwa upande wake lakini gazeti la Süddeutsche Zeitung linazungumzia kukaribiana nchini Zimbabwe.

Kukaribiana kwa tahadhari nchini Zimbabwe laandika gazeti la Frankfurter Rundschau.




Gazeti la Der Spiegel linaadika kuhusu kushtakiwa kwa rais wa Sudan katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague. Gazeti la Der Spiegel linaandika kuwa mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita, ndivyo alivyodai mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita Luis Moreno-Ocampo dhidi ya rais wa Sudan Omar al-Bashir. Wakati majaji watakapotoa hati ya kukamatwa , itakuwa mara ya tatu kiongozi wa nchi kupelekwa katika mahakama hiyo ya kimataifa kukabiliana na sheria. Wakwanza alikuwa rais Slobodan Milosevic wa Serbia, Charles Taylor wa Liberia na Omar Hassan al Bashir sasa wa Sudan.


Lakini linaandika gazeti la Neue Zürcher Zeitung kuwa mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya jumuiya ya nchi za Kiarabu katika mkutano wao mjini Cairo wamesema kuwa mashtaka hayo dhidi ya rais al- Bashir ni kwenda kinyume na uhuru wa taifa hilo la Sudan. Wamemtuma katibu mkuu wa umoja huo kwenda Sudan na mpango ambao utahusisha utaratibu wa jumuiya hiyo wa kusuluhisha mzozo huo.

Nae balozi wa Sudan katika umoja wa Afrika ameonya kuwa hati ya kukamatwa kwa rais wa nchi hiyo itahatarisha hatua za kuleta amani na eneo la kusini mwa nchi hiyo, limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung.


Gazeti la Berliner Zeitung linakichwa cha habari kinachosema matarajio yenye hatari.

Linazungumzia mazungumzo yaliyofanyika kuhusiana na mazungumzo ya kibiashara duniani ya shirika la biashara la dunia WTO, mjini Genf nchini Uswisi. Mwakilishi wa India amesisitiza kuliangalia pendekezo la Marekani la dhihaka , la kupunguza ruzuku zinazopewa wakulima kutoka dola bilioni 48,2 kwa mwaka hadi dola bilioni 15 tu kwa mwaka. Ndipo gazeti hilo linatahadharisha kuwa haya ni matarajio ya hatari.


Kwa maoni hayo ya gazeti la Berliner Zeitung ndio tunafikia mwisho wa makala hii ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii.


►◄